Romania na Vatican zinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Uhusiano wa Kidiplomasia ulioanzishwa kunako mwaka 1929 Romania na Vatican zinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Uhusiano wa Kidiplomasia ulioanzishwa kunako mwaka 1929 

Miaka 100 ya Uhusiano wa Kidiplomasia: Romania na Vatican

Mwezi Juni 2020, Vaticana na Romania zinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya uhusiano wa kidiplomasia ambao unafumbatwa kwa namna ya pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, Ibada kwa Bikira Maria; Ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Romania. Haya ni mahusiano ya kidiplomasia yaliyoanzishwa mara tu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 12 Juni 1920, Miaka 100 iliyopita, Vatican na Romania, zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia. Mwezi Juni 2020, nchi hizi mbili zinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya uhusiano wa kidiplomasia ambao unafumbatwa kwa namna ya pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, Ibada kwa Bikira Maria; Ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Romania. Haya ni mahusiano ya kidiplomasia yaliyoanzishwa mara tu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Tarehe 10 Mei 1927, Vatican na Romania, vikawekeana sahihi kwenye Itifaki ya Makubaliano yaliyoanza kutekelezwa kunako mwaka 1929. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha kwanza katika makubaliano haya, ikizingatiwa kwamba, sehemu kubwa ya wananchi wa Romania ni waamini wa Kanisa la Kiorthodox. Kunako mwaka 1989, utawala wa Kikomunisti uliangushwa, lakini yakafuatia mauaji na madhulumu makubwa dhidi ya Wakristo katika ujumla wao. Mtakatifu Yohane Paulo II akatembelea Romania kunako mwaka 1999 ili kuimaarisha mchakato wa uekumene wa damu, unaofumbatwa katika ushuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2019 alifanya hija ya 30 ya kitume kimataifa nchini Romania iliyoongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu alikwenda nchini Romania kama hujaji na ndugu yao katika Kristo Yesu ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano unaokita mizizi yake katika amana na utajiri wa imani nchini Romania! Hija hii ilikita ujumbe wake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, changamoto na mwaliko wa kuvumbua tena tunu msingi za maisha ya kiroho, katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili familia ya Mungu nchini Romania, iweze kwenda kwa pamoja!

Baba Mtakatifu aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Romania kutembea kwa pamoja katika fadhila ya unyenyekevu, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anataka kushirikiana na kushikamana na waamini katika hija hii, ili kuwahamasisha kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo, kwa kutambua na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa nchini Romania kutokana na uwepo wa Kanisa la Kiorthodox. Hii pia ilikuwa ni sehemu ya kumbukumbu endelevu ya hija iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 1999. Tangu wakati huo, malango ya nchi zenye waamini wengi wa Kanisa la Kiorthodox yakaanza kufunguka.

Changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II ilikuwa ni umoja, hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuimarisha mchakato huu kwa kukazia: Uekumene wa damu unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kiasi hata cha waamini kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hawa ni waamini “wanaofyekelewa mbali” kutokana na ukosefu wa uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini, sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu. Watakatifu wamejenga umoja katika mateso na kifo na sasa wanafurahia maisha na uzima wa milele, changamoto na mwaliko wa kuendelea kufuata nyayo zao! Ni Uekumene wa maisha ya kiroho kwa kuthamini utajiri na amana ya tunu msingi za maisha ya kiroho miongoni mwa waamini wa Makanisa haya mawili.

Huu ni Uekumene wa sala na huduma ya Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea nchini Romania alisema kwamba, nchi hii ni Bustani ya Bikira Maria kwa sababu inapambwa na waamini kutoka katika madhehebu mbali mbali ya Kikristo! Hawa ni waamini wanaotoka Romania, Hungaria, Croatia na Poland. Kuna Waarmenia ambao wengi wao ni waamini wa Kanisa la Kiorthodox. Baba Mtakatifu Francisko aliwaambia wajumbe wa kudumu wa Sinodi ya Kanisa la Kiothodox kwamba, yuko kati yao kwa ajili ya kutafakari, Sura ya Kristo Mteseka, ili kupyaisha matumaini ya watu wa Mungu. Ushuhuda na kifungo cha imani uliwasukuma Mitume Petro na Andrea, ndugu wa damu kutangaza na kushuhudia Injili nchini Romania kadiri ya Mapokeo.

Hawa ni Mitume ambao walisadaka maisha yao, kiasi cha kuanzisha uekumene wa damu unaoendelea kurutubisha majadiliano ya kiekumene. Hata leo hii bado kuna Wakristo wanaoendelea kuteseka katika Ijumaa ya Madhulumu, wakionesha kimya kikuu cha Jumamosi kuu na hatimaye, kuzaliwa upya Jumapili ya Ufufuko wa Bwana! Baba Mtakatifu anayataka Makanisa kutembea kwa pamoja kwa nguvu ya kumbukumbu inayokita mizizi katika historia ya uinjilishaji kwenye karne ya kwanza. Ni katika mazingira haya, wakristo wakawa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia roho ya kinabii, wakajibidisha katika mchakato wa utamadunisho. Hiki ni kipindi ambacho Kanisa lilibahatika kuwa na mashuhuda wa imani na waungama dini; utakatifu wa maisha, ukawa ni chachu inayomwilishwa katika medani mbali mbali, kiasi cha kuutolea ushuhuda na kuvumilia nyanyaso na madhulumu! Hata leo hii, Wakristo wanahamasishwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, ili kwa njia ya neema, waweze tena kugundua ndani mwao kumbukumbu ya umoja, ili kuyaangazia mapito yao.

Jubilei ya Miaka 100

 

 

 

18 June 2020, 13:59