Vatican News
Kardinali Luis Francisko Ladaria Ferrer, SJ., amewasilisha Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasi wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa: Kuboreshwa zaidi kwa kusoma alama za nyakati! Kardinali Luis Francisko Ladaria Ferrer, SJ., amewasilisha Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasi wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa: Kuboreshwa zaidi kwa kusoma alama za nyakati! 

Kardinali Ladaria: Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Nyanyaso

Mwongozo huu unapania kuwasaidia Maaskofu mahalia na wakuu wa mashirika kufikia ukweli, ili hatimaye, haki iweze kutendeka. Mwongozo ni msaada kwa watu wanaoshughulikia sheria na haki ndani ya jamii, kumbe, huu ni mwongozo na wala si sheria ili kushughulikia mchakato wa kesi za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa, tangu mwanzo hadi hatima yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, tarehe 16 Julai 2020 amewasilisha Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa, “Vademecum” ili kusaidia ukweli uweze kufahamika na haki kutendeka. Mwongozo huu ni hitaji lililooneshwa na Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume sehemu mbali mbali za dunia. Hili ni tatizo na changamoto pevu, iliyogeuka na kuwa ni kashfa katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Katika mchakato huu wa kuganga na kuponya kashfa hii, Mama Kanisa anataka kujielekeza zaidi katika kutafuta ukweli, ili haki iweze kutendeka, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazobainishwa na Mama Kanisa. Mwongozo huu unapania pamoja na mambo mengine, kuwasaidia Maaskofu mahalia na wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume kufikia ukweli, ili hatimaye, haki iweze kutendeka.

Ni Mwongozo unaoweza kuwa ni msaada mkubwa kwa watu wanaoshughulikia sheria na haki ndani ya jamii, kumbe, huu ni mwongozo na wala si sheria mpya iliyotungwa, ili kushughulikia mchakato wa kesi za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa, tangu mwanzo hadi hatima yake! Kisheria ni tangu pale habari ya kesi ya uhalifu wa nyanyaso za kijinsia inapotolewa “notitia de delicto” hadi huku yake inapotolewa yaani “res iudicata”. Hiki ni kipindi ambacho kuna hatua muhimu sana zinapaswa kufuatwa na kutekelezwa, taarifa muhimu zinazopaswa kutolewa pamoja na maamuzi yanayopaswa kufanywa kwa kuzingatia ukweli na haki! Mkutano wa Viongozi wa Kanisa uliofanyika kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019, wajumbe walipendekeza mambo makuu 21 yaliyopaswa kufanyiwa kazi kama sehemu ya mchakato wa kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu Francisko alikazia kuhusu umuhimu wa kuwalinda watoto wadogo, adhabu kali kutolewa; toba na wongofu wa ndani; malezi makini; uimarishaji na mapitio ya miongozo ya Mabaraza ya Maaskofu.

Mwongozo unatoa Nyaraka za Rejea zilizotolewa na Viongozi wa Kanisa: Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo mwaka 2001 kwa Barua binafsi “Motu proprio”, “Sacramentorum sanctitatis tutela”, yaani “Ulindaji wa Utakatifu wa Sakramenti”, alitoa taratibu za mchakato wa kuendesha kesi hizo katika Mahakama za Kanisa. Mnamo mwaka 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa Tamko, “Reformatio Normae gravioribus delictis”, yaani “Juu ya Marekebisho ya Kanuni za Makosa Makubwa ya Uhalifu”, aliziboresha taratibu hizo kwa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa havikueleweka barabara! Akatambua na kukiri kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kosa kubwa la kimaadili na linapaswa kushughulikiwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer anasema, Mwongozo huu ni toleo la kwanza na unatarajiwa kufanyiwa maboresho zaidi mintarafu Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa, ili kutoa majibu muafaka kwa changamoto mamboleo, ili kushughulikia kesi zinazobainishwa katika Mwongozo huu. Mwongozo unategemea kuboreshwa zaidi kwa mchango kutoka kwenye Makanisa mahalia, Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa. Ni mwongozo unaotoa changamoto ya kuanzisha mchakato wa kujadiliana na kusikilizana, ili kurekebisha mapungufu yanayoweza kujitokeza, kuongeza pale palipotindikiwa, kuonesha msisitizo na kutolea ufafanuzi mambo ambayo bado hayajafahamika vyema. Kwa hakika kuna umuhimu wa kufanya tafakari na upembuzi yakinifu!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alisisitizia umuhimu wa kuwasindikiza waathirika wa nyanyaso za kijinsia pamoja na kuangalia ulimwengu wa kidigitali na madhara yake pamoja na kupambana na Utalii wa ngono duniani unaodhalilisha utu na heshima ya watu! Baba Mtakatifu alisikitika kusema kwamba, nyanyaso za kijinsia ni janga ambalo limenea sehemu mbali mbali za dunia na wakati mwingine, linajikita katika imani za kishirikina zinazopelekea watoto wadogo kutolewa kafara. Mbinu mkakati utakaosaidia kufutilia mbali nyanyaso dhidi ya watoto wadogo. Hapa Baba Mtakatifu aliorodhesha mambo makuu nane yanayopaswa kuvaliwa njuga ili kukomesha ukatili dhidi ya watoto wadogo. Mosi, ulinzi kwa watoto wadogo unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili kuwalinda dhidi ya nyanyaso za kisaikolojia na kimwili. Watu wanapaswa kutubu na kuongoka; kwa kujikita katika ukweli na uwazi, ili kamwe wasiwe ni sababu ya kashfa kwa watoto wadogo, kwani watakiona cha mtema kuni! Pili, nyanyaso za kijinsia ni uhalifu mkubwa unaonesha jinsi ambavyo watu wamekengeuka kwa kukosa uaminifu kiasi cha kuandamwa na aibu. Hawa ni watu wanaochafua maisha na utume wa Kanisa.

