OSCE: Rushwa na Ufisadi ni adui mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. OSCE: Rushwa na Ufisadi ni adui mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. 

OSCE: Rushwa na Ufisadi ni Adui wakubwa wa Ustawi na Mendeleo!

Vatican inapenda kukazia: Ulinzi na usalama; Amani na Utulivu; Ustawi na Ukuaji wa Uchumi katika Ukanda wa Nchi za OSCE. Lengo ni kuhakikisha kwamba, nchi wanachama zinajizatiti zaidi katika kupambana na rushwa kwa njia ya ubunifu, kwa kuongeza kiwango cha uwajibikaji katika ukweli na uwazi pamoja na matumizi ya mfumo wa kidigital Rushwa na Ufisadi ni hatari kwa utawala bora!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano wa Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, OSCE, Jumanne, tarehe 15 Juni 2020 umesema kwamba, Vatican inapenda kukazia kwa namna ya pekee: Ulinzi na usalama; Amani na Utulivu; Ustawi na Ukuaji wa Uchumi katika Ukanda wa Nchi za OSCE. Lengo ni kuhakikisha kwamba, nchi wanachama zinajizatiti zaidi katika kupambana na rushwa kwa njia ya ubunifu, kwa kuongeza kiwango cha uwajibikaji katika ukweli na uwazi pamoja na matumizi ya mfumo wa kidigitali! Haya ni mawazo makuu yanayopaswa kufanyiwa kazi kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya mkutano wa OSCE ambao umepangwa kuwa kama Jukwaa la kuzungumzia masuala ya kiuchumi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ujumbe wa Vatican unakiri na kutambua uwepo wa janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Madhara yake katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kimazingira yameanza kuonekana katika Nchi wanachama wa OSCE. Madhara yake yamegusa na kutikisha maisha ya mtu binafsi, jamii, na hata kufikia ngazi ya kimataifa. Jambo la kufurahisha ni kuona kwamba, nchi wanachama wa OSCE zimeanza kujizatiti katika kupambana na rushwa pamoja na ufisadi; mambo msingi yanayofumbatwa katika utawala bora. Ujumbe wa Vatican umekumbusha kwamba, vitendo vya rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni kati ya mambo yanayotishia tunu msingi za maisha ya nchi wanachama wa OSCE. Vitendo hivi vyote, vimeendelea kudhohofisha sekta mbali mbali za maisha, kiasi hata cha kutikisa amani na utulivu; ulinzi na usalama; uchumi na tunu msingi za maisha ya watu. Rushwa na ufisadi ni vitendo ambavyo vimeacha madonda makubwa katika maisha ya kijamii na vinaendelea kumong’onyoa misingi bora ya uchumi; kanuni maadili na utu wema.

Ni vitendo vinavyowajengea watu ombwe la kutaka kupata utajiri wa mali na fedha kwa njia ya mkato, lakini madhara yake ni makubwa kwa watu wengi zaidi. Ni vitendo ambavyo vinaendelea kumong’onyoa taratibu hali ya watu kuaminiana, umuhimu wa utekelezaji wa utawala bora unaozingatia kanuni, sheria na taratibu za nchi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, rushwa na ufisadi ni mambo ambayo yanapekenyua: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Jamii inapaswa kusimama kidete kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi katika mifumo yake mbali mbali. Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu wa maandalizi unaendelea kufafanua kwamba, viongozi wa serikali na umma katika ujumla wake, wanapaswa kujipambanua kwa kujenga mahusiano na mafungamano kati ya wananchi na taasisi za umma na za Serikali.

Mwelekeo wa wananchi kutokuwa na imani na Serikali zao, ni chanzo cha kudhohofisha mchakato wa ujenzi wa demokrasia. Ustawi, mafao na maendeleo ya wengi ni mambo msingi yanayopaswa kulindwa na kusimamiwa. Katika hali na mazingira kama haya, Serikali zinapaswa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake mkamilifu kwa kuhakikisha kwamba, utawala bora na unaozingatia sheria za nchi unafuatwa na wote. Katika mapambano dhidi ya janga kubwa la maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kipaumbele cha kwanza ni ulinzi na usalama wa afya ya wananchi. Kama Jumuiya ya Kimataifa haitakuwa macho na makini, ugonjwa wa Corona, COVID-19 unaweza kuwa ni mazalia makubwa ya rushwa na ufisadi kwa kujiingiza na kujipenyeza katika mchakato mzima wa manunuzi usiozingatia sheria, kanuni na taratibu. Hata kama janga la Corona, COVID-19 ni tishio kwa Jumuiya ya Kimataifa, lakini, kuna haja ya kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuibua sera na mbinu mkakati za kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, vinavyoweza kuvishwa blanketi la kisiasa. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanapewa kipaumbele cha kwanza!

Rushwa na Ufisadi
16 June 2020, 14:41