Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amesema, Sekretarieti kuu ya Vatican imekwisha pembua mpango mkakati na utekelezaji wake kuanzia tarehe 4 Mei 2020 Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amesema, Sekretarieti kuu ya Vatican imekwisha pembua mpango mkakati na utekelezaji wake kuanzia tarehe 4 Mei 2020 

COVID-19: Vatican yatangaza mpango mkakati wa 4 Mei 2020

Kardinali Parolin amesema, shughuli mbali mbali zinazotekelezwa mjini Vatican kama sehemu ya maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, zitaanza kurejea taratibu bila haraka. Itifaki ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 inapaswa kuzingatiwa, ili kuhakikisha kwamba, Vatican inaendelea kutoa huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa Kanisa la Kiulimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano, tarehe 22 Aprili 2020 ameongoza mkutano wa dharura uliowahusisha wakuu wote wa Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na taasisi zake. Lengo la mkutano huu, lilikuwa ni kufanya upembuzi wa kina kuhusu hali ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na kujiwekea mpango mkakati wa utekelezaji wa awamu ya pili ya janga hili la COVID-19, inayotarajiwa kuzinduliwa hapo tarehe 4 Mei 2020. Katika mkutano huu, imetiliwa mkazo kwamba, Vatican itaendeleza sera na mikakati iliyokwisha kufikiwa hadi wakati huu kama sehemu ya mapambano dhidi ya janga hili.

Shughuli mbali mbali zinazotekelezwa mjini Vatican kama sehemu ya maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, zitaanza kurejea taratibu bila haraka. Itifaki ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 inapaswa kuzingatiwa, ili kuhakikisha kwamba, Vatican inaendelea kutoa huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa Kanisa la Kiulimwengu! Wakati huo huo, Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican amewaambia waandishi wa habari kwamba, hadi kufikia Jumatatu tarehe 20 Aprili 2020, maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, yamefikia watu tisa, walioambukizwa na Virusi hivi vya hatari mjini Vatican. Hawa ni wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican. Mgonjwa wa tisa aliyebainika, amelazwa hospitalini na hatua za dharura zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kupulizia dawa katika ofisi aliyokuwa anatumia. Watu waliobahatika kukutana naye siku alipowasili kazini nao wanaendelea kuchunguzwa afya zao.

Kardinali Parolin
23 April 2020, 13:48