Vatican News
WHO: Wazee wengi wamepoteza maisha kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19 na wengi wao ni wale waliokuwa wanahudumiwa kwenye nyumba za kutunzia wazee Barani Ulaya. WHO: Wazee wengi wamepoteza maisha kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19 na wengi wao ni wale waliokuwa wanahudumiwa kwenye nyumba za kutunzia wazee Barani Ulaya.  (©Africa Studio - stock.adobe.com)

WHO: Waathirika Wakuu wa COVID-19 Barani Ulaya ni Wazee!

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO, Kanda ya Ulaya zinaonesha kwamba, takribani asilimia 50% ya waathirika wote wa Janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVUID-19 ni wazee na kwamba, wengi wao wamepoteza maisha katika nyumba za kutunzia wazee Barani Ulaya. Uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha vifo vya wazee Ulaya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wazee watambue kwamba, Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja nao. Katika hali hii, tete, wazee wengi wametekelezwa na watoto pamoja na ndugu zao. Baba Mtakatifu Francisko, anawaalika wazee hawa kuwasemehe wote hawa kutoka katika undani wa mioyo yao! Mwenyezi Mungu amewakirimia hekima, maisha na historia na kwamba, Kanisa liko karibu nao kwa njia ya sala na sadaka yake. Baba Takatifu katika mahubiri yake ya hivi karibuni amezungumzia kuhusu umuhimu wa kusamehe daima, jambo ambalo si kawaida katika maisha ya binadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna watu ambao wana tabia ya kuwahukumu wenzao, lakini Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kujenga utamaduni wa kusamehe kutoka katika sakafu ya mioyo na hatimaye, kusahau. Umoja, udugu na mshikamano kati ya ndugu ni katekesi ambayo Kristo Yesu aliitoa kwa wanafunzi wake.

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO, Kanda ya Ulaya zinaonesha kwamba, takribani asilimia 50% ya waathirika wote wa Janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVUID-19 ni wazee na kwamba, wengi wao wamepoteza maisha katika nyumba za kutunzia wazee Barani Ulaya. Dr. Hans Henri P. Kluge, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Ulaya anasema kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuweza kubainisha ni nini chanzo cha matatizo yaliyopelekea kiasi kwamba, wazee wengi kupoteza maisha katika nyumba za kutunzia wazee Barani Ulaya. Inasikitisha kuona kwamba, wafanyakazi katika nyumba za kutunzia wazee wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira tete na wakati mwingine bila hata ya kuwa na vifaa tiba kwa ajili ya ulinzi na usalama mahali pa kazi. Madaktari wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya ni kati ya makundi ambayo yako kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa na ugonjwa wa homa ya mapafu unayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Mama Kanisa katika maisha na utume wake, amekuwa na jicho la pekee katika ulinzi, tunza na huduma kwa wazee sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, mshikamano na mafungamano ya kijamii kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee ni muhimu sana katika tamaduni za watu mbali mbali duniani. Vijana wanapaswa kujenga utamaduni wa kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa wazee, kwa kutambua kwamba, wazee, wamechangia kwa kiasi kikubwa mafaniko katika maisha yao. Heshima, upendo, huduma na nidhamu kwa wazee ni jambo ambalo limekuwa likipewa umuhimu wa pekee na jamii nyingi duniani, lakini katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kumeeanza kujitokeza mwelekeo potofu wa kutowajali wala kuwathamini wazee.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anawakumbusha watu wa Mungu kwamba, kwa asilibinadamu ni dhaifu sana na kwa bahati mbaya, sekta ya huduma ya afya “haijafua dafu” kutoa huduma msingi anazohitaji mwanadamu. Ni kweli kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba kwa mwanadamu, lakini bado kuna changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na wote! Janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni mfano hai kabisa. Hata katika nchi zilizoendelea duniani, kumejitokeza uhaba mkubwa wa miundo mbinu na vifaa tiba kama vile mashine za kusaidia wagonjwa kupumua “Ventilators”. Kumekuwepo na uhaba mkubwa wa barakoa pamoja na vitakasa mikono! Hizi ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya afya ya binadamu ili kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Mama Kanisa anapenda kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajenga upendo kwa Mungu na jirani zao, kwa kuendelea kujikita katika huduma makini kwa wazee. Wazee wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kulindwa, changamoto ambayo imekuwa ikitolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Watu wajifunze utamaduni wa kuwa na moyo wa shukrani, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa umoja na mshikamano wa upendo na wazee. Vijana wawe mstari wa mbele kuwahudumia wazee, kwani kwa kufanya hivi wanajiwekea akiba kwa siku za usoni. Vijana wanakumbushwa kwamba, kamwe “wasichezee ujana wao kwani fainali iko uzeeni.” Kwa bahati mbaya, nyumba nyingi za wazee Barani Ulaya zinakosa uwepo wa vijana katika huduma.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anasema, nyumbani ni mahali ambapo panapaswa kuwa ni chemchemi ya faraja, upendo na huruma kwa wazee; mahali ambapo watu wengi wamepata: historia, maisha na utambulisho wao! Lakini kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya watu wanamalizia uzee wao katika nyumba za kutunzia wazee, ili kuonja maisha ya pamoja na wazee wengine, kwani vijana nyumbani hawaonekani! Wakati mwingine, wazee wanafanya uamuzi huu mzito kinyume cha utashi wao kwani kwa hakika “nyumbani” ambako kulipaswa kuwa “nyumbani” si nyumbani tena! Wafanyakazi katika nyumbsa za kuwatunzia wazee, wanaendelea kujisadaka usiku na mchana! Wazee wanakosa huruma, upendo na faraja kutoka kwa ndugu na jamaa zao wa karibu! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kuangalia maana ya kuwa mzee katika Karne ya Ishirini na Moja! Baba Mtakatifu anasema, wazee wana ndoto lakini vijana wana unabii; wote wanapaswa kusaidiana ili kukamilishana!

Uzee ni amana na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kamwe uzee si ugonjwa! Upweke hasi unaweza kupelekea watu kutumbukia katika ugonjwa wa Sonona! Upweke hasi unaweza kupata tiba kwa kujikita katika Injili ya upendo na mshikamano; kwa uwepo wa huduma za maisha ya kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwenye Kongamano la Kwanza la Huduma ya Wazee Kimataifa, lililoadhimishwa Mjini Vatican hapo tarehe 31 Januari 2020 alikazia amana na utajiri wa maisha ya wazee kutokana na uzoefu na historia ya maisha yao. Kumbe, kuna haja ya kuthamini uzee kama amana na utajiri wa maisha ya jamii na wala si kuwaona wazee kama watu waliopitwa na wakati au “magari mabovu yanayopaswa kuegeshwa”! Mama Kanisa anataka kuandika kurasa mpya za utakatifu wa maisha, sala na huduma. Wazee ni leo na kesho ya Mama Kanisa; wao pia wameshiriki katika mpango wa kazi ya ukombozi! Hawa ndio akina Ibrahamu na Sara mkewe, Elizabeth na Zakaria, wazazi wake Yohane Mbatizaji. Wazee wote hawa hata katika uzee wao, Mwenyezi Mungu amewatumia kama mashuhuda na vyombo vya historia ya wokovu!

Afya ya Wazee

 

04 June 2020, 08:07