Tafuta

Vatican News
Dr. Paolo Ruffini, ametuma ujumbe wa video kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Juma la Mawasiliano ya Jamii Nchini Italia kwa kukazia ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya Upashanaji Habari 2020. Dr. Paolo Ruffini, ametuma ujumbe wa video kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Juma la Mawasiliano ya Jamii Nchini Italia kwa kukazia ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya Upashanaji Habari 2020.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Kilele cha Juma la Mawasiliano ya Jamii Nchini Italia

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika ujumbe wake kama sehemu ya maadhimisho ya Juma la Mawasiliano ya Jamii Nchini Italia anakazia kwa namna ya pekee kabisa: Umuhimu wa kutamba hadithi mpya; uzuri wa mawasiliano na Mwenyezi Mungu; chemchemi ya matumaini, ili kupandikiza mbegu ya ujenzi wa jumuiya inayosimikwa katika ukarimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 24 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, unaongozwa na kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Kutoka:10:2. Maisha yanakuwa ni historia. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anapembua kwa kina na mapana kuhusu mwingiliano wa hadithi na kwamba, si kila hadithi ni hadithi njema. Kuna hadithi ya hadithi; hadithi iliyopyaishwa na hatimaye kuna hadithi inayoendelea kumpyaisha mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao ukweli wa historia ya Habari Njema ya Wokovu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 24 Mei 2020 limeadhimisha Juma la Mawasiliano ya Jamii Nchini Italia, hii ikiwa ni awamu yake ya kumi na tano. Lakini kutokana na itifaki ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, maadhimisho haya yamefanyika kwa njia ya mtandao, kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee na Masista wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo, lililoanzishwa kunako mwaka 1915 na Mwenyeheri James Alberione, huko Alba nchini Italia na linatekeleza utume wake katika nchi 52 duniani kote! Katika hali na mazingira ya sasa ambamo watu wengi wamejikatia tamaa na kugubikwa kwa taharuki wanasema Masista wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo kuna haja kwa binadamu kuendelea kutamba ujumbe unaofumbata: ukweli, uzuri, matumaini na faraja. Huu ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni.

Katika kipindi hiki ambacho watu wengi wamewekwa karantini, mitandao ya kijamii, imekuwa ni msaada mkubwa katika medani mbali mbali za jamii. Ikumbukwe kwamba, dini zinapaswa kuwa ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa watu waliokata tamaa. Ni wajibu wa wadau wa tasnia ya habari kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na kuondokana na habari za kughushi zinazosababisha madhara makubwa katika maisha ya watu! Ni katika muktadha huu, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya maadhimisho ya Juma la Mawasiliano ya Jamii Nchini Italia anakazia kwa namna ya pekee kabisa: Umuhimu wa kutamba hadithi mpya; uzuri wa mawasiliano na Mwenyezi Mungu; chemchemi ya matumaini, ili kupandikiza mbegu ya ujenzi wa jumuiya inayosimikwa katika ukarimu. Ni wakati wa kujizatiti katika mawasiliano dhidi ya Virusi vya ubinafsi, kwa kuendeleza hadithi zinazowakirimia watu furaha ya kweli!

Mchango wa Dr. Paolo Ruffini katika maadhimisho haya unaongozwa na Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu, anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kushirikishana hadithi, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza, lakini kumsikiliza Mwenyezi Mungu Muumbaji na Mtamba hadithi, ambaye kwa neno lake, aliumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Katika kipindi hiki cha janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kuna haja ya kufanya tafakari ya kina kuhusu Injili ya uhai, na kuendelea kushukuru mchango mkubwa ambao umetolewa na maendeleo ya sayansi na teknolojia hasa katika ulimwengu wa kidigitali, “ulioyofyekelea mbali” umbali uliokuwepo kati ya watu ndani ya jamii, lakini bado watu wamebaki na wasiwasi mkubwa kwamba, yale maingiliano na mafungamano ya kijamii yanaweza kubaki katika ulimwengu wa kidigitali.

Katika hali na mazingira ya sasa, watu wengi wamejikuta wakiwa na kishawishi cha kutaka kupata majibu ya mkato kutokana na matatizo na changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu. Kwa watu kuwekwa karantini, jamii imeweza kujifunza umuhimu wa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii yanayobubujika kutoka katika hadithi za watu wenyewe. Wadau wa tasnia ya habari wanapaswa kuwa: ni wahudumu na vyombo vya ukweli, wema na uzuri, kwa kusimama kidete kutetea kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu. Mawasiliano ya jamii iwe ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu, ili kuganga na kuponya madonda yaliyosababishwa na habari potofu. Wadau wa tasnia ya mawasiliano wanapaswa kuendeleza kipaji cha ubunifu ili kuwaondoa watu jangwani na hivyo kuanzisha mchakato wa mawasiliano mubashara unaojenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii.

Huu ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati, ili kuibua na kuendeleza maisha mapya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni muda wa kujenga na kudumisha ujasiri unaofumbwatwa katika misingi ya ukarimu, udugu wa kibinadamu na mshikamano. Mtandao wa mawasiliano ya jamii hauna budi kuendelezwa katika ulimwengu wa utandawazi pamoja na kuzingatia mahitaji ya jamii mahalia. Huu ni mfumo wa kidigitali na unaozingatia ukweli, ili kuwaunganisha watu katika medani mbali mbali za maisha na kamwe si kuwatenganisha na kuwasambaratisha. Maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii hayana budi kuwa na mwelekeo wenye mafao mapana zaidi kwa watu. Huu ni wakati wa kujikita katika mawasiliano dhidi ya virusi vya ubinafsi, ili kudumisha umoja, mshikamano, ukweli na kuendeleza mchakato wa watu kukutana. Mahusiano na mafungamano yamwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kujenga uchumi shirikishi, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu.

Watu wadumishe ushirikiano unaosimikwa katika tunu msingi za maisha ya kiutu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Wadau wa tasnia ya mawasiliano wanapaswa kujisadaka kwa kutoa muda wao, ujuzi, weledi, rasilimali fedha na sala zao. Ni wajibu na dhamana ya Kanisa kutoka na kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Mama Kanisa hana budi kuhakikisha kwamba, anatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mungu. Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie watu kugawana mambo ya kidunia, kufahamu yanayoendelea kujiri sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi, viwe ni chemchemi ya upendo. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya maadhimisho ya Juma la Mwasiliano ya Jamii nchini Italia, kwa kuwasihi wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuwa chemchemi ya furaha, kwa kusimulia hadithi, kwa kushirikiana na kushikamana, ili watu wote kwa pamoja, waweze kufurahi.

Dr. Ruffini
25 May 2020, 14:20