Siku ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II!

Papa Yohane Paulo II alizaliwa tarehe 18 Mei 1920 na mauti yakamfikia kunako tarehe 2 Aprili 2005.Jina lake la kuzaliwa lilikuwa ni Karol Józef Wojtyła.Alikuwa ni Papa wa 264 kuanzia tarehe 16 Oktoba 1978.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Dominika tarehe 17 Mei maadhimisho ya misa yamefanyika huko Wadowice, Poland, mji alikozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II ambapo Askofu Mkuu Marek Jędraszewski ameadhimisha misa saa 4.30 majira ya Ulaya katika Kanisa Kuu la Kuwakilishwa kwa Bikira Maria Hekaluni. Saa saba walikuwa katika Nyumba ya Familia ya Papa Yohane Paulo II  ambapo kulifanyika tamasha la nyimbo kwa kuongozwa na mada “nimezaliwa huko Wadowice - Karol Wojtyła”.  Matukio yote mawili yametangazwa moja kwa moja na vituo vya matangazo ya Televisheni mahalia (TVP1).  Jioni Kardinali Stanisław Dziwisz ametoa ujumbe wake kwa wanapoland wote kupitia Televisheni ya Taifa  TVP1.

Tarehe 18 Mei 2020  katika kilele cha  Jubilei ya Mtakatifu Yohane Paulo II, saa 11 jioni masaa ya Ulaya, katika madhabahu ya Yohane Paulo II  huko  Krakow misa imeadhimishwa na ambayo imetangazwa moja kwa moja na Televisheni TVP3 ambayo imeongozwa na Askofu Mkuu Marek Jędraszewski. Katika kilele cha Jubilei ya  Papa tarehe 18 Mei saa 11 jioni katika Madhabahu ya Yohane Paulo II huko Krakow, wameadhimisha ya Misa ambayo imetangazwa moja kwa moja na televisheni ya taifa TVP3, kwa kungozwa na Askofu  Mkuu Marek Jędraszewski.

Papa Yohane Paulo II alizalikwa tarehe 18 Mei 1920  na mauti yakamfikia kunako tarehe 2 Aprili 2005. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa ni Karol Józef Wojtyła Alikuwa  ni Papa wa 264 kuanzia tarehe 16 Oktoba 1978. Hadi kufikia kifo chake alidumu katika huduma hiyo ya kipindi kirefu kuliko mapapa wengine wote, isipokuwa  kwa Mtume Petro na Papa Pius IX. Alimfuata Papa Yohane Paulo I akiwa Papa wa kwanza asiye Mwitalia tangu miaka 455 iliyokuwa imepita wakati huo na  akiwa papa wa kwanza kutoka Polandi katika historia ya Kanisa.

  

Atakumbukwa sana, hasa kwa sababu tangu mwanzo wa upapa wake alipambana na Ukomunisti uliotesa nchi yake asili na nyinginezo, akachangia kwa kiasi kikubwa kikomo chake na kusambaratika kwa Urusi. Vilevile alilaumu ubepari wa nchi za magharibi na kudai haki katika jamii zote, akitetea hasa uhai wa binadamu na uhuru wa dini. Hata hivyo Papa Francisko wakati wa misa yake asubuhi katika Kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II amebainisha juu ya sifa  nyingi lakini zaidi sifa tatu za Mtakatifu huyu, kwanza kusali, pili ukaribu na tatu upendo wa haki.”(Mahubiri Papa 18,Mei 2020 katika kaburi la Mtakatifu Petro)

Upande wa dini, aliboresha uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya Ukristo pamoja na ule na dini mbalimbali, kuanzia Uyahudi, Ubudha, Uislamu na mengine. Alifanya ziara zake  za kitume 104 kati nchi 129 ulimwenguni kote, mbali na 146 nchini Italia na 317 katika parokia za Roma, ambazo zilikusanya mara nyingi umati mkubwa. Kwa wasta alisafiri kuliko jumla ya mapapa wote waliomtangulia, akiwa mmojawapo kati ya viongozi wa dunia waliosafiri zaidi.

Papa Wojtyła alitangaza wenye heri 1,340 na watakatifu 483, ili kuwapa Wakristo wa leo vielelezo mbalimbali kwa maisha yao ili walenge utakatifu walioitiwa na Mungu. Idadi hiyo ni kubwa kuliko ile ya waliotangazwa na jumla ya Mapapa wote waliomtangulia walau katika karne tano za mwisho. Alikuwa anaongea lugha mbalimbali, zikiwemo za Kipolandi, Kiitalia, Kifaransa, Kijerumani, Kiingereza, Kihispania, Kireno, Kiukraina, Kirusi, Kiserbokroatia, Kiesperanto, Kilatini na Kigiriki cha kale. Yohane Paulo II alitangazwa na mwandamizi wake Papa Benedikto XVI kuwa mwenye heri tarehe 1 Mei 2011na Papa Fransisko akamtangaza mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014. Sikukuu yake huadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Oktoba, kulingana na siku ya kuanza rasmi huduma yake ya Kipapa kwa Misa iliyofanyika katika uwanja mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican.

18 May 2020, 20:40