Vatican News
Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki Duniani, kinawaalika wanachama wake, kukesha na kusali ili kumwomba Roho Mtakatifu awape nguvu ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo. Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki Duniani, kinawaalika wanachama wake, kukesha na kusali ili kumwomba Roho Mtakatifu awape nguvu ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo.  (AFP or licensors)

Wakarismatiki Wakatoliki: Mkesha wa Pentekoste Kwa Mwaka 2020

Wakarismatiki Wakatoliki, wanapaswa kutumia fursa hii kujiandaa kwa kusali na kutafakari Neno la Mungu linalomwishwa katika huduma ya upendo. Hiki ni kipindi cha Roho Mtakatifu, mwenye nguvu zaidi kuliko COVID-19. Kwa wale wanaomwamini na kumpenda Mwenyezi Mungu, wataweza kuuona wema wa Mungu hata katika matatizo na changamoto za Corona, COVID-19. Hadi raha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kunako mwaka 2019 lilianzisha kitengo maalum kijulikanacho kama “CHARIS” kinachosimamia na kuratibu shughuli za Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia. Kitengo hiki kilianza utekelezaji wa huduma yake wakati wa Sherehe ya Pentekoste, tarehe 9 Juni 2019. Katika mukatadha huu, Chama cha Udugu wa Kikatoliki, (The Catholic Frarenity) na Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki Kimataifa, (ICCRS) vikakoma kutoa huduma. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu unakuwa ni mwanzo mpya wa Chama Cha Wakarismatiki Wakatoliki, kielelezo cha neema na zawadi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwaliko kwa Wakarismatiki kuwa ni mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaoteseka. Wawe ni alama ya umoja na mshikamano wa Kanisa, wakiendelea kupyaisha maisha yao kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa; mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

CHARIS kinapaswa kuwa ni chombo cha huduma kwa watu wa Mungu. Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa ndiye pia Mshauri mkuu wa maisha ya kiroho ya Wakarismatiki katika ngazi ya kimataifa. Kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa mwaka huu, mkesha wa Sherehe ya Pentekoste unafanyika kwa njia ya mtandao. Padre Cantalamessa anawaalika Wakarismatiki Wakatoliki, kutumia fursa hii kujiandaa kwa kusali na kutafakari Neno la Mungu. Hiki ni kipindi cha Roho Mtakatifu Paji la Baba wa Milele, mwenye nguvu zaidi kuliko Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni muda wa kusali na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani na kwamba, Mwenyezi ni chemchemi ya wema na utakatifu wa maisha. Ni ukweli usiofumbiwa macho kwamba, Corona, COVID-19 imeutikisa ulimwengu, imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, lakini kwa wale wanaomwamini na kumpenda Mwenyezi Mungu, wataweza kuuona wema wa Mungu hata katika matatizo na changamoto za Corona, COVID-19.

Katika hali na mazingira haya, Baba Mtakatifu anawakumbusha walimwengu kwamba, hiki ni kipindi cha kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa kuondokana na uchoyo, ubinafsi na utaifa usiokuwa na tija wala mashiko! Padre Cantalamessa anakazia zaidi kwa kusema, hiki ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na sala pamoja na kuhakikisha kwamba, waamini wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Waamini watumie muda huu kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya toba na upatanisho; ili kushiriki kwa ibada na uchaji, maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Waamini waikimbie dhambi na nafasi zake; wajivike fadhila na utu wema; daima wakiendelea kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Muujiza wa Roho Mtakatifu kwa waamini si majibu ya sala na maombi yao. Ni muujiza unaofumbatwa katika sala na shukrani, hasa pale mwamini anapoguswa na kutikiswa kutoka katika undani wa maisha yake. Virusi vya Corona, COVID-19 “vimewapapasa na kuwatikisa waamini”. Sherehe ya Pentekoste, iwe ni mwanzo mpya kwa waamini kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo yao kwa kumkimbilia Roho Mtakatifu, Paji la Baba na Mfariji!  

Katika asili yake, neno “CHARIS” maana yake ni “neema au zawadi maalum kutoka kwa Roho Mtakatifu”. Kitengo cha CHARIS kilizinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hii pia ilikuwa ni siku ya kuzindua rasmi Katiba inayoratibu shughuli za kitengo hiki kama dira na mwongozo wa kusimamia na kukuza imani ya Kanisa Katoliki. Zote hizi ni kazi za Roho Mtakatifu zinazoendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa wakati huu! Kitengo hiki kimeanzishwa kwa maamuzi ya Baba Mtakatifu Francisko ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika huduma inayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya waamini milioni 120 wa Kanisa Katoliki ambao ni wanachama wa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki wanaoendelea kupyaisha dhamana na utume wao unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na kwa kuimarishwa na Roho Mtakatifu, zawadi ya Baba wa milele. Utume huu unamwilishwa katika vikundi vya sala; Jumuiya za Wakarismatiki pamoja na shule za uinjilishaji na hivyo kuunda mtandao wa mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa.

Kimsingi kitengo hiki, hakitakuwa na mamlaka juu ya Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, bali wataendelea kutekeleza dhamana na shughuli zao kama kawaida, chini ya usimamizi wa Maaskofu mahalia. Kila tawi linaweza kupata huduma na msaada wa kiufundi utakaokuwa unatolewa na CHARIS sehemu mbali mbali za dunia. Chama hiki kimeenea katika ngazi mbali mbali, kuanzia Parokiani, Kijimbo, Kitaifa na Kimataifa! Kumekuwepo na “ukakasi” kwa baadhi ya Maaskofu kuwakubali na kuwapokea wanachama hawa na kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa mahalia! Lakini, Kanisa linakumbusha kwamba, zote hizi ni zawadi za Roho Mtakatifu zinazopaswa kuratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu! Wakristo kwa kupakwa Krisma Takatifu wanaingizwa katika maisha ya Kristo Yesu ambaye amepakwa mafuta kuwa: Kuhani, Nabii na Mfalme. Chama hiki ni chachu ya majadiliano ya kiekumene na umoja miongoni mwa Wakristo. Wanachama wake wanajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa njia ya maisha na utume wao, wanashiriki kikamilifu katika utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ajili ya Kanisa zima! Itakumbukwa kwamba, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, lilimteua Jean-Luc Moens kuwa Mratibu wa kwanza wa CHARIS. Huyu ni Baba wa familia, yenye watoto 7 ambaye kwa muda wa zaidi ya miaka 45 amejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma na utume kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki nchini Ubelgiji. Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa ndiye Mshauri mkuu wa maisha ya kiroho ya Wakarismatiki duniani. Padre Cantalamessa aliteuliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuwahudumia wanachama hawa!

CHARIS: Kesha Pentekoste 2020
28 May 2020, 13:45