Tafuta

Vatican News
Mamlaka ya Habari za Kifedha Mjini Vatican, AIF, imetoa taarifa ya utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kwa mwaka 2019. Mamlaka ya Habari za Kifedha Mjini Vatican, AIF, imetoa taarifa ya utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kwa mwaka 2019. 

Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican: Taarifa ya Mwaka 2019

Katika kipindi cha Mwaka 2019, kumekuwepo na matukio 64 yaliyotiliwa shaka kuhusu uhalali wake. Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF imeshirikiana kwa karibu sana na nchi mbali mbali na matokeo yake yameanza kuonekana. Akaunti iliyokuwa na Euro 240, 000 pamoja na Euro 178, 970, 65 ilizuiliwa. Kumekuwepo na matukio ya utapeli wa kimataifa na ukwepaji wa kodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, “Financial Information Authority” imechapisha taarifa yake kwa Mwaka 2019. Hii ni taarifa inayoonesha shughuli mbali mbali zilizotekelezwa na Taasisi hii katika kipindi cha Mwaka 2019 mintarafu udhibiti wa mchakato wa kutakatisha fedha haramu pamoja na kudhibiti ufadhili wa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Usimamizi wa mali na fedha za Kanisa unapaswa kuzingatia misingi ya: ukweli, uwazi, uadilifu na weledi, mambo yanayoendelea kupewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko ili kweli rasilimali fedha iweze kutumika kiaminifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Katika kipindi cha Mwaka 2019, kumekuwepo na matukio 64 yaliyotiliwa shaka kuhusu uhalali wake. Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF imeshirikiana kwa karibu sana na nchi mbali mbali na matokeo yake yameanza kuonekana. Akaunti iliyokuwa na kiasi cha Euro 240, 000 pamoja na Euro 178, 970, 65 ilizuiliwa.

Kumekuwepo na matukio ya utapeli wa kimataifa, ukwepaji wa kodi halali pamoja na baadhi ya watu kuingia madeni makubwa ambayo yangehatarisha usalama wa fedha. Watu 370 wamehusishwa katika mchakato wa ubadilishanaji wa habari za kifedha kimataifa na hatimaye, kubainisha uhalali wa fedha hizi. Hivi karibuni, Bodi ya Baraza la Malipo Ulaya, EPC, imeidhinisha upanuzi wa mtandao wa huduma yake kijiografia kwa nchi zinazolipia gharama kwa kutumia fedha moja ya Euro kwa Vatican, kuanzia tarehe 1 Machi 2019 ilipojiunga rasmi. SEPA inaratibu malipo yote yanayofanyika Barani Ulaya kwa njia ya Euro. Mpango huu unawawezesha walaji, wafanyabiashara na viongozi wa Serikali mbali mbali kutuma, kupokea au hata kukopa fedha kwa kuzingatia masharti na vigezo vilivyowekwa kiasi cha kulahihisha malipo ya ndani yanayofanyika kwa njia ya fedha ya Euro! Mpango huu wa SEPA unazijumuisha nchi 36 kati yake kuna Nchi 28 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya, EU. Na nyingine ni Iceland, Norway, Liechteinstein, Uswiss, Monaco, San Marino, Andorra na Vatican.

Kwa upande wake, Dr. Carmelo Barbagallo Rais wa Baraza la Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF anasema, katika kipindi cha mwaka 2019 hadi mwanzoni mwa mwaka 2020 kuna mabadiliko makubwa ambayo yamefanyika, hususan kwa kuimarisha udhibiti wa mali na fedha ya Kanisa, kielelezo makini kuwa, Vatican inaendelea kuimarisha misingi ya ukweli na uwazi katika masuala ya rasilimali fedha! Moneyval ni Kamati ya Wataalam wanaotathmini mikakati ya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ufadhili wa vitendo vya kigaidi, sehemu mbali mbali za dunia. Mwezi Septemba 2020, Kamati hii inaweza kujionea maendeleo makubwa ambayo yametekelezwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF. Dr. Carmelo Barbagallo anaendelea kufafanua kwamba, kumekuwepo na mabadilishano ya habari za kifedha katika ngazi za Kimataifa. Kwa kiasi kikubwa wafanyakazi wamenolewa ili kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ufadhili wa vitendo vya kigaidi pamoja na kuhakikisha kwamba, Benki Kuu ya Vatican, IOR inatekeleza dhamana yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Kimataifa sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF, inaendelea kupata ushirikiano kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na utekelezaji wa dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia ukweli, uwazi na weledi. Mamlaka hii inataka kuendelea kuratibu habari za kifedha kwa kutumia intelijensia, ili kuimarisha utawala bora unaozingatia sheria, kanuni na taratibu. Utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi ni kati ya vipaumbele vinavyovaliwa njuga na Mamlaka hii. Lakini katika taarifa yake kwa Mwaka 2019, hakukuwepo na dalili zinazohusisha vitendo hivi. Bado kuna haja kwa Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF kujizatiti zaidi katika kuratibu mahusiano ya fedha inayotolewa kama “sadaka” au mchango kwa Taasisi Zisizo za Kiserikali; uratibu zaidi wa matumizi ya fedha ya Kanisa pamoja na mikataba ya kitaifa na kimataifa, mianya ambayo inaweza kutumiwa kwa ajili ya kulihujumu Kanisa. Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa na mabadilishano ya habari za kifedha kutoka mjini Vatican kama sehemu ya mchakato wa Kanisa kupambana na utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi ambavyo vinakwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, hakuna wakwepa kodi wa kitaifa na kimataifa wanaotumia mfumo wa fedha wa Vatican kujinufaisha binafsi.

Habari za Kifedha
04 July 2020, 13:44