Tafuta

Wiki ya LAUDATO SI’:Kujenga dunia kwa pamoja ili iwe bora!

Imeandaliwa Wiki ya Maombi kuanzia tarehe 16-24 Mei 2020,ikiongozwa na kaulimbiu “Wiki ya Laudato Si:kujenga pamoja dunia ili iwe bora.Ni mpango ulioandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma ya Maendeleo Fungamani ya Watu na kwa ushirikiano na mashirika mbalimbali katoliki duniani.Ni katika muktadha wa kuenzi Wosia wa Kitume wa Papa Francisko unapotimiza miaka 5 tangu kutangazwa kwa lengo la kutunza sayari nyumba yetu ya pamoja.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Wiki ya Laudato Si' ni sehemu ya kampeni ya kimataifa katika fursa ya mwaka wa 5 tangu kutangazwa kwa Wosia wa Kitume  wa Papa kuhusu utunzaji wa Sayari ambayo ni nyumba yetu ya Pamoja. Mada ya wiki hiyo imeunganishwa. Kwa njia hiyo kuanzia tarehe 16 hadi 24 Mei 2020 wakatoliki wote wanaalikwa kushiriki sehemu ya semina ya mafunzo ya moja kwa moja kupitia mtandaoni, mitandao inoyoingiliana na ya kushirikiana. Jumapili tarehe 24 Mei saa sita mchana, masaa ya Ulaya kutakuwa na sala ya pamoja ya ulimwengu wote.

Hata hivyo katika fursa hii, imeandaliwa hata ujumbe wa Papa kwa njia ya video. Katika ujumbe wa  Papa Francisko anawatia moyo waamini wote kushiriki na kufikiria wakati ujao wa nyumba yetu ya pamoja. “Je! Tunataka kuacha ulimwengu gani kwa wale watakaokuja baada yetu, kwa watoto ambao wanakua?  Kuanzia na  swali hili, Papa Francisko anarudia kutoa wito wake “ Ni dharura ya  haraka katika kujibu mgogoro wa kiekolojia, kilio cha dunia na kilio cha maskini ambacho hakiwezi kusubiri tena.  Acha tutunze kazi ya uumbaji, zawadi ya Muumba wetu Mungu mwema.  Tusherekee pamoja  wiki ya Laudato Si. Mungu awabariki na msisahau kusali kwa ajili yangu”

Kwa mujibu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo ya Fungamani ya Binadamu anabainisha kuwa Wosia kwa namna ya pekee ni chachu katika muktadha wa sasa wa janga la virusi vya corona au Covid-19 na ambavyo vimeenea kila pembe ya Dunia. Laudato si inatoa maono ya kuweza kuujenga kwa upya ulimwengu,uweze kuwa wa haki na endelevu. Aidha wanasema kuwa Wiki ya Laudato ni sehemu ya mpango ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo fungamani ya watu kwa kushirikiana pamoja na mashirika mengine katoliki ulimwenguni. Na zaidi ya watu 2000 wamejikita kuwania ushiriki huu wa Wiki ya Laudato Si’.  Kadhalika hata shughuli nyingine zimeandaliwa kufanyika kila sehemu mahalia kuanzia bara la Asia hadi Amerika ya Kusini.

16 May 2020, 10:25