Dr. Paolo Ruffini, anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kujenga na kudumisha: umoja, ukweli, mshikamano na uaminifu kwani mawasiliano ni vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Dr. Paolo Ruffini, anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kujenga na kudumisha: umoja, ukweli, mshikamano na uaminifu kwani mawasiliano ni vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. 

Changamoto kwa Wadau wa Tasnia ya Mawasiliano Barani Afrika!

Baraza la Kipapa la Mawasiliano liko bega kwa bega pamoja nao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, Barani Afrika. Dr. Paolo Ruffini, amekazia umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Vitoe: matatizo, changamoto, fursa na matumaini ya Bara la Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa kitume “Africae Terrarum” yaani “Bara la Afrika” uliochapishwa kunako tarehe 29 Oktoba 1967, anakazia pamoja na mambo mengine: Utajiri, amana na urithi mkubwa wa Mapokeo kutoka Barani Afrika sanjari na mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mtakatifu Paulo VI, alihimiza umoja na mshikamano kama chachu ya maendeleo endelevu na fungamani, kwa kutambua kwamba, Bara la Afrika lilikuwa limebarikiwa kuwa na tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiroho, kiutu na kijamii. Hizi ni tunu ambazo zinapaswa kuendelezwa ili kupambana na ubaguzi, ukabila, udini, vita na misigano, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kufutilia mbali maadui wakuu wa Afrika ambao ni ujinga, umaskini na maradhi.

Mtakatifu Paulo VI alionesha pia matumaini ya Bara la Afrika wakati ambapo nchi nyingi zilikuwa zinajipatia uhuru wake; vikwazo na vizingiti ambavyo vilikuwa mbele yao na kwamba, maendeleo na msaada wa hali na mali ni mambo msingi katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwataka wakleri na watawa kujikita zaidi katika utamadunisho na huduma makini kwa watu wa Mungu, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa viongozi wa Serikali, aliwataka kukuza na kudumisha uhuru wa kidini, demokrasia na uhuru wa kweli na kwamba, wanazuoni na wasomi, wasadake maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Bara la Afrika. Alizitaka familia kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu, bila kusahau kuheshimu, kulinda na kudumisha haki, utu na heshima ya wanawake wa Bara la Afrika.

Ni katika muktadha huu, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Idhaa ya Kiingereza ya Radio Vatican kwa ajili ya Bara la Afrika, (1950-2020) amependa kuwahakikishia wadau mbali mbali wa mawasiliano Barani Afrika kwamba, Baraza la Kipapa la Mawasiliano liko bega kwa bega pamoja nao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, Barani Afrika. Uzinduzi wa maadhimisho haya umefanyika kwa njia ya mtandao, Ijumaa tarehe 17 Julai 2020 na kuwashirikisha wadau mbali mbali waliokuwa wamejiunga kwa njia ya mtandao. Amekazia umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika mchakato wa ujenzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika.

Huu ni wakati wa mawasiliano ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu, badala ya kuendelea kuwa ni vyombo vinavyoshabikia chuki, uhasama na hali ya watu kutoelewana. Changamoto mamboleo katika sekta ya afya, zinaendelea kuonesha umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii. Ni wajibu wa vyombo hivi kuweza kushughulikia matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili, kuweza kuwa na mwelekeo wenye matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Vyombo vya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 23 Septemba 2019 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano pamoja na wafanyakazi wa vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Katika hotuba yake hiyo aligusia kuhusu: Changamoto za mawasiliano, mawasiliano kama utume wa Kanisa; umuhimu wa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kama timu na kwamba, mfumo wa mawasiliano ya Kanisa unafumbatwa katika ushiriki na kushirikishana kama ushuhuda wa umoja wa Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia na kwamba, Papa Francisko ataendelea kuunga mkono miradi mbali mbali ya ushirikiano kati ya Vatican na Makanisa mahalia.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, rasilimali watu, fedha na vitu vinatumika kikamilifu, ili kupunguza pia gharama za uendeshaji wa sekta ya mawasiliano ndani ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, mawasiliano ndani ya Kanisa ni utume unaoliwezesha Kanisa kuwekeza katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu. Katika muktadha huu, kila karama inapaswa kutumiwa vizuri ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa sanjari na kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko ya kile ambacho Kanisa linatangaza. Wafanyakazi wawe na ujasiri wa kufanya mabadiliko, bila kukata wala kukatishwa tama, kwa kujimanua kutoka kwenye mtego wa usalama usiokuwa na uhakika, tayari kukumbatia changamoto za mbeleni kwa moyo wa matumaini. Katika muktadha huu, wafanyakazi waendelee kuambata kumbukumbu za mambo msingi waliyotenda, tayari kuunganisha nguvu, ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Baba Mtakatifu anaungana na wafanyakazi kumshukuru Mungu kwa nguvu anazowakirimia.

