Vatican inaunga mkono jitihada za Shirika la UNCTAD la Kupunguza pamoja na kufuta madeni ya nje kwa Nchi Changa zaidi duniani, ili kuokoa maisha ya watu kutokana na mtikisiko wa uchumi kimataifa. Vatican inaunga mkono jitihada za Shirika la UNCTAD la Kupunguza pamoja na kufuta madeni ya nje kwa Nchi Changa zaidi duniani, ili kuokoa maisha ya watu kutokana na mtikisiko wa uchumi kimataifa. 

Vatican: Deni la Nje ni Mzigo Kwa Mataifa Maskini Duniani

Vatican: Ni wakati wa kusimama kidete kulinda maisha ya watu, kwa kuangalia uwezekano wa kufuta madeni makubwa kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani, madeni ambayo kwa sasa yamekuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka hata kidogo. Hali hii inagumishwa zaidi kutokana na athari za janga kubwa la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, nchini Uswiss, hivi karibuni, ameshiriki katika mkutano wa 67 wa Bodi ya Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNCTAD, kwa kukazia ukweli na uwazi; kanuni maadili na utu wema. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limekuwa na athari kubwa katika ustawi na maendeleo ya wananchi hasa wanaotoka katika Nchi zinazoendelea duniani. Kipindi kirefu cha watu kuwekwa karantini, kuporomoka kwa vitega uchumi na uzalishaji; ukosefu wa fursa za ajira na mambo mengine kama haya yanaendelea kuchangia kuporomoka kwa soko la fedha kimataifa. Ni hakika kwamba, watu wengi kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani, wataathirika sana. Ni wakati wa kusimama kidete kulinda maisha ya watu, kwa kuangalia uwezekano wa kufuta madeni makubwa kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani, madeni ambayo kwa sasa yamekuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka hata kidogo. Hali hii inagumishwa zaidi kutokana na athari za janga kubwa la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Nchi changa zenye madeni makubwa, HIPC, pamoja na Mpango Mkakati wa Nafuu ya Deni la Nje, MDRI, ni ushuhuda kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kutenda kwa dhati pale inapotakiwa.

Huu ni wakati wa kuongeza juhudi kama hizi, kwa kuhakikisha kwamba, madeni ya nje ambayo yamekuwa ni mzigo mzito, yanapunguzwa na kama si kufutwa kabisa, ili kutoa nafuu katika sera na mipango ya Nchi Zinazoendelea duniani. Ujumbe wa Vatican unaunga mkono jitihada za Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNCTAD, la kupunguza pamoja na kufuta madeni kama ilivyooneshwa kwenye taarifa yake kwa Mwezi Juni 2020. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi katika ujenzi wa jamii fungamani na endelevu ya binadamu. Jambo hili halina budi kwenda sanjari na uboreshaji wa masoko, uwekezaji wa rasilimali watu pamoja na kuendelea kuwamotisha wafanyakazi. Juhudi hizi zilenge pia kuwajengea uwezo maskini pamoja na kuwalinda walaji. Mchakato wa huduma na uzalishaji vijijini hauna budi kuboreshwa maradufu kwa kukazia utawala bora katika masuala ya kiuchumi, ili kuibua sera na mikakati itakayowasaidia wananchi kupambana na changamoto za utandawazi kitaifa na kimataifa. Katika muktadha huu, kanuni maadili, utu wema na utamaduni wa watu mahalia ni mambo ambayo hayawezi  hata kidogo kuangaliwa “kwa jicho la kengeza”.

Matatizo na changamoto mbali mbali anazokabiliana nazo mwanadamu katika ulimwengu mamboleo kwenye masuala ya fedha na uchumi ni matokeo ya kutozingatia kanuni maadili na utu wema. Maadili yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya uchumi, ili hatimaye, kujenga mshikamano wa kimaadili utakaosaidia kumwilisha kwa vitendo vipaumbele hivi. Katika miaka ya hivi karibuni, soko huria limepewa kipaumbele cha pekee na matokeo yao ni kuporomoka kwa sera na mikakati mbali mbali ya kiuchumi, kuanguka kwa miundo mbinu ya huduma ya afya, uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote; mambo ambayo kimsingi yanaleta athari kubwa katika maisha ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuketi kitako na kuanza kupanga mambo ya mbeleni, kwa kuzingatia kanuni maadili na uwajibikaji, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watunga sera wawe na rasilimali fedha itakaowawezesha kurekebisha athari za uchumi na huduma ya afya.

Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu, umehimiza kwa namna ya pekee, utekelezaji wa misingi ya ukweli na uwazi; uwajibikaji na ujasiri, kwa ajili ya kuhudumia maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kuwasaidia watu kudumisha utu na heshima yao, kwa kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, ili kweli sera na mikakati mbali mbali ya uchumi iwe ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, ujenzi wa amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Janga la Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Kumbe, mfumo wa fedha kimataifa hauwezi kuendelea kuwa ni chanzo cha kuyumba kwa uchumi kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujipanga ili kuhakikisha kwamba, hakutakuwepo tena na mtikisiko katika sekta ya fedha kwa siku za usoni!

UNCTAD 2020
06 July 2020, 13:59