Tatu, kuna haja ya kufanya utakaso wa kweli, kwa kujikita katika sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo; kwa viongozi wa Kanisa kuendelea kupyaisha maisha yao kwa kuambata utakatifu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanalinda na kutunza haki msingi za watu wa Mungu. Kanisa linataka kujitakasa na kusimama kidete kuwalinda watoto wadogo; kuendelea kujifunza makosa yaliyopita, ili kuondoa kashfa hii ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake! Nne, Kanisa litaendelea kukazia malezi, kwa kuwateua vijana wanaostahili kushiriki maisha na wito wa Kipadre; Kanisa linataka kujikita katika malezi na makuzi yenye uwiano bora sanjari na kukazia useja kama sadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!

Tano, Kanisa litaendelea kuimarisha pamoja na kupitia miongozo mbali mbali ambayo imetolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, ili kuhakikisha kwamba, inatekelezwa vyema na Maaskofu mahalia. Ukweli, uwazi na ulinzi wa watoto wadogo ni mambo yanayopaswa kupewa uzito unaostahili. Lengo ni kuzuia nyanyaso za kijinsia katika maeneo yote ya Kanisa, ili watoto waweze kupata mali pazuri zaidi pa malezi na makuzi yao. Sita, Kanisa liwasindikize waathirika wa nyanyaso za kijinsia, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali wanaouhitaji! Kanisa lijenge na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuganga na kuponya madonda ya watu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema.

Saba, Ulimwengu wa kidigitali kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii unapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Viongozi na wafanyakazi wa Kanisa watambue madhara yanayoweza kuwakumba watumiaji wa mitandao hii. Serikali mbali mbali duniani hazina budi kudhibiti mitandao ambayo inahatarisha utu na uhuru wa kweli wa binadamu. Picha za utupu zitendelee kudhibitiwa ili kuhakikisha kwamba, majandokasisi na wakleri hawageuzwi na kuwa ni watumwa wa picha za ngono na utupu! Makosa makubwa ya uhalifu, Delicta graviora, kama yalivyofafanuliwa na kupitishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI yapitiwe tena na kuongezewa vipengele kuhusu ununuzi, umiliki na usambazaji wa picha za ngono za watoto wadogo unaoweza kufanywa na wakleri kwa kutimia aina yoyote ile ya teknolojia. Na kwamba, umri wa watoto wadogo unapaswa kuongezwa na kufikia miaka kumi na sita

Nane ni kuhusu Utalii wa Ngono! Watu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Wanapaswa kupewa nafasi ya kukua na kukomaa: kiroho na kimwili pamoja na kuendeleza mahusiano na mafungamano yao na jirani. Kumbe, utu, heshima na utakatifu wao vinapaswa kulindwa dhidi ya nyanyaso, unyonyaji pamoja na rushwa. Mapambano dhidi ya utalii wa ngono yaende sanjari na kuwajengea uwezo waathirika kurejea tena katika jamii na hivyo kuendelea na maisha. Taasisi za Kanisa ziwasaidie waathirika wa utalii wa ngono. Serikali mbali mbali zisimame kidete kupambana na biashara ya binadamu na unyonyaji wa watoto wadogo kingono kwa kuhakikisha kwamba, sheria zilizopo zinatekelezwa kikamilifu. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wakleri na watawa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwalinda na kuwatetea waathirika wa utalii wa ngono.

Baba Mtakatifu anahitimisha kwa kusema, katika usiku na giza nene, huu ndio wakati wa kuibuka kwa Manabii na Watakatifu! Unabii wa Kanisa unatekelezwa kikamilifu kati pamoja na watu wa Mungu! Zawadi kubwa inayoweza kutolewa kwa watu wa Mungu ni toba na wongofu wa ndani; unyenyekevu katika kujifunza; kusikiliza na kuhudumia sanjari na kuwalinda watoto wadogo! Baba Mtakatifu anawataka watu kusimama kidete kupambana na nyanyaso na dhuluma dhidi ya watoto wadogo! Serikali ziunge mkono juhudi hizi, ili mafanikio yaweze kupatikana.

Kardinali Ladaria
16 July 2020, 14:49