Tafuta

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linasema, litaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge duniani hata baada ya janga la virusi vya Corona, COVID-19. Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linasema, litaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge duniani hata baada ya janga la virusi vya Corona, COVID-19. 

Caritas Internationalis Itaendelea Kuwa ni Sauti ya Wanyonge!

Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, ni tukio ambalo limetikisa mifumo ya sekta ya afya duniani, kiasi kwamba, kwa sasa kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya. Maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni kati ya vipaumbele vya Caritas Internationalis kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, katika mkutano mkuu wa Shirikisho hili hivi karibuni kwa njia ya video, amekazia mambo makuu matatu ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga, ili kuwajengea watu wa Mungu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, ni tukio ambalo limetikisa mifumo ya sekta ya afya duniani, kiasi kwamba, kwa sasa kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya. Maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni kati ya vipaumbele vya Caritas Internationalis kwa siku za usoni.

Caritas Internationalis itaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge duniani, kwa kuiangalia dunia baada ya janga la COVID-19. Kwa upande wake, Aloysius John, Katibu mkuu wa Caritas Internationalis amesema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuingilia kati kuhusu: suala la deni la nje kimataifa pamoja na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa huko Mashariki ya Kati. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle amesema, janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limeipekenya na “kuipapasa” Caritas Internaionalis, kiasi cha kuifanya kusitisha miradi, sera na mikakati ya shughuli zake: kiroho na kimwili. Lakini, jambo la kumshukuru Mungu ni kuona kwamba, Mashirika 162 ya Misaada ya Kanisa Katoliki katika mataifa mbali mbali yameendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ufanisi mkubwa, huku yakijitahidi kujibu changamoto, matatizo na dharura iliyojitokeza kutokana na kuibuka kwa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Mashirika haya yameendesha kampeni ya huduma kwa waathirika wa Virusi vya Corona, wakawapatia taarifa muhimu pamoja na kuwatunza katika kipindi hiki, ambacho wagonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 walikuwa wanaogopwa hata na ndugu zao wenyewe! Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle amewataka viongozi wa Caritas Internationalis kujifunga kibwebwe na kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna mamilioni ya watu ambao kwa sasa wanaanza kuteseka kutokana na baa la njaa. Hali ya watu wa Mungu nchini Lebanon, Siria na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake, inaendelea kudhohofu sana. Hii inatokana na vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimewekwa na Jumuiya ya Kimataifa katika baadhi ya nchi zilizoko huko Mashariki ya Kati, lakini waathirika wakubwa ni maskini, “akina yakhe, pangu pakavu, tia mchuzi”.

Gharama ya maisha imepanda sana kutokana na ongezeko la bei ya mahitaji msingi ya binadamu, wakati ambapo hali ya maisha imeendelea kudidimia kila kukicha! Baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni tishio kwa mamilioni ya watu duniani. Hali hii inagumishwa pia na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Lebanon, ambayo kwa miaka mingi imejipambanua kuwa ni kielelezo makini cha demokrasia na uchumi thabiti, leo hii, asilimia 75% ya wananchi wake wanahitaji msaada wa dharura, kwa sababu wametumbukizwa chini ya kiwango cha umaskini duniani. Lebanon imekuwa ikitoa hifadhi kwa wakimbizi, wahamiaji na watu waliokuwa wakitafuta hifadhi ya kisiasa, kwa sasa inakabiliwa na mzigo mzito wa kuwahudumia watu hawa wanaohitaji: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Janga la Virusi vya Corona, COVID 19, limetikisa na kuvuruga uchumi kwa mataifa mengi duniani, kiasi kwamba, kwa sasa kuna wimbi kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira; watu wanaoendelea kutumbukizwa katika baa la umaskini wa hali na kipato! Ni wakati wa kusimama kidete kulinda maisha ya watu, kwa kuangalia uwezekano wa kufuta madeni makubwa kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani, madeni ambayo kwa sasa yamegeuka na kuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka hata kidogo. Hali hii inagumishwa zaidi kutokana na athari za janga kubwa la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Waathirika wakuu ni watu wa Mungu kutoka Barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Deni la nje lisilolipika kwa wakati lina madhara makubwa katika mchakato wa ukuaji wa uchumi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Caritas Internationalis

 

21 July 2020, 13:37