2020.06.13 Kardinali Turkson katika ziara ya kambi ya wakimbizi 2020.06.13 Kardinali Turkson katika ziara ya kambi ya wakimbizi 

Turkson atembelea watu wasio na makazi rasmi kando ya Roma!

Kardinali Turkson ameshiriki ziara ya kutembelea kambi moja ya wakimbizi kandoni mwa jiji la Roma kwa kuwapelekea vifaa vya kujikanga na maambukizi ya virusi kama vile barakoa glavu na madawa.Hawa ni watu wanaoshi maisha magumu ya mateso na ambao mara nyingi wamesahaulika kwa mujibu wa maelezo yake.Kambi hiyo inaishi watu karibia 600 na nusu yake ni watoto katika mazingira magumu.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Katika harakati nyingi za Kanisa  za kuwa karibu na walio wa mwisho, zinaendelea kwa kasi kuwa karibu hata na na watu wasio kuwa na makazi rasmi kwenye mitaa mibovu kandoni mwa jiji la Roma. Kardinali Peter K.A. Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Watu, tarehe 13 Juni 2020 amefanya ziara yake katika Kambi ya Castel Romano, iliyo  kandoni kidogo na mji  wa Roma ili kushuhudia  na kupeleka mshiakamano na ukaribu wa Papa kwa watu hawa kukutana na familia, mama wengi na watoto wao  wadogo wanaoishi katika majengo ambayo mara nyingi wanahisi kubaguliwa.

Tendo la kuwekwa karantini kutokana na virusi vya corona halikusimamisha jitihada za Kanisa licha ya ugumu wa shughuli zake za maandalizi na watu wa kujitolea ambao waliendelea kushirikiana kwa ajili ya watu hawa. Huko Castel Romano wanaishi watu wasio na makazi rasmi 600  na nusu yake ni watoto wadogo. Kwa upande wao, Kardinali Turkson amepeleka mchango kutoka Duka la Madawa Vatican, pia kutoka kwa Wafadhili wa  wa Tume ya Vatican kwa ajili ya Covid-19 iliyoundwa na Baraza hilo, vifaa mbali mbali vya kinga ikiwemo glavu 3000, barakoa 6000 za kimatibabu zilizotengenezwa kwa  vitambaa ambazo zinaweza kufuliwa, na box 500 za dawa ya Paracetamol. Kwa maana hiyo madawa na vifaa vya kujilinda vilivyo muhimu katika kipindi hiki cha baada ya janga vimewafikia watu hawa. Shukrani kwa “Chama cha 21 Luglio” ambacho kwa miaka sasa wanashughulikia watu hao wamewakabidhi mabox 260 ya vitu msingi hasa kwa ajili ya watoto kuanzia miaka 0-3.

Kardinali Turkson baada ya kufika kwanza amekutana na watu wa kujitolea wa Kituo cha Maendeleo ya elimu na utamaduni huko Tor Bella Monica, nje ya Roma.  Ni eneo gumu sana kwa raia wanaoishi na matatizo ya kiuchumi, na ukosefu wa ajira, lakini wakiwa na shauku ya kujikomboa. Baadaye Kardinali alikutana na Askofu wa sehemu hiyo, Askofu Gianpiero Palmieri; na viongozi mbali mbali mbali wanaojihusisha katika sekta hiyo akiwemo mwakilishi wa Hosptali ya watoto Bambino Gesu, kwa maana hiyo: Padre Giovanni De Robertis, Makamu Mkurugenzi wa Migrantes; Askofu Pierpaolo Felicolo, Mkurunzi wa Mfuko wa Migrantes Roma; Dk. Maria Rosaria Giampaolo wa hospitali ya Watoto ya Bambino Gesù. Hali halisi ya kambi hiyo katika mji mkuu wa Roma, imefafanuliwa na  Rais wa Chama cha “21 luglio”, Bwana Carlo Stasolla, kwamba kinahitaji ulinzi mkubwa wa shughuli ya kushirikisha na watu hao.  Kila wiki chama hicho kinakabidhi mabox 250 kutoka kwa wafadhili mbalimbali binafsi.

Kama Papa Francisko mara nyingi anavyorudia kusema kuwa hakuna yoyote abaki nyuma, Kardinali Turkson amewambia kuwa “ tumekuja hapa leo hii kushuhudia msaada kwa wote ambao wanaishi katika hali ya mateso na kuathirika na mara nyingi waliosahauliwa hasa katika kipindi hiki cha kiafya, kijamii na kiuchumi.Tukumbuke kuwa maendeleo fungamani ya binadamu yamesukana pamoja na utunzaji bora wa mazingira, kwa maana kushindwa kwa mmoja ni sawa na kushindwa kwa mwingine. Katika kambi hiyo ya Castel Romano maji yanapelekwa kwa magari, hata umeme wanatumia generator ambayo wakati mwingine haiwaruhusu kufanya shughuli nyingine. Watoto ambao wanakwenda shuleni kila mara ni asilimia 15%. Na wakati wa kuzuka janga la virusi, kujifunza kwao kwa umbali kumekuwa ni vigumu, kwa maana kompyuta na unganisho la mtandao havipo.

Nyumba zenyewe ni mbovu, wengine walala kwenye container, kwa njia hiyo panafanaa na mtaa mbovu sana. Kardinali ameingia katika nyumba hizi, na kukutana na mama  maman a watoto.  Watu wengi ambao wanaishi eneo hilo la Castel Romano walikimbia wakati wa vita vya Bosnia na kwa maana hiyo hawa ni wakimbizi ambao hawana makazi rasmi. Ili kuwasaidia kwa mtazamo wa matibabu, wafanyakazi wa Hospitali ya Kipapa ya  Bambino Gesù Roma, kwa kutumia gari moja katika kambi “Usinisahau” wameweza kutibu watoto 700 ambao wanaishi katika kambi hii.

14 June 2020, 14:00