Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Mauricio Agostinho Camuto kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Caxito, nchini Angola. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Mauricio Agostinho Camuto kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Caxito, nchini Angola. 

Mh. Padre Mauricio A. Camuto, Askofu mpya Caxito, Angola!

Askofu mteule Maurício Agostinho CAMUTO alizaliwa tarehe 26 Desemba 1963 huko Colungo, Jimbo Katoliki la Ndalatando. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 5 Septemba 1987 akaweka nadhiri zake za kwanza kwenye Shirika la Roho Mtakatifu, C.S.Sp. Tarehe 28 Julai 1991 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Ni mtaalamu wa sayansi ya mawasiliano jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa sana Padre Maurício Agostinho CAMUTO, wa Shirika la Roho Mtakatifu, C.S.Sp., kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Caxito, nchini Angola. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Maurício Agostinho CAMUTO alikuwa ni Mkurugenzi mkuu wa Radio Ecclesia inayomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Angola. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Maurício Agostinho CAMUTO alizaliwa tarehe 26 Desemba 1963 huko Colungo, Jimbo Katoliki la Ndalatando. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 5 Septemba 1987 akaweka nadhiri zake za kwanza kwenye Shirika la Roho Mtakatifu, C.S.Sp. Tarehe 28 Julai 1991 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Tangu wakati wakati huo hadi mwaka 1995 alijipatia uzoefu na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji, Jimbo Katoliki la Cabinda, Angola. Kati ya Mwaka 1995 hadi mwaka 1999 aliteuliwa kuwa Gambera wa nyumba ya Malezi ya kwanza ya Shirika iliyoko Jimboni Malanje. Kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Gambera wa wanafunzi wa Shirika Jimboni Huambo na Benguela. Kati ya Mwaka 2000 hadi mwaka 2003 alitumwa mjini Roma ili kujiendeleza katika masomo ya sayansi ya mawasiliano ya jamii, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesian, kilichopo mjini Roma.

Kati ya Mwaka 2003 hadi mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki Angola Sao Tome na Principe, CEAST. Tangu mwaka 2006 hadi mwaka 2010 akateuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa Radio Ecclesia, Angola. Kati ya Mwaka 2010 hadi mwaka 2016 kwa awamu mbili, alichaguliwa kuwa Padre Mkuu wa Kanda, Shirika la Roho Mtakatifu, C.S.Sp. Baada ya kumaliza awamu yake ya uongozi, akateuliwa tena kuwa ni Mkurugenzi mkuu wa Radio Ecclesia, nchini Angola!

Papa: Uteuzi Angola
15 June 2020, 12:45