Askofu mkuu Mitja Leskovar amewekwa wakfu tarehe 8 Agosti 2020 sasa anatumwa kwenda nchini Iraq kuwa ni chombo na shuhuda wa imani, matumaini na mapendo kati ya watu wa Mungu. Askofu mkuu Mitja Leskovar amewekwa wakfu tarehe 8 Agosti 2020 sasa anatumwa kwenda nchini Iraq kuwa ni chombo na shuhuda wa imani, matumaini na mapendo kati ya watu wa Mungu. 

Askofu mkuu Mitja Leskovar: Shuhuda wa Matumaini Iraq

Nembo yake ni Kiaskofu inapambwa na maneno yafuatayo: “Crux Lignum Vitae” yaani “Msalaba ni Mti wa Uzima”. Hii ni kauli mbiu inayoongoza maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, anapaswa kuungama na kushuhudia ukuu wa Fumbo la Msalaba katika ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Mitja Leskovar aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Iraq, tarehe 8 Agosti 2020 amewekwa wakfu kuwa Askofu mkuu katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Franc Rodè, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na kuadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicola, Jimbo kuu la Lubiana nchini Slovenia. Askofu mkuu Mitja Leskovar alizaliwa tarehe 3 Januari 1970 huko Kranj nchini Slovenia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Juni 1995 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mei Mosi 2020, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Iraq na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu na hivyo kuwekwa wakfu hapo tarehe 8 Agosti 2020, neema ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre inayopata sasa utimilifu wake kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu.

Nembo yake ni Kiaskofu inapambwa na maneno yafuatayo: “Crux Lignum Vitae” yaani “Msalaba ni Mti wa Uzima”. Hii ni kauli mbiu inayoongoza maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, anapaswa kuungama na kushuhudia ukuu wa Fumbo la Msalaba katika ukombozi wa mwanadamu. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kumbe, Fumbo la Msalaba ni kiini na chemchemi ya maisha na uzima wa milele. Askofu mkuu Mitja Leskovar mara baada ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu, amemshukuru Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wale wote waliomsaidia na kumtegemeza katika maisha na utume wake. Wengi walitamani kuhudhuria tukio hili muhimu katika maisha na utume wake kama Askofu mkuu, lakini kutokana na uwepo wa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, wengi hawakuthubutu kwenda kumuunga mkono, lakini wamemsindikiza kwa sala na sadaka zao.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Jean-Marie Speich, Balozi wa Vatican nchini Slovenia na Mwakilishi wa Kitume nchini Kosovo amemshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Mitja Leskovar kwa kukubali kupokea Daraja Takatifu ya Uaskofu na kama Mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro nchini Iraq. Huu ni wito unaofumbatwa katika huduma kwa watu wa Mungu kwa kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza. Kwa kutumia amana na utajiri wa imani na Mapokeo ya Kanisa kutoka Slovania, ataweza sasa kujisadaka bila ya kujibakiza na kuwaendea watu wa Mungu nchini Iraq kama: Mchungaji mwema, Baba mwenye huruma na mapendo, kaka na shuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu. Huu ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, daima akiyaelekeza macho na mawazo yake kwenye Fumbo la Msalaba, mti wa uzima. Roho Mtakatifu awe ni dira na kiongozi wake wa maisha, asindikizwe na kufarijiwa kwa sala za Kanisa na baraka za kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awe ni kimbilio, mlinzi na tunza yake ya daima, ili baada ya maisha ya hapa duniani, aweze kustahilishwa kupata tuzo la maisha na uzima wa milele. Naye, Askofu mkuu Stanslav Zore, OFM, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lubiana nchini Slovenia, amepongeza Askofu mkuu Askofu mkuu Mitja Leskovar kwa kukubali na kutikia wito huu Mtakatifu na sasa anatumwa kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, akianzia nchini Iraq.

Balozi Iraq

 

10 August 2020, 14:02