Tafuta

Jumapili ya Utume wa Bahari inaadhimishwa tarehe 12 Julai 2020 ili kutafakari na kuangalia matatizo,. changamoto na fursa wanazokabiliana nazo mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Jumapili ya Utume wa Bahari inaadhimishwa tarehe 12 Julai 2020 ili kutafakari na kuangalia matatizo,. changamoto na fursa wanazokabiliana nazo mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. 

Ujumbe wa Jumapili ya Utume wa Bahari 12 Julai 2020

Maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari, yalianzishwa kunako mwaka 1975, ili kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi pamoja na familia zao. Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwa kuwashirikisha Wakristo wa Makanisa na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano wa kidugu na wadau hawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2020 anaadhimisha Jumapili ya Utume wa Bahari, fursa makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kumtukuza na kumshukuru Mungu, kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini: mchango na sadaka ya watu hawa, ambao wakati mwingine, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari, yalianzishwa kunako mwaka 1975, ili kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi pamoja na familia zao. Hii ni siku maalum ambayo Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mabaharia katika ustawi na maendeleo ya binadamu katika nyanja mbali mbali za maisha. Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani yanawashirikisha Wakristo kutoka katika Makanisa na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano wa kidugu na mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.

Kuanzia tarehe 4 Oktoba 2019 hadi tarehe 4 Oktoba 2020 yalikuwa ni maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris”. Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika Utume wa Bahari, kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati na kuendelea kujibu kilio cha mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na utume wao baharini! Pamoja na mambo mengine, Utume wa Bahari umeendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, mabaharia na wavuvi ambao wanajisadaka usiku na mchana ili kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, wanapata pia fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Takwimu zinaonesha kwamba, Utume wa Bahari unatekeleza dhamana na wajibu wake katika bandari 261 zilizoko katika nchi 55 na wanahudumiwa na Mapadre zaidi ya 200 bila kuwasahau watu wa kujitolea.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia zaidi kwa kusema, Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbali mbali za dunia. Roho Mtakatifu, kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya ulimwengu mamboleo! Kuna mabaharia ambao dhamiri zao zinahangaika sana na mara nyingi Mapadre wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi wamekuwa ni msaada mkubwa. Mabaharia ni watu wanaofanya kazi zao mara nyingi nje ya nchi, makazi na familia zao! Mapadre washauri wa kiroho katika muktadha kama huu, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini kwa mabaharia na wavuvi waliopondeka na kuvunjika moyo! Mapadre wanapaswa kuwa ni watu wenye huruma, wapole na wanyenyekevu!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika ujumbe wake kwa Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2020 anasema, kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, maadhimisho haya yamesogezwa mbele zaidi, hadi hapo mwaka 2021 huko Glasgow, nchini Scotland. Maadhimisho ya Mwaka 2020 yameingiwa na hofu na mashaka makubwa kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni wakati wa kufarijiana na kutiana hamasa. Watu wa Mungu sehemu mbali mbali wamejikuta wakiwa wamewekwa chini karantini kwa muda mrefu. Lakini mabaharia na wavuvi waliendelea kuchakarika usiku na mchana, huku wakikabiliana na matatizo na changamoto mbali mbali za maisha.

Ni katika muktadha huu, mabaharia na wavuvi, wakawa nao mstari wa mbele kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19. Meli zikabeba shehena za dawa na vifaa tiba. Wakati mwingine, ikawawia vigumu mabaharia na wavuvi kutua nanga kwenye bandari kwa kuhofiwa kwamba, wangeweza kusababisha maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Licha ya changamoto zote hizi, bado mabaharia na wavuvi wameendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa kitaifa na kimataifa. Ndiyo maana Jumapili ya Utume wa Bahari ni fursa makini ya kupembua mchango wa mabaharia na wavuvi, kwa kupitia pia mambo ambayo yanahatarisha maisha ya mabaharia na wavuvi kwa hofu ya kuweza kuambukizwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Katika miezi ya hivi karibuni, maisha na kazi za mabaharia pamoja na wavuvi zimebadilika sana, kwa sababu wanapaswa kuendelea kujisadaka zaidi bila ya kujibakiza. Kutokana na hofu ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, mabaharia wengi walizuiliwa kwenye meli zao, hali ambayo imepelekea mabaharia wengi kuanza kusumbuliwa na afya ya akili, uchovu pamoja na kupunguza uwezo wao wa kufanya kazi.

Hali ya mabaharia kuendelea kufanya kazi katika mazingira haya magumu na hatarishi ni hatari sana kwa mabaharia weyewe, hali ambayo pia inahatarisha usalama wa vyombo vyao baharini. Baadhi yao wamediriki hata kujinyonga kwa kutoona tena maana ya maisha. Wengi wao bado wanaendelea na matibabu ya muda mrefu, kwa sababu walicheleweshwa kupata huduma ya afya. Kuna baadhi ya makampuni na wamiliki wa meli hizi wametumia mwanya wa janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kukwepa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kushindwa kuwalipa mshahara, kuwahakikishia ulinzi na usalama wa maisha yao pamoja na mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka 2020 kumekuwepo na ongezeko la asilimia 24% ya matukio ya mashambulizi ya kiharamia, ikilinganishwa na mwaka 2019. Maharamia wameendelea kuwa ni tishio kwa usalama na maisha ya mabaharia na wavuvi. Ni katika muktadha huu,  kazi ya mabaharia na wavuvi inahesababika kuwa ni kati ya kazi za hatari sana duniani. Hii inatokana na ukweli kwamba, hawa ni watu ambao maisha yao daima yako hatarini kutokana na kupata kipato “kiduchu” kiasi hata cha kushindwa kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wa kuzitegemeza familia zao kwa hali na mali.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari, kwa mwaka 2020 iwe ni fursa ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, mabaharia na wavuvi, kwa kuonesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mshikamano ni fadhila inayomwezesha mwamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ndio mwelekeo sahihi unaopaswa kutekelezwa kwa kuwaona mabaharia na wavuvi kuwa watu maskini, kwa sababu ya kuhatarisha maisha yao, lakini pia ni wasafirishaji wakuu wa dawa na vifaa tiba sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, wanapaswa kuoneshwa moyo wa shukrani kwa kutambua kwamba, wanathaminiwa na jamii. Mabaharia na wavuvi watambue kwamba, hawako peke yao na wala hawajasahaulika hata kidogo! Kama anavyosema Bwana Kitack Lim, Katibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Bahari ‘International Maritime Organization" (IMO).

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anapenda kutumia fursa hii, kuwapatia ujumbe wa sala ya matumaini na faraja mintarafu matatizo na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao. Anapenda pia kuwatia shime, wahudumu wa maisha ya kiroho na watu wa kujitolea, wanaoshirikiana nao bega kwa bega katika utume wa bahari kwa ajili ya mabaharia na wavuvi. Kamwe bado hawajasahauliwa, Mama Kanisa ataendelea kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao ya kiroho na kimwili. Ataendelea kuthamini mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; haki zao msingi na kupinga mifumo yote ya ubaguzi dhidi yao. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na matatizo na changamoto za maisha yao, anapenda kuelekeza Nia zake kwa Mwezi Agosti kwa Ajili ya Wafanyakazi Baharini. Watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia wanahimizwa na Mama Kanisa kusali na kuwaombea mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao bila kuwasahau watu wa kujitolea. Mwishoni mwa ujumbe wake, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anapenda kuwaombea wote hawa pamoja na familia zao, heri na baraka sanjari na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari aweze kuwakinga na hatari zote, lakini zaidi hatari ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Utume wa Bahari 2020
10 July 2020, 14:25