Waraka: Maagizo: "Wongofu wa kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa. Waraka: Maagizo: "Wongofu wa kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa. 

Waraka: Wongofu wa Kichungaji, Parokia, Huduma ya Uinjilishaji!

Kiini cha Waraka huu ili kudumisha umoja na mshikamano kati ya Parokia mbali mbali kwa kuendelea na mchakato wa upyaisho wa kimisionari, wongofu wa shughuli za kichungaji, ili hatimaye kila mbatizwa aweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Hiki ni chombo cha kisheria na mwongozo wa shughuli za kichungaji, kama chachu ya upyaisho wa Parokia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, tarehe 29 Juni 2020 limechapisha Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa”. “Instruction: The pastoral conversion of the Parish community in the service of the evangelising mission of the Church.”. Waraka huu unajikita katika tema ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Jumuiya ya Kiparokia kwa ushiriki mkamilifu wa: wakleri, watawa na waamini walei, kama kielelezo makini cha wajibu wa wabatizwa wote. Mama Kanisa anawakumbusha waamini wote kwamba, ndani ya Kanisa kila mtu anayo nafasi, dhamana na kwamba, wanawajibika kikamilifu kama watu wa familia ya Mungu, kwa kuheshimu wito wa kila mbatizwa. Hiki ndicho kiini cha Waraka huu ili kudumisha umoja na mshikamano kati ya Parokia mbali mbali kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa upyaisho wa kimisionari, wongofu wa shughuli za kichungaji, ili hatimaye kila mbatizwa aweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo.

Waraka huu ni matunda ya changamoto iliyotolewa na sehemu kubwa ya Maaskofu mahalia, ili kuliwezesha Kanisa kuwa na chombo cha kisheria pamoja na mwongozo wa shughuli za kichungaji, kama chachu ya upyaisho wa Jumuiya ya Kiparokia unaopaswa kufikia kilele chake katika maisha na utume wa Majimbo mahalia ambayo kwa sasa yanaendelea kupyaishwa ili kudumisha umoja na mshikamano katika kanda za kichungaji. Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” umegawanyika katika Sura 11, lakini unaweza kufupishwa na kugawanywa katika sehemu kuu mbili yaani: Sura ya Kwanza hadi Sura ya sita. Hapa, Waraka  unajadili kuhusu wongofu wa kichungaji, maana ya umisionari na tunu msingi za maisha ya Parokia katika ulimwengu mamboleo. Sehemu ya Pili ni kuanzia Sura ya Saba hadi Sura ya Kumi na moja. Hapa Waraka unajikita katika mchakato wa mgawanyo wa Parokia, dhamana na nyajibu mbali mbali ndani ya Parokia na jinsi ya kutekeleza sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa.

Parokia ni alama muhimu inayoonesha uwepo endelevu wa Kristo Mfufuka kati ya waamini wake. Kumbe, Parokia ni nyumba kati ya nyumba zilizopo na umuhimu wake unajikita katika mchakato wa uinjilishaji. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kidigitali, yameleta mabadiliko makubwa, kiasi kwamba, mahusiano na mafungamano ya kijamii ni muhimu sana. Ni katika muktadha huu, Parokia inapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, kwa kusoma alama za nyakati na kuendelea kupyaisha huduma zake kwa waamini na katika historia. Upyaisho wa huduma Parokiani hauna budi kujikita katika miundombinu ya kimisionari iliyoko Parokiani. Huu ni mwaliko wa kujikita zaidi katika masuala ya maisha ya kiroho na wongofu wa kichungaji unaokita mizizi yake katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni wasanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Ni kwa njia ya huduma makini kwa maskini, Parokia inageuka kuwa ni chombo cha uinjilishaji, tayari pia kutoa nafasi ili iweze kuinjilishwa na maskini! Kila mbatizwa Parokiani anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Hapa wanaparokia hawana budi kubadili mawazo kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kweli mageuzi ya kimisionari katika shughuli za kichungaji yaweze kutekelezwa. Huu ni mchakato unaopaswa kufanyiwa tafakari ya kina na hivyo kuruhusu kwenda hatua kwa hatua, ili kuweza kukita mizizi yake katika maisha ya wanajumuiya, bila “shuruti kutoka juu”, kwani hii ni huduma ya kichungaji. Mgawanyo wa Parokia: Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” katika sehemu hii, unakazia umuhimu wa kuzingatia ujirani katika mchakato wa kugawanya au kuunganisha Parokia. Mchakato uzingatie tabia za watu mahalia na mazingira yao. Viongozi watakaoteuliwa wawe kweli ni chachu ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu kama inavyopaswa kuwa kwa ajili ya Kanda za Kichungaji. Paroko ndiye mchungaji mkuu wa Jumuiya ya Parokia, anayepaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaongoza watu wa Mungu. Kimsingi, Paroko lazima awe ni Padre aliyepewa Daraja Takatifu ya Upadre na wala si vinginevyo!

Paroko ni msimamizi halali wa mali ya Parokia na ni mwakilishi wa Parokia kisheria. Maaskofu Jimbo wanapowateua Maparoko wapya, wawapatie muda wa kutosha ili kuwafahamu wanaparokia wao na hivyo kuonesha ukaribu wao. Kimsingi, Paroko anaweza kuongoza Parokia kwa muda usiopungua miaka mitano. Kwa Maparoko ambao wametimiza miaka 75 ya kuzaliwa, wanao wajibu wa kimaadili, kuomba ruhusa kutoka kwa Askofu Jimbo, ili kung’atuka kutoka madarakani. Paroko ataendelea kukaa madarakani, hadi pale, Askofu Jimbo atakapomjibu kwa maandishi! Jambo la msingi ni kuondokana na dhana ya kudhani kwamba, “Mapadre ni wafanyakazi wa mshahara”.

Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo na ni vyombo na mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa, shuhuda na chombo cha huduma ya Injili ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Pia Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa kadiri ya Sheria, taratibu na miongozo ya Kanisa. Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu pamoja na Mapadre; wamewekwa wakfu kwa ajili ya kuinjilisha katika huduma; kwa kusimamia mali za Kanisa na kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Ni wahudumu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kamwe Mashemasi “si watu wa mshahara” anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Ushuhuda wa watawa na dhamana ya upendo na ukarimu inayotekelezwa na waamini walei. Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unawakumbusha watawa kwamba, uwepo wao Parokiani unapaswa kuwa ni ushuhuda wa wafuasi wa Kristo Yesu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wanapaswa kuwa mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili katika Parokia wanamoishi na kutekeleza maisha na utume wao wa kitawa. Waamini walei, licha ya ushuhuda wao unaopania kuyatakatifuza malimwengu, wanaweza pia kufundishwa liturujia takatifu na hivyo kushiriki kama: Wasomaji wa Neno la Mungu na Wahudumu Altareni, kwa kuzingatia madhehebu na ibada zake kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katoliki. Wawe wameungana na Kanisa na kwamba, malezi na majiundo yao kama mtu binafsi na katika shughuli za kichungaji, yawasaidie ili waweze kuwa ni watu wa kuigwa kutokana na mifano yao bora ya maisha!

Pamoja na maelekezo haya, baadhi ya waamini walei wanaweza kufundwa na hatimaye, wakateuliwa na Askofu Jimbo, kwa kuzingatia busara ya kichungaji, ili waweze kuadhimisha Ibada ya Neno la Mungu pale ambapo hakuna Mapadre. Wanaweza kuongoza Ibada za mazishi na kutoa Sakramenti ya Ubatizo; wakawa mashuhuda wa ndoa. Ili waweze kuhubiri Kanisani na katika Madhabahu watahitaji kupata kibali kutoka Vatican. Kwa ufupi, waamini walei hawana ruhusa ya kuhubiri wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu! Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapembua pia miundombinu ya Parokia pamoja na watendaji wake wakuu. Kamati ya fedha na uchumi Parokiani, inayoongozwa na Paroko, akisaidiwa na wajumbe wasiopungua watatu. Hawa wana dhamana na wajibu wa kulinda na kuratibu vyema rasilimali fedha na vitu vya Parokia, kama chachu ya uinjilishaji na ushuhuda wa Kanisa linaloinjilisha. Wanapaswa kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na jamii inayowazunguka. Kamati ya fedha na uchumi ijenge na kudumisha utamaduni wa ukweli, uwazi na uwajibikaji katika kutimiza mahitaji msingi ya Kanisa.

Kamati ya Shughuli za Kichungaji Parokiani nayo ni muhimu sana, ili kujenga na kudumisha tasaufi ya maisha ya kiroho inayofumbatwa katika umoja, huku watu wa Mungu wakipewa kipaumbele cha kwanza kama wadau wakuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Hawa wanayo dhamana ya kuibua: sera na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji Parokiani pamoja na kuhakikisha kwamba, Injili ya huruma na upendo wa Mungu inamwilishwa katika maisha na vipaumbele vya waamini, daima wakizingatia sera na miongozo ya Jimbo katika shughuli za kichungaji. Maoni na ushauri wao, ili uweze kuwekwa katika matendo, kwanza kabisa lazima ukubaliwe na Paroko! Sakramenti za Kanisa haziuzwi hata kidogo! Katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa waamini wanahamasishwa kutoa sadaka kwa kusukumwa na dhamiri zao nyofu na wala hakuna kodi kwa maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Na kamwe, Kanisa haliwezi kugeuza maadhimisho ya Ibada na Liturujia mbali mbali kama biashara!

Mapadre wanashauriwa kutumia fedha ya Parokia kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi na kiasi. Ni kwa njia ya mwelekeo huu, waamini walei wanaweza kuhamasishwa kuchangia zaidi katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, kwa kutambua kwamba, Parokia ni mali yao na wala si mtaji wa Paroko! Nyaraka zilizotangulia: Itakumbukwa kwamba,  tarehe 15 Agosti 1997, Mabaraza ya Kipapa kwa pamoja yalichapisha Maagizo Kuhusu Fumbo la Kanisa: Mambo msingi kuhusu ushirikiano wa walei katika utume wa mapadre” “Ecclesia de Mysterio, “On certain questions regarding the collaboration of the non-ordained faithful in the ministry of priests”. Kunako tarehe 4 Agosti 2002, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri lilichapisha Maagizo Kuhusu: Padre, Mchungaji na Kiongozi wa Jumuiya ya Parokia. Nyaraka zote hizi zinapania kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu maisha na utume wa Parokia, ili kuhakikisha kwamba, mifumo mbali mbali ya utume iliyoko Parokiani, kadiri ya malengo yake, inatumika barabara kwa ajili ya utume wa uinjilishaji wa Kanisa.

Waraka wa Parokia
21 July 2020, 14:01