Tafuta

Waraka Kuhusu Maagizo: Wongofu wa kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa. Waraka Kuhusu Maagizo: Wongofu wa kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa. 

Waraka: Wongofu wa Kichungaji Parokiani, Huduma ya Uinjilishaji

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri limechapisha Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa”. Waraka huu unajikita katika tema ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Jumuiya ya Parokia kwa ushiriki wa: wakleri, watawa na waamini walei, kama kielelezo makini cha wajibu wa wabatizwa wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani ntendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Inasikitisha kuona kwamba, kuna waamini wengi ambao hawashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa parokiani. Lakini, ikumbukwe kwamba, kila mwamini anayo nafasi na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Parokiani.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, tarehe 29 Juni 2020 limechapisha Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa”. “Instruction: The pastoral conversion of the Parish community in the service of the evangelising mission of the Church.”. Waraka huu unajikita katika tema ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Jumuiya ya Parokia kwa ushiriki mkamilifu wa: wakleri, watawa na waamini walei, kama kielelezo makini cha wajibu wa wabatizwa wote Mama Kanisa anawakumbusha waamini wote kwamba, ndani ya Kanisa kila mtu anayo nafasi, dhamana na kwamba, wanawajibika kikamilifu kama watu wa familia ya Mungu, kwa kuheshimu wito wa kila mbatizwa. Waraka huu ni matunda ya changamoto iliyotolewa na sehemu kubwa ya Maaskofu mahalia, ili kuliwezesha Kanisa kuwa na chombo cha sheria pamoja na mwongozo wa shughuli za kichungaji, kama chachu ya upyaisho wa Jumuiya ya Kiparokia unaopaswa kufikia kilele chake katika maisha na utume wa Majimbo mahalia ambayo kwa sasa yanaendelea kupyaishwa ili kudumisha umoja na mshikamano katika kanda za kichungaji.

Waraka huu pamoja na mambo mengine, unapania kuwa ni chombo cha huduma kwa wachungaji parokiani na msaada wa majaribio kwa ajili ya watu wa Mungu, ili kuchangia katika mchakato wa upembuzi mintarafu haki za Parokia pamoja na haki za jumla. Katika muktadha huu, Paroko anatambulikana kama “Mchungaji makini” wa Jumuiya ya Kiparokia. Dhamana na mchango wa huduma ya kichungaji inayotolewa na mashemasi, watawa na waamini walei imepewa uzito wa pekee, kwa sababu wanaitwa na kuhimizwa kushiriki kikamilifu katika wito wao kama sehemu ya utume wa uinjilishaji wa Kanisa. Monsinyo Andrea Ripa, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anasema, Waraka kwa Waebraia kuhusu Jumuiya ya kweli unabainisha kwamba, hapa duniani, wanadamu hawana mji udumuo, bali wanautafuta ule ujao na kwamba, Jumuiya hii inaitwa Kanisa la Kristo. Na Mababa wa Kanisa wanakiri kwamba, lakini ilimpendeza Mungu kuwatakatifuza na kuwaokoa watu, sio mmoja mmoja na pasipo muungano kati yao, bali kwa kuwaunda kama taifa moja, lenye kumjua katika ukweli na kumtumikia kitakatifu. Rej. LG.9.

Watu wanaishi katika historia na nyakati na ndani mwake wanashiriki katika kazi ya ukombozi waliyoipokea kutoka kwa Kristo Yesu. Watu wa Mungu, kila mmoja wao kadiri ya wito wake anashiriki kikamilifu katika maisha na wito wa Kanisa. Kumbe, ni watu wa Mungu wanaoinjilisha kila mtu mintarafu wito, hali ya maisha na mazingira anamoishi. Taalimungu ya maana ya Parokia, imefafanuliwa katika Sheria za Kanisa namba 515, Ibara 1 kwa kusema kwamba, Parokia ni Jumuiya ya wafuasi wa Kristo inayoundwa na waamini wenye miito mbalimbali kama vile: wakleri, watawa, waamini walei, vyama na mashirika ya kitume pamoja na familia zinazoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa chini ya uongozi wa Paroko kama mchungaji mkuu wa Parokia. Itakumbukwa kwamba,  tarehe 15 Agosti 1997, Mabaraza ya Kipapa kwa pamoja yalichapisha Maagizo Kuhusu Fumbo la Kanisa: Mambo msingi kuhusu ushirikiano wa walei katika utume wa mapadre” “Ecclesia de Mysterio, “On certain questions regarding the collaboration of the non-ordained faithful in the ministry of priests”. Kunako tarehe 4 Agosti 2002, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri lilichapisha Maagizo Kuhusu: Padre, Mchungaji na Kiongozi wa Jumuiya ya Parokia.

Nyaraka zote hizi zinapania kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu maisha na utume wa Parokia, ili kuhakikisha kwamba, mifumo mbali mbali ya utume iliyoko Parokiani, kadiri ya malengo yake, inatumika barabara kwa ajili ya utume wa uinjilishaji wa Kanisa. Ndani ya Kanisa kila mtu anayo nafasi ya kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa.Waraka huu mpya hauna sheria mpya bali ni kutaka kuwahimiza watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao sheria zilizopo hasa sheria za Kanisa namba 34 Ibara ya 1., kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Parokia husika. Waraka huu ni nyenzo muhimu katika sera, mang’amuzi pamoja na mikakati ya shughuli za kichungaji Parokiani, ili kuweza kuziboresha tena na kuwafanya wabatizwa kuwajibika na kushirikiana zaidi. Ikumbukwe kwamba, huu ni mwono wa Parokia kama unavyofafanuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na “Magisterium” yaani “Mamlaka Fundishi ya Kanisa”, Sheria za Kanisa na kwa namna ya pekee, mkazo unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maisha na utume wa wakleri ndani ya Kanisa.

Ushirikishwaji wa watu wa Mungu ni changamoto inayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko. Parokia iwe ni mahali pa kuonesha umoja na utofauti wa karama kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania pia kuhamasisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa Parokia jirani, ili kujenga: umoja, mshikamano na mafungamano ya Kikanisa kati ya Parokia zilizoko mjini na zile ambazo ziko pembezoni mwa miji. Katika muktadha huu, Askofu Jimbo anaweza kuwateua madekano, watakaoendeleza umoja na Askofu Jimbo. Pale ambapo baadhi ya Parokia zitaunganishwa ili kuboresha ufanisi zaidi, kuna haja ya kujenga na kuimarisha mchakato wa ushirikiano kati ya Askofu Jimbo, Wasaidizi wake wa karibu pamoja na waamini walei na kwamba, Waraka huu utakuwa ni msaada mkubwa kwao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Ili kuweza kuwa na mwingiliano wa Parokia wenye tija kwa wengi, kuna haja ya kuzingatia historia ya watu, maisha na tofauti zao msingi. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watu wote wa Mungu wanahusishwa kikamilifu hatua kwa hatua na katika hali ya unyenyekevu, kabla ya kufikia maamuzi ya mwisho, ili kujenga mwendelezo wa mafungamano ya kijamii na wala si kinyume chake! Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” ni jibu makini kwa wakati huu, ili kusoma alama za nyakati, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, wachungaji wakuu wa Kanisa, wakiwa wameshibana na watu wa Mungu chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Maagizo haya yanabeba ndani mwake, utajiri wa kitaalimungu, shughuli za kichungaji na sheria za Kanisa. Lengo ni kujenga umoja katika tofauti kama kielelezo cha amana na utajiri wa Kanisa.

Waraka: Parokia

 

 

20 July 2020, 13:24