Tafuta

Vatican News
Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, FAS: Kipaumbele cha kwanza: Utu, heshima na haki msingi za binadamu! Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, FAS: Kipaumbele cha kwanza: Utu, heshima na haki msingi za binadamu!  (ANSA)

Mfuko wa Bima ya Afya Vatican: Utu na Haki Msingi za Binadamu

Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, FAS., unawahudumia wafanyakazi wa Vatican na taasisi zinazosimamiwa na kuendeshwa na Vatican kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mfuko unagharimia huduma za matibabu kwa wanachama wake wagonjwa kwa kutambua kwamba, ugonjwa ni kati ya mambo yanamsukumizia mtu pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Prof. Dr. Giovanni Battista Doglietto kuwa Mkurugenzi mpya wa Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, “Fondo Assistenza Sanitaria, FAS”. Prof. Dr. Giovanni Battista Doglietto alizaliwa tarehe 17 Aprili 1948 huko mjini Torino, Kaskazini mwa Italia. Tangu mwaka 1974 amekuwa katika sekta ya huduma ya afya na kunako mwaka 1996 aliteuliwa kuwa mkuu wa kitengo cha upasuaji wa magonjwa ya mfumo wa chakula, Hospitali ya Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Katika taaluma yake, amefanikiwa kufanya upasuasi wa kati na wa hali ya juu kabisa kwa wagonjwa zaidi ya 5, 000. Kwa hakika ni mtaalam, aliyetaalaumiwa, ili kuwataalam watalaumiwa wa siku za usoni katika huduma ya upasuaji wa magonjwa ya mfumo wa chakula. Licha ya shughuli zote hizi katika huduma ya afya, bado Prof. Dr. Giovanni Battista Doglietto anatambulikana na Jumuiya ya Kimataifa kwa machapisho yake ya kisayansi na kitaaluma. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi mwaka 2020 amekwisha kuchapisha makala 500.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Monsinyo Luigi Misto’, Rais wa Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, FAS., anasema, Mfuko huu unawahudumia wafanyakazi wa Vatican, pamoja na taasisi zinazosimamiwa na kuendeshwa na Vatican kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mfuko huu unagharimia huduma za matibabu kwa wanachama wake wagonjwa kwa kutambua kwamba, ugonjwa ni kati ya mambo yanayomsukumizia mwanadamu pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mfuko huu unachota utajiri wa huduma zake kutoka katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kuzingatia Injili ya upendo na huduma kwa wagonjwa, ushuhuda unaopaswa kutolewa na Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, FAS. Kumbe, hapa kila mfanyakazi anachangia katika Mfuko huu kadiri ya uwezo na nafasi yake, ili kuweza kutoa huduma makini kwa wafanyakazi wagonjwa pamoja na familia zao. Hii ina maana kwamba, hata wale ambao wamebahatika kuwa na afya njema, wanachangia kwenye Mfuko wa Bima ya Afya, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo.

Ili kuhudumiwa vyema na Mfuko huu, kuna wakati ambapo wanachama wanatakiwa kuchangia sehemu ya gharama ya matibabu kadiri ya mkataba uliopo, ili kuboresha huduma hii makini. Ni katika msingi wa kuzingatia Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu, tarehe 16 Juni 2000, Vatican na Serikali ya Italia, vilitiliana sahihi Mkataba wa Usalama wa Jamii, kwa ajili ya wafanyakazi wa Vatican ili kuweza kuwahakikishia usalama wa maisha yao wanapokuwa kazini. Ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa za huduma ya afya, Monsinyo Luigi Misto’, Rais wa Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, FAS., anasema, “Tume ya Kipapa ya Huduma za Afya” inakazia misingi ya ukweli na uwazi ya matumizi ya rasilimali ya Kanisa, ili kuendelea kutoa huduma bora zaidi, bila ya kuingia kwenye myumbo wa rasilimali fedha. Katika kipindi cha Mwaka 2017, Mfuko wa Bima ya Afya Vatican, FAS ulikuwa na akiba ya kiasi cha Euro milioni 3.6. Fedha ya FAS haiwezi kutumika kama kitega uchumi.

Bima ya Afya Vatican
20 July 2020, 10:40