Tafuta

Vatican News
Kardinali Peter Turkson, Jumamosi, tarehe 13 Juni 2020 ametembelea kambi ya watu wasiokuwa na makazi maalum kama kielelezo cha huruma, upendo na mshikamano wa Mama Kanisa kwa watu wote! Kardinali Peter Turkson, Jumamosi, tarehe 13 Juni 2020 ametembelea kambi ya watu wasiokuwa na makazi maalum kama kielelezo cha huruma, upendo na mshikamano wa Mama Kanisa kwa watu wote!  (Vatican Media)

Ushuhuda wa mshikamano wa huruma na mapendo kwa maskini!

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kushirikiana na Duka la Dawa la Vatican pamoja na Tume ya Vatican Dhidi ya COVID-19 iliyoundwa hivi karibuni mjini Vatican, wametoa dawa na vifaa tiba kwenye kambi ya watu wasiokuwa na makazi maalum. Kardinali Turkson amepata pia fursa ya kutembelea na kuzungumza na watu wanaoishi kwenye kambi hii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, Jumamosi jioni tarehe 13 Juni 2020 ametembelea eneo la watu wasiokuwa na makazi maalum, “Tor Bella Monaca” lililoko mjini Roma. Kardinali Turkson amepata nafasi ya “kuchonga” na Kikundi cha watu wa kujitolea kijulikanacho kama “21 Luglio”, chini ya uongozi wa Carlo Stasolla. Hiki ni kikundi kinachotoa msaada wa chakula kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi mjini Roma, watoto ambao wanatishiwa kushambuliwa na utapiamlo wa kutisha na hasa wakati huu wa janga kubwa la maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kushirikiana na Duka la Dawa la Vatican pamoja na Tume ya Vatican Dhidi ya COVID-19 iliyoundwa hivi karibuni mjini Vatican, wametoa dawa na vifaa tiba kwenye kambi ya watu wasiokuwa na makazi maalum. Kardinali Turkson amepata pia fursa ya kutembelea na kuzungumza na watu wanaoishi kwenye kambi hii. Imekuwa ni fursa pia ya kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu hawa ambao wanakabiliwa na matatizo na changamoto kubwa za maisha hasa katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anapenda kuwahakikisha watu wote kwamba, hakuna hata mmoja wao ambaye amesahaulika katika huruma na upendo wa Mama Kanisa kwa hali na mali.

Hiki ni kipindi kigumu sana katika historia ya mwanadamu, kwani kimegusa na kutikisa sekta ya afya na miundombinu yake, uchumi na sera zake, lakini athari kubwa zaidi ni katika masuala ya kijamii. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson amekumbushia kwamba, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu yanapaswa pia kuzingatia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana! Katika ziara hii ya kikazi, Kardinali Turkson ameambatana na viongozi mbali mbali wa Jimbo kuu la Roma, Caritas Romana pamoja na viongozi wa vikundi vya kujitolea!

Kard. Turkson: Mshikamano na Maskini

 

15 June 2020, 13:01