Askofu mkuu mteule Ante Jozic ateuliwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Belarus. Askofu mkuu mteule Ante Jozic ateuliwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Belarus. 

Askofu mkuu mteule Ante Jozic: Balozi Belarus!

Askofu mkuu mteule Ante Jozić alizaliwa tarehe 16 Januari 1967 huko Trilj, nchini Croatia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 28 Juni 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alianza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican tarehe1 Julai 1999. Alikuwa awekwe wakfu kuwa Askofu tarehe 21 machi 2020 lakini kutoka na ugonjwa wa Corona, sherehe zimesogezwa mbele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu mteule Ante Jozić, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Belarus. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mteule Ante Jozić alikuwa Balozi wa Vatican huko Pwani ya Pembe. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Ante Jozić alizaliwa tarehe 16 Januari 1967 huko Trilj, nchini Croatia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 28 Juni 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Askofu mkuu mteule Ante Jozić, alijiendeleza zaidi katika masomo ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa na kujipatia Shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Tarehe 1 Julai 1999 akaanza utume wa kidiplomasia mjini Vatican. Katika kipindi chote hiki, amewahi kufanya utume wake kwenye Ofisi za Ubalozi wa Vatican huko: India, Urussi na Ufilippini. Kwa miaka 10 akiwa Hong Kong, alipewa kazi maalum ya kustadi uhusiano kati ya China na Vatican kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya pande hizi mbili.

Tarehe 2 Februari 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe. Tarehe 7 Aprili 2019 akiwa nchini Croatia akapata ajali mbaya ya gari na kunalazwa hospitalini huko nchini Croatia. Baada ya matibabu ya kina, tarehe 20 Juni 2019 akaruhusiwa kurejea nyumbani kwao. Tarehe 22 Januari 2020 akakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Alikuwa anatarajiwa kuwekwa wakfu kama Askofu mkuu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican hapo tarehe 21 Machi 2020, lakini kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 Ibada ya kumweka wakfu ikasogezwa mbele zaidi. Tarehe 21 Mei 2020 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Belarus. Hii ni nchi ambayo ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican hapo tarehe 11 Novemba 1992.

Papa: Uteuzi
22 May 2020, 14:40