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anawahimiza wadau wa tasnia ya mawasiliano ndani ya Kanisa kujizatiti katika imani, umoja na mshikamano wa dhati, ili kukabiliana na changamoto mamboleo katika sekta ya mawasiliano ya jamii. Hakuna sababu msingi ya kuogopa, wadau wa mawasiliano watambue kwamba, katika ulimwengu mamboleo kuna “utitili wa habari za kughushi”, kumbe, wajibu wao ndani ya Kanisa ni kuhakikisha kwamba, wanatoa habari kwa wakati muafaka; habari ambazo ni za kuaminika kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Kipapa la Mawasiliano linaendelea na mchakato wa kuunda: “Vatican News Agency” yaani: “Wakala wa Habari za Vatican” ili kutoa habari za maisha na utume wa Kanisa kwa uhakika zaidi. Hili litakuwa ni Jukwaa la tasnia ya habari kutoka ndani na nje ya Vatican, jambo ambalo linahitaji ushirikiano wa hali ya juu kabisa.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko  katika Maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2020 umepambwa na kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Kitabu cha Kutoka:10:2. "Maisha yanakuwa ni historia”. Kuhusu mwingiliano wa hadithi na kwamba, si kila hadithi ni hadithi njema. Kuna hadithi ya hadithi; hadithi iliyopyaishwa na hadithi inayoendelea kumpyaisha mwanadamu. Dr. Paolo Ruffini amewataka wadau wa tasnia ya mawasiliano Barani Afrika kutangaza kuhusu: changamoto, matatizo, mafanikio na matumaini ya watu wa Mungu Barani Afrika. Habari hizi zichochee na kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kisiasa na kitamaduni, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ndani ya Kanisa wawe ni mashuhuda wa maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika misingi ya imani tendaji na ukweli unaofumbatwa katika mafungamano ya kijamii, kwa kutambua kwamba, wote wanahitajiana, wanakamilishana na wanapaswa kusaidiana kwa dhati.

Sauti ya watu wa Mungu Barani Afrika inapaswa kufika masikioni mwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni wakati wa ujenzi wa jukwaa la mawasiliano linalosimikwa katika umoja na mshikamano ili kufyekelea mbali “virusi” vya kinzani, migawanyiko na mipasuko ya kijamii. Ulimwengu wa kidigitali, uwe ni nyenzo ya kuwaunganisha watu na wala si vinginevyo! Ni muda wa kujenga umoja katika utofauti, ili kudumisha udugu wa kibinadamu, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati! Kila watu wawajibike barabara kwa wale waliko Roma, waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza na wale wanaotekeleza dhamana na wajibu wao Barani Afrika, waendelee kuchakarika usiku na mchana. Ni muda wa kusaidiana na kushirikiana ili kujenga na kudumisha Jumuiya na kwamba, Baraza la Kipapa la Mawasiliano liko tayari kushirikiana na wadau wa tasnia ya mawasiliano Barani Afrika. Katika mchakato wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Idhaa ya Kiingereza ya Radio Vatican kwa ajili ya Bara la Afrika kwamba, “TUKO PAMOJA”.

The recorded YouTube of Webinar can be found at this link:

https://www.youtube.com/watch?v=YmiH9mMU3vg

Dr. Ruffini. English Africa 70 Years
18 July 2020, 14:37