Tanzia: Padre Adolfo Nicolas aliyekuwa mkuu mstaafu wa Shirika la Wayesuit, amefariki dunia tarehe 20 Mei 2020 huko Tokyo, nchini Japan. Tanzia: Padre Adolfo Nicolas aliyekuwa mkuu mstaafu wa Shirika la Wayesuit, amefariki dunia tarehe 20 Mei 2020 huko Tokyo, nchini Japan. 

Tanzia: Padre Adolfo Nicolas, SJ. Amefariki dunia, 20 Mei 2020

Padre Adolfo Nicolás Pachón alizaliwa tarehe 29 Aprili 1936 huko Hispania. Tarehe 17 Machi 1967 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kuanzia mwaka 1968 hadi mwaka 1971 alijiendeleza zaidi kwa masomo kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma na kujipatia shahada ya Uzamivu. Amekuwa Mkuu wa Shirika la Wayesuit kuanzia mwaka 2008 hadi Mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mheshimiwa Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika la Wayesuit anasikitika kutangaza kifo cha Mheshimiwa Padre Adolfo Nicolás Pachón kilichotokea tarehe 20 Mei 2020 huko Tokyo nchini Japan baada ya kuugua kwa muda mrefu Padre Adolfo Nicolás Pachón alizaliwa tarehe 29 Aprili 1936 huko Villamuriel de Cerrato, nchini Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Machi 1967 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kuanzia mwaka 1968 hadi mwaka 1971 alijiendeleza zaidi kwa masomo kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma na kujipatia shahada ya Uzamivu. Kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1978 akateuliwa kuwa Jaalimu wa Taalimungu Chuo Kikuu cha Sophia nchini Japan. Kati ya Mwaka 1978 hadi mwaka 1984 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Shughuli za Kichungaji Jimbo kuu la Manila, Nchini Ufilippini.

Kati ya Mwaka 1993 hadi mwaka 1999 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Kanda ya Shirika la Wayesuit nchini Japan. Na mwaka 2004 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Kanda za Shirika la Wayesuit huko Asia ya Mashariki pamoja na Oceania. Amekuwa mkuu wa Shirika la Wayesuit tangu tarehe 19 Januari 2008 hadi tarehe 3 Oktoba 2016 alipong’atuka kutoka madarakani. Padre Adolfo Nicolás Pachón Katika maisha yake, alibahatika kuwa ni mtu mwenye hekima na neema; aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu, Kanisa na Shirika lake. Alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedito XVI, akajitahidi kuendeleza uhusiano huu hata na Baba Mtakatifu Francisko. Ni kiongozi aliyejitahidi kuishi kikamilifu karama ya Shirika lake. Alikuwa ni mcheshi sana, jasiri na mnyenyekevu katika maisha na utume wake

Mheshimiwa Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika la Wayesuit, Jumamosi tarehe 23 Mei 2020: Majira ya Saa 4:30 za Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye “Chiesa di Gesù”, Kanisa lililoko hapa mjini Roma. Kwa ushuhuda zaidi unaweza kufuatilia habari hii kwa kutumia anuani ifuatayo:

https://www.youtube.com/watch?v=vXJN6MUHtYo

Tanzia

 

 

21 May 2020, 13:41