Tafuta

Vatican News
Katika ya Kitume: Vultum Dei Quaerere iliyochapishwa mwaka 2016 inafafanua mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na watawa wa ndani: tarehe 7 Juni 2020, Hispania imeadhimisha Siku ya Watawa wa Ndani. Katika ya Kitume: Vultum Dei Quaerere iliyochapishwa mwaka 2016 inafafanua mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na watawa wa ndani: tarehe 7 Juni 2020, Hispania imeadhimisha Siku ya Watawa wa Ndani. 

Katiba ya Kitume: Mambo Msingi kwa Maisha ya Watawa wa Ndani!

Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume ya "Vultum Dei Quaerere" yaani "Kuutafuta Uso wa Mungu" anakazia umuhimu wa: Majiundo kwa watawa; sala binafsi na sala za kijumuiya; Tafakari ya Neno la Mungu; Toba na Wongofu wa ndani sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani! Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume ya “Vultum Dei Quaerere” Yaani “Kuutafuta Uso wa Mungu” uliochapishwa kunako mwaka 2016 kwa ufupi anasema: kuna haja ya kudumisha majiundo makini; umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu; vigezo muhimu kwa Jumuiya ya Kimonaki ili kuweza kujitegemea pamoja na uwezekano wa kuunda Shirikisho la Wamonaki ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakazia majiundo makini: awali na endelevu bila kushikwa na kishawishi cha kutafuta idadi na mafanikio na kwamba, malezi yanahitaji muda na nafasi kubwa zaidi, yaani kati ya miaka tisa hadi kumi na miwili. Pili ni umuhimu wa Sala kwani hiki ni kiini cha maisha na utume wa Wamonaki na wala si hali ya mtawa kujiangalia mwenyewe. Mwaliko ni kupanua wigo ili kuweza kuwakumbatia watu wengi zaidi hasa wale wanaoteseka na kusumbuka katika maisha yao, yaani maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa tafakari ya Neno la Mungu, chemchemi ya maisha ya kiroho na kiungo makini cha maisha ya kijumuiya, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wamonaki. Tafakari ipewe kipaumbele cha pekee kwa mtawa mmoja mmoja na jumuiya katika ujumla wake, ili kutambua na kumwilisha mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Wamonaki wawe makini kusoma alama za nyakati ili kung’amua mapema mambo yanayoweza kuwapeleka mbali na mapenzi ya Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu haina budi kumwilishwa katika matendo, kwa kujisadaka kwa ajili ya wengine katika upendo. Baba Mtakatifu anawataka wamonaki kuadhimisha Fumbo la Ekaristi na Sakramenti ya Upatanisho kwa kuwa na mwendelezo wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Toba na wongofu wa ndani ni mahali muafaka pa kutafakari Uso wa huruma ya Mungu na msamaha ili kuwa kweli ni manabii na mitume wa huruma ya Mungu na vyombo vya upatanisho, msamaha na amani; mambo ambayo ulimwengu unahitaji sana kwa nyakati hizi!” Papa anahimiza sala na kazi yaani: “Ora et Labora”. Hapa kazi inapaswa kutambuliwa kuwa ni mchango katika kazi ya uumbaji, huduma makini kwa binadamu na mshikamano na maskini, kwa kuwa na uwiano mzuri wa ushirikiano katika masuala haya yanayotekelezwa kila siku ya maisha. Baba Mtakatifu anatambua na kuthamini maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano duniani na mchango wake katika uundaji wa mawazo na mahusiano ya watu duniani. Vyombo vya mawasiliano ni muhimu katika majiundo na mawasiliano ya kijamii, lakini hapa wamonaki wanapaswa kuwa na kiasi katika matumizi ya vyombo hivi vya mawasiliano ya kijamii, ili visiwe ni sababu ya kukwepa wajibu wa maisha ya kijumuiya, kukosa mwelekeo; kuathiri wito au kuwa ni kikwazo katika maisha ya taamuli.

Baba Mtakatifu anasema, ukimya ni usikivu unaopata mwanga kutoka katika Neno la Mungu. Ni kielelezo cha utupu wa ndani ili kuunda mazingira ya kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni ukimya unaomsikiliza Mungu na kilio cha binadamu! Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa kwani alifaulu kulipokea Neno la Mungu kwa sababu alikuwa ni mwanamke mkimya na ukimya wake ulisheheni utajiri wa upendo. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, katika Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Jumapili tarehe 7 Juni 2020 limeadhimisha pia Siku ya Kitaifa ya Kuombea Watawa wa Ndani, “Pro Orantibus”. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni Bikira Maria, katika maisha na utume wa Kanisa. Watawa wanaalikwa kumwangalia Bikira Maria kama mfano bora wa maisha ya sala na tafakari. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ni wajibu wa watawa wa ndani, kuitika na kufuata wito wao ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwa upande wake, Mama Kanisa ataendelea kuwasindikiza watoto wao kwa njia ya upendo, mshikamano na tunza ya kimama, hatua kwa hatua na hasa wakati wa shida na changamoto za maisha.

Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, maisha yake, yalifichwa machoni pa wengi na hivi ndivyo ilivyo hata kwa watawa wa ndani katika maisha na utume wao. Lakini uwepo wao ni sawa na mwangaza unaong’aa, pande zote za dunia. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linabainisha kwamba, Bikira Maria ni kumbukumbu ya pekee ya upendo wa Mungu wenye huruma. Maisha yake yalisheheni tafakari zilizohifadhiwa kwenye “sakafu ya moyo wake”. Ni mwanga angavu kwa maisha na utume wa Kanisa na hasa wakati giza nene linapowagubika watoto wa Kanisa na kuanza kutembea katika giza na uvuli wa mauti. Ikumbukwe kwamba, Bikira Maria ni kielelezo cha imani na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Watawa kwa njia ya sala na tafakari katika ukimya, wanaendelea kuwa ni mwanga angavu na mapito kwa watu wa Mungu. Watawa wa ndani wanapaswa kudumu katika sala, tafakari ya Neno la Mungu na kwa kuwa na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa.

Uvumilivu na udumifu wa maisha na utume wa Watawa wa ndani ni muhimu sana katika kukabiliana na matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia. Watawa wa ndani wawe ni mfano bora wa kuigwa, kama vyombo na mashuhuda wa furaha ya Habari Njema ya Wokovu. Maisha ya kila siku, yawe kama ni “Divai Mpya” ya Furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya.

Siku ya Watawa Hispania

 

10 June 2020, 12:46