Baada ya Serikali ya Zimbabwe kutoa shutuma kali dhidi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, Balozi wa Vatican nchini Zimbabwe ameonesha mshikamano wa Vatican na Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe. Baada ya Serikali ya Zimbabwe kutoa shutuma kali dhidi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, Balozi wa Vatican nchini Zimbabwe ameonesha mshikamano wa Vatican na Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe. 

Sakata Kati ya Kanisa na Serikali Zimbabwe: Mshikamano na Vatican

Askofu mkuu Paolo Rudelli, Balozi wa Vatican nchini Zimbabwe, Jumapili, tarehe 16 Agosti 2020 amemtembelea na kwenda kumsalimia Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu kama kielelezo cha mshikamano wa Vatican kwa Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe. Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu ambaye ndiye aliyeelekezewa “makombora ya mashambulizi” kutoka Serikali ya Zimbabwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika Waraka wa Kichungaji wa Mwezi Agosti, 2020 linayaangalia matukio ya wakati huu, saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, umuhimu wa kuenzi siku ya mashujaa na vikosi vya ulinzi na usalama. Maaskofu wanakazia umuhimu wa mchakato wa mageuzi makubwa kama sehemu ya mapambano dhidi ya umaskini na kwamba, kuna umuhimu wa kuunda jukwaa litakalojadili vipaumbele vya familia ya Mungu nchini Zimbabwe. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linasikitika kusema kwamba, kwa sasa Zimbabwe inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kuna ongezeko kubwa la umaskini wa hali na kipato; kuna ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula. Saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma unaendelea kuwapekenya watu wa Mungu nchini Zimbabwe, kiasi kwamba, haki msingi za binadamu si kati ya vipaumbele nchini Zimbabwe, hali ambayo imepelekea hata baadhi ya viongozi wa Serikali kuanza kutumia madaraka yao vibaya na kusahau utawala wa sheria.

Haya ni matatizo na changamoto zinazohitaji kupewa suluhu ya haraka kabla ya mambo hayajaharibika zaidi. Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe umepelekea shutuma nzito zilizotolewa na Serikali dhidi ya Kanisa Katoliki katika ujumla wake, lakini zaidi dhidi ya Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Paolo Rudelli, Balozi wa Vatican nchini Zimbabwe, Jumapili, tarehe 16 Agosti 2020 amemtembelea na kwenda kumsalimia Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu kama kielelezo cha mshikamano wa Vatican kwa Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe na kwa namna ya pekee kwa Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu ambaye ndiye aliyeelekezewa “makombora ya mashambulizi” kutoka Serikali ya Zimbabwe.

Waziri wa habari na huduma ya mawasiliano Bi Monica Mutsvangwa, Jumamosi, tarehe 15 Agosti 2020 kupitia kwenye Kituo cha Televisheni cha Taifa, alitoa shutuma nzito dhidi ya Kanisa Katoliki na viongozi wake. Waamini wengi wa Kanisa Katoliki na watu wenye mapenzi mema, wengi wao wanaunga mkono Waraka wa Kichungaji Uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe kwamba, ni ukweli usioweza kufumbiwa macho na matokeo yake hali ya watu kutoridhika na uongozi ulioko madarakani kwa sasa. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inashughulikia kikamilifu matatizo na changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii badala ya kutumia nguvu kutaka kuwanyamazisha watu.

Balozi wa Vatican nchini Zimbabwe
18 August 2020, 07:51