Tafuta

Vatican News
Dr. Matteo Bruni msemaji mkuu wa Vatican amebainisha kwamba, hadi kufikia tarehe 6 Mei 2020, kumekuwepo na wafanyakazi 12 walioambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19 mjini Vatican. Dr. Matteo Bruni msemaji mkuu wa Vatican amebainisha kwamba, hadi kufikia tarehe 6 Mei 2020, kumekuwepo na wafanyakazi 12 walioambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19 mjini Vatican.  (AFP or licensors)

Maambukizi ya Virusi vya Corona Vatican Sasa ni Wafanyakazi 12

Hadi kufikia tarehe 6 Mei 2020, idadi ya wafanyakazi wa Vatican walioambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19 imefikia watu kumi na wawili. Mfanyakazi mmoja, aliyekuwa anatekeleza dhamana na wajibu wake, mbali na ofisi za Vatican tangu mwanzoni mwa Mwezi Machi, 2020 alianza kupata dalili zote za Virusi vya Corona na hivyo kujitenga kwa ridhaa binafsi “Self isolation”. Jikinge kwanza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, amesema kwamba, hadi kufikia tarehe 6 Mei 2020, idadi ya wafanyakazi wa Vatican walioambukizwa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 imefikia watu kumi na wawili. Mfanyakazi mmoja, aliyekuwa anatekeleza dhamana na wajibu wake, mbali na ofisi za Vatican tangu mwanzoni mwa Mwezi Machi, 2020 alianza kupata dalili zote za Virusi vya Corona na hivyo kujitenga kwa ridhaa binafsi “Self isolation”. Kabla ya kurejea tena ofisini kwake ili kuendelea na kazi, akapimwa tena na kugunduliwa kwamba, bado alikuwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Kurugenzi ya Afya na Usafi mjini Vatican imeagiza kwamba mfanyakazi huyu aendelea kupata tiba na uangalizi wa wataalam wa afya akiwa nyumbani kwake.

Janga la Corona, COVID-19 ni kipindi cha kuimarisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayosimikwa katika ubunifu, kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali muda, vitu na watu inatumika vyema kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Watu wajenge umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kamwe asiwepo mtu anayepoteza maisha katika hali ya upweke na kiza kinene katika maisha yake. Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, “umekwisha kupiga hodi mjini Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, anakaza kusema, huu ni muda muafaka wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano kwa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Kutenga muda wa sala kwa ajili ya kuwaombea wagonjwa, wahudumu na wale wote waliotangulia mbele ya haki, wakiwa na imani na matumaini ya ufufuo na uzima wa milele. Kanisa linawahamasisha waamini kujiandaa vyema ili kuweza kupokea Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa kwa nyakati kama hizi. Waamini watumie fursa hii kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao! Tafakari hii iwe ni shirikishi ili familia nzima iweze kujisikia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani.Ugonjwa huu umeibua changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika huduma ya Sakramenti. Kuna wagonjwa wengi wanaoitupa mkono dunia bila ya huduma ya Kanisa. Hii ni changamoto kwa waamini walei wanaotekeleza dhamana na utume wao hospitalini na kwenye nyumba za wazee kuwa ni alama ya imani, matumaini na mapendo, kwa wagonjwa na wale wote walio kufani!

Huu ni ugonjwa ambao umezishambulia nchi tajiri na maskini. Mama Kanisa ana wasi wasi mkubwa ikiwa kama janga hili linavyoonekana katika nchi kama Italia, Hispania na Marekani, madhara yake pia yatatua na kutikisa nchi maskini duniani. Kanisa litaendelea kuonesha upendo na mshikamano na Makanisa yote mahalia, ili baada ya dhoruba hii kali, watu waweze kuwa na mwelekeo mpya na mpana zaidi katika maisha. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, umefika wakati kwa viongozi mbali mbali kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kumezwa na utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto! Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waangalie njaga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuzingatia hekima inayowawajibisha kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ili kukuza: uhuru, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi!

Maambukizi Vatican

 

07 May 2020, 13:08