Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia limeundwa ili kutekeleza maazimio na mapendekezo ya Mababa wa Sinodi kwa Ajili ya Ukanda wa Amazonia iliyofanyika Oktoba, 2019. Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia limeundwa ili kutekeleza maazimio na mapendekezo ya Mababa wa Sinodi kwa Ajili ya Ukanda wa Amazonia iliyofanyika Oktoba, 2019. 

Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia: Utekelezaji wa Sinodi!

Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, limeanzishwa wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani. Lengo ni kukazia dhana ya unabii na utume wa kimisionari ambao Mama Kanisa hana budi kuuendeleza hadi miisho ya dunia. Huu ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko! Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6 - 27 Oktoba, 2019 yaliongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Mababa wa Sinodi walipitia, wakajadili na hatimaye wakapigia kura vipengele vyote na kupitisha Hati ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019. Hati hii ikaongozwa na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani”. Baada ya kusali, kutafakari na kusikiliza kwa makini, sasa ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, shughuli za kichungaji na kitamaduni. Kanisa liliangalia pia njia mpya za wongofu Ukanda wa Amazonia pamoja na kutoa hitimisho la Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Querida Amazonia”, yaani “Wapendwa watu wa Ukanda wa Amazonia” uliochapishwa tarehe 12 Februari 2020 anagusia kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa ndoto ya jamii, ndoto ya kitamaduni, ndoto ya kiekolojia, ndoto ya Kikanisa na hatimaye, anamwonesha Bikira Maria kuwa ni Mama wa Ukanda wa Amazonia. Itakumbukwa kwamba, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, walipendekeza kuundwa kwa Baraza litakalosaidia kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, kuanzia tarehe 26 hadi 29 Juni 2020, wajumbe kutoka kwenye “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM” wameunda Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia.

Kwa mara ya kwanza, wajumbe wa mkutano huu, wameshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii, hali inayowapatia jeuri ya kutembea kwa pamoja na kusonga mbele kwa ari, moyo mkuu na matumaini, huku wakitekeleza ile dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, limeanzishwa wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani. Lengo ni kukazia dhana ya unabii na utume wa kimisionari ambao Mama Kanisa hana budi kuuendeleza hadi miisho ya dunia. Huu ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hili ni tukio la matumaini ya Mababa wa Sinodi wakiwa wameunganika na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwa nao bega kwa bega katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Wajumbe wa Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia wanaoesha umoja katika utofauti wao kama ulivyofafanuliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Kuna wajumbe kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, kama kielelezo cha umoja na mshikamano na watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Ni matumaini ya wajumbe wa  Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia kwamba, Vatican itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na  watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Hili ni Baraza ambalo tayari limekwisha kuunda Katiba yake. Katika hali na mazingira haya, Kardinali Claudio Hummes, OFM, amechaguliwa kuwa Rais wa kwanza Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia. Kardinali Claudio Hummes, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Sao Paulo, Brazil, ambaye pia aliwahi kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, alikuwa pia Mwezeshaji mkuu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Askofu David Martinez De Aguirre Guinea, O.P. wa Jimbo Katoliki la Puerto Maldonado nchini Perù amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais. Wakati wa maadhimisho ya Sinodi alikuwa ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni kati ya Makatibu maalum. Wajumbe wa Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia wanasema, bado janga kubwa la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 linaendelea “kufyeka na kuteketeza maisha ya watu wengi Ukanda wa Amazonia. Hapa kuna umuhimu wa toba na wongofu wa kiekolojia. Baraza linataka kuwa ni sauti ya Habari Njema, kwa kusikiliza na kujibu kilio Mama Dunia na Maskini, Ukanda wa Amazonia. Baraza linapania pamoja na mambo mengine, kutekeleza kwa dhati maamuzi na mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia. Baraza linataka kujielekeza zaidi, ili kuwa ni daraja la utekelezaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; kiuchumi, kijamii na kimazingira ndani na nje ya Ukanda wa Amazonia.

Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia

 

01 July 2020, 14:08