Kamati kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inawaalika waamini wa dini na madhehebu mbali mbali: kusali, kufunga na kufanya matendo ya huruma. Kamati kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inawaalika waamini wa dini na madhehebu mbali mbali: kusali, kufunga na kufanya matendo ya huruma. 

Mwaliko wa Sala Kuombea Udugu wa Kibinadamu 14 Mei 2020

Tume inatoa wito kwa waamini wa dini mbali mbali, ulimwenguni kote kumwelekea Mwenyezi Mungu kwa: kufunga na kusali, kwa unyenyekevu mkuu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kila mtu mahali pake alipo, kadiri ya dini, imani au dhehebu lake, kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuliondoa janga na kuwanusuru kwa athari zote zinazotokana na ugonjwa huu wa Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo.

Ni katika muktadha huu, Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, inawaalika waamini wa dini mbali mbali ulimwenguni hapo tarehe 14 Mei 2020, kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwalinda binadamu. Wanakimbilia huruma na upendo wake, ili kushinda Janga la Virusi vya Corona, COVID-19, ili hatimaye, kurejesha tena amani na utulivu, afya, ustawi na maendeleo. Baada ya Janga hili, ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa njia ya mshikamano na mafungano ya udugu wa kibinadamu kuliko ilivyokuwa hapo awali! Wapendwa waamini wa dini mbali mbali, Tume inasema, leo hii ulimwengu umekumbwa na janga kubwa linalotishia maisha ya mamilioni ya watu kwa sababu ya kuenea kwa haraka maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Tume inapenda kusisitiza kuhusu umuhimu wa tiba na tafiti za kisayansi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, lakini haiwezi kushindwa kumwelekea Mwenyezi Mungu, Muumbaji  katika janga hili kubwa. Hivyo basi, Tume inatoa wito kwa waamini wa dini mbali mbali, ulimwenguni kote kumwelekea Mwenyezi Mungu kwa: kufunga na kusali, kwa unyenyekevu mkuu na hatimaye kumwilisha sala hii katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kila mtu mahali pake alipo, kadiri ya dini, imani au dhehebu lake, kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuliondoa janga na kuwanusuru kwa athari zote zinazotokana na ugonjwa huu. Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu, awajalie wanasayansi na watafiti ili waweze kugundua tiba ya ugonjwa huu, ili kuuokoa ulimwengu kutokana na madhara yake makubwa: kiafya, kiuchumi na kiutu kutokana na kuenea kwa janga hili la hatari.

Kwa kutambua umuhimu na uzito wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, kumeundwa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati hii na kati ya wajumbe wake ni pamoja na: Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii.

Sala y udugu wa Kibinadamu
04 May 2020, 13:59