Kardinali Pietro Parolin, tarehe 30 Juni 2020 amekutana na kuzungumza na Mabalozi wa Israeli na Marekani mjini Vatican kuhusu uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israeli na Palestina. Kardinali Pietro Parolin, tarehe 30 Juni 2020 amekutana na kuzungumza na Mabalozi wa Israeli na Marekani mjini Vatican kuhusu uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israeli na Palestina. 

Vatican: Uhusiano Kati ya Israeli na Palestina ni Tete Sana!

Vatican imeelezea kuhusu hatari inayoonekana mbeleni, inayoweza kugumisha mchakato wa kutafuta amani ya kudumu kati ya Israeli na Palestina pamoja na kuzingatia hali nzima ya Ukanda wa Mashariki ya Kati. Kama ilivyowahi kujitokeza 20 Novemba 2019 na kujirudia tena tarehe 20 Mei 2020. Israeli na Palestina ni Mataifa mawili yanayopaswa kuwepo na kuishi kwa amani na usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 30 Juni 2020 amekutana na kuzungumza na Mabalozi wa Marekani na Israeli mjini Vatican. Lengo la mkutano huu, lilikuwa ni kuelezea wasiwasi wa Vatican kuhusu hatari inayoonekana mbeleni, inayoweza kugumisha mchakato wa kutafuta amani ya kudumu kati ya Israeli na Palestina pamoja na kuzingatia hali nzima ya Ukanda wa Mashariki ya Kati. Kama ilivyowahi kujitokeza tarehe 20 Novemba 2019 na kujirudia tena tarehe 20 Mei 2020, Vatican inapenda kuonesha msimamo wake kwa kutambua kwamba, Israeli na Palestina ni Mataifa mawili yanayopaswa kuwepo na kuendelea kuishi kwa amani na usalama kwa kuzingatia mipaka ya nchi hizi mbili inayotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari inabainisha kwamba, Vatican inapenda kuwahamasisha wadau wote wanaohusika kwenye mgogoro huu, kujielekeza zaidi katika kuanzisha majadiliano ya kisiasa, kwa kuzingatia itifaki zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, huku zikisaidiwa na juhudi mbali mbali ili, kurejesha tena imani kati ya pande hizi mbili. Kardinali Parolin anasema, huu ni wakati wa kujikita katika ujasiri wa kukubali kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi pamoja na kukataa katu katu falsafa ya kutumia vita. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni wakati wa kukubali majadiliano katika ukweli na uwazi na kufutilia mbali chuki na uhasama. Umefika wakati wa kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa kwa kuondokana na vitendo vinavyoweza “kutibua nyongo” na huo ukawa ni mwanzo wa vita na kinzani. Huu ni wakati wa kujikita katika ukweli na uwazi kwa kuondokana na unafiki!

Israeli na Palestina

 

02 July 2020, 14:13