Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Mitja Leskovar anatumwa kama mjumbe wa haki, amani na madhiriano kati ya watu wa Mataifa. Askofu mkuu Mitja Leskovar anatumwa kama mjumbe wa haki, amani na madhiriano kati ya watu wa Mataifa. 

Askofu mkuu Leskovar: Mjumbe wa Haki, Amani na Upatanisho Iraq!

Kama Balozi wa Vatican anatumwa kusaidia mchakato wa kulinda na kudumisha utambulisho wa Wakristo huko Iraq, kwa kuendelea kujizatiti katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Askofu mkuu Leskovar anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho wa kitaifa kwa kutafuta na kuambata suluhu makini ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo katika ukweli na uwazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Franc Rodè, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, tarehe 8 Agosti 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu na kumweka wakfu Monsinyo Mitja Leskovar kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Iraq. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicola, Jimbo kuu la Lubiana nchini Slovenia na kuhudhuriwa na watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Slovenia. Kardinali Franc Rodè katika mahubiri yake alikazia kwa namna ya pekee kuhusu: Heri za Mlimani, Sadaka na Majitoleo ili aweze kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa. Katika maisha na utume wake, aoneshe upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na watu wa Mungu watakaokabidhiwa kwake na Mama Kanisa, tayari kulinda, kutetea na kudumisha imani ya Kanisa hata ikimbidi kumimina maisha yake kama wanavyofafanua Baba wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Askofu mkuu Mitja Leskovar alibahatika kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na huo ukawa ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho na mlango unaomwezesha kupata Sakramenti nyingine na hivyo kuendelea kuwa ni sehemu ya viungo vya Kristo na hatimaye, kuingizwa na kufanywa washiriki katika utume wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu, anaingizwa kwenye urika wa Maaskofu ambao kimsingi ni waandamizi wa Mitume wa Yesu na kwa namna ya pekee kabisa anakuwa ni Mwakilishi wa Baba Mtakatifu kwa watu wa Mungu nchini Iraq. Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake kama dira na mwongozo wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kumbe, Askofu mkuu Mitja Leskovar anaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa, kwa njia ya ushuhuda wa matendo yake mema, ili wale wanaoyaona waweze kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Chumvi kadiri ya Maandiko Matakatifu ni kielelezo cha Agano na Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanaingizwa katika Fumbo la Mwenyezi Mungu na hivyo kuwa ni alama ya Agano la milele na waja wake. Wajibu wao msingi ni kuwa mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu uliomiminwa rohoni mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Chumvi ni kwa ajili ya kukoleza, kulinda na kuongeza ladha. Anatumwa kuwa ni mwanga unaongaza utukufu wa Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Hekima ya Mungu, tayari kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kumhudumia mwanadamu: kiroho na kimwili.

Daraja takatifu ya Uaskofu ndani ya Kanisa ni huduma makini kwa ajili ya watu wa Mungu, kwa kuonesha uwepo na ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu, mwaliko na changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Askofu mkuu Mitja Leskovar, kwa mara nyingine tena anaitwa kumpenda Kristo Yesu na Kanisa lake; kumpenda na kuheshimu Khalifa wa Mtakatifu Petro na waamini ambao watakabidhiwa kwake na Mama Kanisa. Familia ya Mungu nchini Iraq ina nafasi ya pekee kabisa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Hawa ni watu wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na vita, njaa na umaskini wa hali na kipato! Ni watu ambao Baba Mtakatifu alitamani kuwatembelea mwaka 2020 ili kuwatia shime, lakini kutokana na sababu mbali mbali hija hii ya kitume kwa sasa, imebaki kama ndoto ya Baba Mtakatifu Francisko.

Kama Balozi wa Vatican anatumwa kusaidia mchakato wa kulinda na kudumisha utambulisho wa Wakristo huko Iraq, kwa kuendelea kujizatiti katika majadiliano ya kidini na kiekumene; katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu mkuu Mitja Leskovar anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho wa kitaifa kwa kutafuta na kuambata suluhu makini ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, ambazo kwa bahati mbaya kabisa, zimeigeuza Iraq kuwa ni uwanja wa vita. Kwa kusaidiana na wadau mbali mbali, wanapaswa kuhakikisha kwamba, Iraq inageuzwa tena na kuwa ni bustani nzuri yenye kuvutia, haki, amani, upendo na udugu wa kibinadamu. Kama Askofu mkuu, atapaswa kuilinda, kuitetea na kuishuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake hadi tone la mwisho la maisha yake, ikibidi. Awe ni mtangazaji mahiri wa Neno la Mungu pamoja na kuhifadhi amana na utajiri wa imani, daima akijitahidi kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ajitahidi kuwa ni kiungo cha umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Anapaswa kuwa ni mchungaji mwema na mwaminifu wa watu Mungu, akionesha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, huku akijitahidi kuwa mwaminifu. Kwa kuwekwa wakfu, amepokea nguvu ya Roho Mtakatifu, anayeliongoza na kulitegemeza Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu aliye Mchungaji wa milele alijenga Kanisa Takatifu, akawatuma Mitume kama waandamizi wao, yaani Maaskofu, wawe wachungaji wa Kanisa lake hata ukamilifu wa nyakati. Kusudi Uaskofu wenyewe uwe mmoja na usiogawanyika, akamweka Mtakatifu Petro juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi udumuo na uonekanao wa umoja wa imani na wa ushirika. Ni katika muktadha huu, Maaskofu wanatambuliwa na Kanisa kama waandamizi wa Mitume kwani wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili kwa ajili ya Kanisa na asili ya maisha na utume wake siku zote. Maaskofu wamekabidhiwa huduma ya jumuiya pamoja na msaada wa Mapadre na Mashemasi, wakiliongoza kundi lake kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, ambalo wao ni wachungaji wake, wakiwa kama walimu wa mafundisho, makuhani wa ibada takatifu, wahudumu wa uongozi. Kimsingi Maaskofu wanao wajibu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. LG, 20.

Basi, katika nafsi za Maaskofu, wanaosaidiwa na Mapadre, yupo kati kati ya waamini Kristo Yesu, aliye Kuhani Mkuu na kwa njia ya huduma yao mashuhuri huyashuhudia na kuyatangazia Mataifa yote Neno la Mungu na kuwapa waamini Sakramenti za imani bila kikomo. Tena kwa uangalifu wao wa kibaba, huviunganisha viungo vipya na Mwili wake kwa kuvizaa upya kutoka juu kwa Maji na Roho Mtakatifu. Kwa  hekima na busara yao hulielekeza na kuliongoza taifa la Mungu katika safari ya kuelekea kwenye heri ya milele. Kumbe, Maaskofu ni watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu nao wamekabidhiwa huduma ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu, na huduma ya Roho na ya haki katika utukufu, daima wakijiweka chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu, anayewajalia ukamilifu wa Daraja Takatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Maaskofu, kwa namna bora na dhahiri, wanashika nafasi ya Kristo Yesu mwenyewe aliye: Mwalimu, Mchungaji na Kuhani Mkuu na hutenda katika nafsi yake “in Eius persona”.

Kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu, huwaingiza wateuliwa wapya katika umoja na Maaskofu. Hurika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Franc Rodè, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Askofu ni kielelezo cha utukufu wa Kanisa la Kristo Yesu. Maisha na utume wake, uwe ni sehemu ya mchakato wa kutafuta: haki, amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Iraq.

Askofu mkuu Leskovar

 

 

11 August 2020, 13:45