Vatican News
Dr. Andrea Tornielli katika Tahariri yake anafafanua kuhusu dhamana na utume wa Roho Mtakatifu katika maisha ya Kanisa mintarafu Nyaraka za Papa Francisko alizozitoa hivi karibuni. Dr. Andrea Tornielli katika Tahariri yake anafafanua kuhusu dhamana na utume wa Roho Mtakatifu katika maisha ya Kanisa mintarafu Nyaraka za Papa Francisko alizozitoa hivi karibuni.  (Vatican Media) Tahariri

TAHARIRI: Roho Mtakatifu Katika Maisha na Utume wa Kanisa!

Bila nguvu ya Roho Mtakatifu, Kanisa haliwezi kufua dafu! Ni Kristo Yesu anayelituma Kanisa kutoka ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Kumbe, kazi ya kwanza ya Kanisa ni utume wa kutangaza Injili kwa watu wa Mataifa. Mitume wa Yesu waliokuwa wamejifungia ndani kwa woga wa Wayahudi walishindwa kupanga na kuibua mbinu mkakati wa maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Pentekoste inahitimisha kipindi cha Pasaka ya Kristo Yesu, kwa kumminina Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu. Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii.Hii ni siku ambayo Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hii ni Siku kuu ya waamini walei wanaohimizwa kutoka kifua mbele, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa karama na matunda ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko, ameadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Jumapili tarehe 31 Mei 2020, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu: Karama za Roho Mtakatifu; Historia ya Pentekoste; Umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo; Roho Mtakatifu ndiye siri ya umoja na sadaka ya maisha kwa ajili ya jirani!

Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho: 12:24 anaelezea kuhusu Karama za Roho Mtakatifu kwamba, kuna tofauti za karama, huduma na kutenda kazi, bali Roho ni yeye yule. Hapa kuna umoja na utofauti, kielelezo kwamba, Roho Mtakatifu ndiye anayeunganisha mambo kwa pamoja. Na kwa njia hii, Kanisa liliweza kuzaliwa. Kuna tofauti kubwa kati ya watu, lakini wote wanaunganishwa chini ya kifungo cha Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa mwaka 2020 anakazia: Umuhimu wa kuwashirikisha watu wa Mungu furaha ya Injili, kama mashuhuda wa zawadi ya imani. Wawe ni watu wenye mvuto kutokana na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mihimili ya uinjilishaji iwe ni kielelezo cha shukrani na sadaka inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. Wasaidie kurahisisha mambo na wala wasiyagumishe hata kidogo, daima wakijitahidi kuwa karibu na maisha ya waamini wanaowainjilisha kadiri ya hali na mazingira yao pamoja na kuzingatia ufahamu wa watu wa Mungu “Sensus fidei”. Wajitahidi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu: “Mimi hapa, nitume mimi” kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya: 6:8. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuutafakari utume wa Kanisa mintarafu janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kristo Yesu, alikamilisha utume wake kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Kanisa linatumwa na Kristo Yesu na kuongozwa na Roho Mtakatifu. Amri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kila kiumbe ni utume wa kimisionari na ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Bila kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, Kanisa litabaki kuwa kama “Chama cha Maisha ya kiroho” kinachoshindwa kutoa nafasi kwa Kristo Yesu ili kuendelea kukutana na waja wake, katika hija ya maisha yao ya ndani. Baba Mtakatifu anaongeza kusema, bila Roho Mtakatifu, Kanisa litashindwa kusonga mbele. Maisha ni zawadi ya bure kabisa inayopaswa kuwashirikisha wengine katika miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Utume wa Kanisa ni jibu makini la wito wa Mungu. Huu ni wakati wa kusoma alama za nyakati ili kutambua Mwenyezi Mungu anataka kusema nini kupitia janga hili la Virusi vya Corona, COVID-19. Hii pia ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake anagusia mambo makuu yaliyozungumziwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maisha na utume wa Kanisa. Askofu mkuu Ignas wa Jimbo kuu la Laodicea, mwanataalimungu mahiri kutoka katika Kanisa la Kiorthodox, tarehe 5 Julai 1968 katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni alisema kwamba, bila ya Roho Mtakatifu, Mwenyezi Mungu yuko mbali sana na waja wake, Kristo Yesu, anabaki katika kumbukumbu ya mambo ya kale; Injili inageuka kuwa ni Maandiko yaliyokufa na Kanisa linakuwa ni kama Chama; viongozi wake wanageuka kuwa ni watawala. Utume wa Kanisa unageuka kuwa ni propaganda. Mwishowe, Ibada inaonekana kuwa kama mwongozo na kanuni maadili kwa watumwa! Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2020 imechukua maana ya pekee kabisa, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kurejea tena kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya kushiriki na waamini, mahujaji na watu wenye mapenzi mema, tafakari na sala wakati wa mchana.

Baba Mtakatifu anafahamu fika kwamba, hii ni sehemu ya utume wake wa kimisionari, unaomsukuma kuwashirikisha waamini zawadi ya Roho Mtakatifu aliyoipokea na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yake. Bila nguvu ya Roho Mtakatifu, Kanisa haliwezi kufua dafu! Ni Kristo Yesu anayelituma Kanisa kutoka ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Kumbe, kazi ya kwanza ya Kanisa ni utume wa kutangaza Injili kwa watu wa Mataifa. Mitume wa Yesu waliokuwa wamejifungia ndani kwa woga wa Wayahudi anasema Baba Mtakatifu, walishindwa kupanga na kuibua mbinu mkakati wa maisha na utume wa Kanisa. Nyaraka mbali mbali zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa kwa siku za hivi karibuni ni rejea muhimu sana. Kristo Yesu anaendelea kukutana na waja wake katika uhalisia wa maisha yao na wala si wakati wa makongamano, semina za majiundo endelevu au hata katika Hekalu. Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS, ni chombo cha huduma ya Injili ya upendo kinachotumiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia!

Tahariri
01 June 2020, 13:37