Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema, kifolaini au Eutanasia ni kinyume cha Sheria ya Mungu. Maandiko Matakatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema, kifolaini au Eutanasia ni kinyume cha Sheria ya Mungu. Maandiko Matakatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa.  (REUTERS)

Kifolaini; Eutanasia ni Kinyume cha Sheria ya Mungu na Kanisa!

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limemwandikia barua Bruda Renè Stockman, Mkuu wa Shirika la Mabruda wa Upendo “Frères de la Charitè” kuhusiana na matukio ya kifolaini yaliyofanywa kwenye hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Shirika hili huko nchini Ubelgiji. Hizi ni hospitali za wagonjwa wa afya ya akili ambazo zimekiuka Sheria ya Mungu na Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayotishiwa na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za kifolaini na utoaji mimba. Hakuna uhuru wa kuchagua kifolaini, bali huu ni utamaduni wa kifo. Ni maneno mazito yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Septemba 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Chama cha Madaktari wa Saratani nchini Italia, “AIOM, yaani “Associazione Italiana di Oncologia Medica” kilichoanzishwa kunako mwaka 1973. Mgonjwa anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa hasa kutokana na ukali wa mateso anayokabiliana nayo. Kila huduma ya matibabu inayotolewa kwa mgonjwa iwe ni chemchemi ya huruma na upendo kwa wagonjwa wanaoteseka. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya mwanadamu yanapaswa kuwa kweli ni chombo cha huduma kwa wagonjwa na wala si vinginevyo. Kamwe mgonjwa asionekane kuwa ni mgizo mzito, kiasi cha kuanza kuhalalisha kisheria mchakato wa kifolaini.

Kwa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu Francisko jambo hili linaweza kuonekana kuwa kama sehemu ya uhuru wa mtu binafsi; lakini ndani mwake, uhuru huu unafumbata ubinafsi unao thubutu kupima utu wa mtu kutokana na umuhimu wake. Kifolaini hakimsaidii mtu kupungumza maumivu. Kumbe, ni dhamana na wajibu wa madaktari kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wagonjwa kupata nafuu katika mahangaiko yao; kwa kujenga na kudumisha utamaduni unaothamini utu, heshima na haki msingi za binadamu; chemchemi ya matumaini katika maisha ya mwanadamu! Madaktari wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa wagonjwa waliokata tamaa; kwa kusaidia kuzuia magonjwa; kwa kufanya uchunguzi wa kina pamoja na kuwaheshimu wagonjwa wenyewe kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Changamoto za maisha kwenye miji mikuu imepelekea watu wengi kutumbukia katika msongo wa mawazo pamoja uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Saratani sehemu mbali mbali za dunia hayana budi kujielekeza zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; hii ni sehemu ya utu wa mwanadamu na maendeleo yake kijamii.

Ni katika muktadha huu, Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa pamoja na Askofu mkuu Giacomo Morandi, Katibu mkuu wa Baraza, wamemwandikia barua Bruda Renè Stockman, Mkuu wa Shirika la Mabruda wa Upendo “Frères de la Charitè” kuhusiana na matukio ya kifolaini yaliyofanywa kwenye hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Shirika hili huko nchini Ubelgiji. Hizi ni hospitali za wagonjwa wa afya ya akili. Hospitali hizi zimekuwa zikiongozwa na mambo makuu matatu: ulinzi wa maisha ya binadamu, uhuru wa wagonjwa na uhusiano na huduma ya tiba. Lakini kwa bahati mbaya, mwongozo huu hauna rejea hata kidogo kwa Mwenyezi Mungu ambaye ndiye asili na hatima ya maisha ya mwanadamu; Maandiko Matakatifu, ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini na kwamba, mwongozo una kasoro kubwa kuhusu mwono wa maisha ya mwanadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Jitihada za Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji, ili kuweza kupata ufumbuzi wa tatizo na changamoto hii, hazikuweza kufua dafu tangu mwaka 2017 hadi wakati huu.

Hospitali hizi zilipaswa kusimama kidete kulinda na kutetea uhai wa binadamu, lakini badala yake, zimekengeuka na hatimaye, kumezwa na utamaduni wa kifo unaotekelezwa kwenye Hospitali zinazosimamiwa na kuendeshwa na Shirika la Kitawa ndani ya Kanisa! Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, kifolaini au “eutanasia” ni mauaji yanayokwenda kinyume kabisa cha Sheria ya Mungu, kwa sababu yanakinzana na kanuni maadili pamoja na utu wema. Kifolaini ni kinyume cha Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anakazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wagonjwa wanapaswa kuonjeshwa huruma, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huruma na upendo kwa wagonjwa, hauwezi kamwe kukumbatiwa katika utamaduni wa kifolaini. Kanisa Katoliki linafundisha kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Kanisa linathamini na kuguswa na mateso na mahangaiko ya wagonjwa kama sehemu ya ushiriki wao katika mateso ya Kristo. Kimaadili na kiutu, kifolaini, kamwe hakiwezi kukubalika kuingizwa katika mfumo wa huduma ya afya inayotolewa na Kanisa. Ni katika mazingira haya tete, Hospitali hizi zimeshindwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wagonjwa wa afya ya akili wamekuwa ni wahanga wa utamaduni wa kifo nchini Ubelgiji kwa kuwanyima wamiliki wa hospitali uwezo wa kulinda maisha ya wagonjwa wao kisheria. Askofu Johannes Willibrordus Maria Hendriks alifanya ziara ya kitume kwenye hospitali hizi, ili kuzikagua, lakini ziara hii haikuzaa matunda yanayokusudiwa. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema, kwa vile hospitali za wagonjwa wa afya ya akili za Shirika la Mabruda wa Upendo zilizoko nchini Ubelgiji zimeshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kutetea uhai na badala yake, zimekumbatia utamaduni wa kifo kwa kukubali kifolaini, tangu sasa na kuendelea, hazitahesabika kuwa ni hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki.

Kifolaini
02 July 2020, 14:31