Ujumbe wa Vatican kwenye Mkutano wa OSCE umekazia kuhusu: Uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kupata habari kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Ujumbe wa Vatican kwenye Mkutano wa OSCE umekazia kuhusu: Uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kupata habari kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu. 

Vatican: Uhuru wa Vyombo vya Habari; Kujieleza na Kupata Habari!

Jumuiya za Kidini hazina budi kupewa nafasi ya kushiriki katika majadiliano ya hadhara kwa wakati muafaka. Wawakilishi wa dini mbali mbali duniani hawana budi kupewa fursa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii kuweza kutoa maoni yao mintarafu: imani, kanuni maadili na utu wema. Kamwe vyombo vya mawasiliano visitumike kwa ajili ya masilahi ya watu wachache ndani ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano wa Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, OSCE, hivi karibuni, kwa mara ya kwanza umechangia kwa kina na mapana kuhusu umuhimu wa kudumisha: Uhuru wa kujieleza; Uhuru wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa kupata habari kama sehemu muhimu ya haki msingi za binadamu. Mkutano huu umefanyika huko Vienna, Austria. Mkutano huu uliandaliwa kwa ushirikiano na Ofisi kwa ajili ya Taasisi za Demokrasia na Haki Msingi za Binadamu (ODHIR) na Wawakilishi wa Uhuru wa Vyombo vya habari (RfoM) ambao walichangia na hatimaye, kufanikisha mjadala huu unaopania pamoja na mambo mengine kukoleza: ukweli, uhuru, haki na mshikamano katika jamii.

Vyombo vya mawasiliano ya jamii, havina budi kupewa uhuru wa kutosha pamoja na kulindwa, mintarafu sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa. Lakini, inapaswa kukumbukwa kwamba, kila haki msingi ya binadamu inawajibisha pia. Huu ni ukweli ambao hauwezi kufumbiwa macho. Uhuru wa vyombo vya mawasiliano ya jamii havina budi kuhakikisha kwamba, vinazingatia kanuni msingi za maadili na utu wema kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na jumuiya ya mwanadamu, kama walengwa na hatima ya mchakato mzima wa mawasiliano ya jamii. Mawasiliano yasaidie kujenga na kukuza mafungamano ya kijamii kati ya watu, ili hatimaye, kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Vyombo vya mawasiliano ya jamii ni nyenzo msingi zinazotumiwa na binadamu kwa ajili ya maendeleo. Ni katika muktadha huu, ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu umeonesha uhusiano uliopo kati ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa dini.

Inasikitisha kuona kwamba, uhuru wa kujieleza unatumiwa kuhalalisha vitendo vya ubaguzi, chuki na uhasama dhidi ya dini au waamini wa dini mbali mbali. Uhuru wa kujieleza hauna budi kutoa nafasi kwa waamini kutoa maoni yao, kwa kuwaheshimu jirani zao bila ya “kuogopa macho na maneno ya watu” hata kama mawazo haya yanasigana na mkondo wa mawazo mamboleo. Pamoja na yote haya, vyombo vya mawasiliano ya jamii havina budi kutoa taarifa ambayo inakita mizizi yake katika ukweli na usawa kuhusu mambo ya kidini. Ujumbe wa Vatican unapenda kuwatia shime wajumbe kutoka Ofisi kwa ajili ya Taasisi za Demokrasia na Haki Msingi za Binadamu (ODHIR) na Wawakilishi wa Uhuru wa Vyombo vya habari (RfoM), kuhakikisha kwamba, wanatoa mwongozo utakaotumika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, ubora na weledi vinazingatiwa.

Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na mchakato wa ujenzi wa maridhiano kati ya watu pamoja na kuondokana na mifumo mbali mbali ya ubaguzi. Vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinapaswa kuwa ni jukwaa linalotoa fursa kwa watu mbali mbali kushirikisha mawazo yao ya kisiasa, kidini na kiimani, kama njia ya watu kutajirishana. Jumuiya za Kidini hazina budi kupewa nafasi ya kushiriki katika majadiliano ya hadhara kwa wakati muafaka. Wawakilishi wa dini mbali mbali duniani hawana budi kupewa fursa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii kuweza kutoa maoni yao mintarafu: imani, kanuni maadili na utu wema. Kamwe vyombo vya mawasiliano ya jamii visitumike kwa ajili ya masilahi ya watu wachache ndani ya jamii. Wawakilishi wa dini mbali mbali walishirikishe maoni yao kuhusu kanuni maadili na utu wema. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa makini na matumizi ya internet na mitandao ya kijamii ambayo mara nyingi imetumiwa kwa ajili ya kusambaza kashfa dhidi ya dini nyingine na ibada zao.

Wamiliki na wasambazaji wa mitandao ya kijamii, wanapaswa kuongoza na kanuni ya ukweli na uwazi, ili kuondokana na mifumo ya ubaguzi au maneno ya kashfa yanayoweza kuchochea hali ya watu kushindwa kuvumiliana. Wakati wa janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosabanishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, lilipokuwa limepamba moto, Jumuiya ya Kimataifa imeshuhudia jinsi ambavyo kumekuwepo na usambazaji wa habari usiokuwa na uwiano mzuri, hali ambayo imesababisha mateso na mahangaiko makubwa ya watu, sehemu mbali mbali za dunia. Kuna ombwe kubwa kati ya ulimwengu wa kidigitali na wale ambao bado wanatumia mfumo wa analogia; kati ya nchi tajiri zaidi duniani na nchi zinazoendelea. Ukosefu wa habari sahihi kwa wakati muafaka, ni jambo linaloweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kumbe, kuna haja kwa wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, wanawajibika barabara, kwa kuzingatia ukweli na uwazi sanjari na kuendelea kuboresha takwimu zao,  ili kuonesha hali halisi badala ya watu kusambaziwa habari za kughushi na hivyo kusababisha hofu na taharuki kubwa kati ya watu wa Mataifa.Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo ambayo yanapaswa kupewa msukumo wa pekee katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Haki jamii na maendeleo fungamani ya binadamu ni mambo muhimu katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini duniani na hivyo kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kupata habari wanazohitaji kwa wakati muafaka.

Vyombo vya Habari

 

 

27 June 2020, 07:34