Tafuta

Vatican News
Mama Tazama Mwanao: Tangu wakati huo, Bikira Maria akawa ni Mama wa waamini wote. Chini ya Msalaba waamini wote wakapata maisha mapya! Mama Tazama Mwanao: Tangu wakati huo, Bikira Maria akawa ni Mama wa waamini wote. Chini ya Msalaba waamini wote wakapata maisha mapya! 

Mama Tazama Mwanao: Bikira Maria Mama wa Waamini Wote!

Bikira Maria ni chemchemi ya matumaini ya watu wa Mungu yanayotiririka kutoka katika sakafu ya Moyo wake Mtakatifu. Bikira Maria Mama wa Mungu ni heshima inayotolewa na Kanisa kwa kutambua kwamba, Bikira Maria ndiye mzazi wa Kristo Yesu, Mtu kweli na Mungu kweli. Ni Mama wa waamini wote katika maisha na kweli za kiimani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Mama Maria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu ambayo imekuwa ikiongoza tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 zinazotolewa kwa Baba Mtakatifu Francisko, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Romana”, wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni: “Na penye Msalaba wake Yesu alikuwa amesimama mamaye” Rej. Yoh. 19:25). Bikira Maria katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu. Huu ni mwendelezo wa tafakari iliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa wakati wa Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2019-2020. Padre Cantalamessa, katika tafakari yake, Ijumaa, tarehe 3 Aprili 2020, amechambua maneno ya Kristo Yesu alipokuwa ametundikwa Msalabani: “Mama tazama mwanao.” Yoh. 19:26-27. Tangu wakati huo, Bikira Maria akawa ni Mama wa waamini wote! Chini ya Msalaba, waamini wote wakapata maisha mapya. Bikira Maria anayo nafasi ya pekee katika Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama Mama wa Mungu na Kanisa. Kristo Yesu kabla ya kukata roho, alimkabidhi Bikira Maria kwa mwanafunzi aliyempenda na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake.

Bikira Maria ni chemchemi ya matumaini ya watu wa Mungu yanayotiririka kutoka katika sakafu ya Moyo wake Mtakatifu. Bikira Maria Mama wa Mungu ni heshima inayotolewa na Kanisa kwa kutambua kwamba, Bikira Maria ndiye mzazi wa Kristo Yesu, Mtu kweli na Mungu kweli. Ni Mama wa waamini wote katika maisha na kweli za kiimani kama sehemu ya mchakato unaopania kuimarisha na kudumisha imani hii kwa Kristo Yesu. Bikira Maria ni Mama wa Jumuiya ya waamini wa Agano Jipya; watu wote wanaoishi. Mwinjili Yohane anapenda kumwonesha Kristo Yesu akiwa Msalabani, kama kielelezo cha juu kabisa cha ufunuo wa utukufu na ukamilifu wa Maandiko Matakatifu. Yohane, mwanafunzi yule aliyempenda alibahatika kuwa chini ya Msalaba, kama mwakilishi wa wanafunzi wote wa Yesu. Kristo Yesu akamkabidhi Mama yake pamoja na kuwakabidhi wafuasi wake wote chini ya ulinzi na tunza ya Mama yake mpendwa. Bikira Maria anakuwa ni Mama wa wote kwa njia ya neema. Waamini wote wanafanyika kuwa ni watoto wa Bikira Maria kwa “Maji na Roho Mtakatifu”, ili kushiriki imani na mateso yaliyousonga Moyo Safi wa Bikira Maria.

Bikira Maria na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: Padre Raniero Cantalamessa anaendelea kufafanua kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wana mpatia Bikira Maria nafasi ya pekee katika historia na kazi ya ukombozi. Ni Mama aliyeteuliwa kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Umwilisho. “Kwa kumtunga mimba na kumzaa Kristo, kwa kumlisha, kumtolea kwa Baba Hekaluni, kwa kuteswa pamoja na Mwanae aliyekufa Msalabani, alishiriki kwa namna iliyo ya pekee kabisa kazi ya Mwokozi kwa utii wake na imani, matumaini na mapendo yake yenye kuwaka, ili uzima wa kimungu utengenezwe upya katika roho za wanadamu. Kwa sababu hiyo amekuwa mama kwa ajili yetu katika mpango wa neema” LG, n. 61. Bikira Maria ni mwombezi kwa ajili ya wokovu, ni Bikira na Mama, mfano mtimilifu wa Kanisa. Mama wa Mungu ni kielelezo “typus” cha Kanisa kwa habari ya imani, mapendo, umoja kamili na Kristo. Katika Fumbo la Kanisa, Maria anaitwa: Bikira na Mama kutokana na imani na utii wake kwa mpango wa Mungu. Bikira Maria ni sehemu ya Kanisa na Kanisa linapaswa kuiga utakatifu wa Bikira Maria. Mtakatifu Paulo VI alitamka wazi kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa anapaswa kuheshimiwa na Kanisa zima.

Padre Raniero Cantalamessa anaendelea kufafanua kwamba, “Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake”. Yoh. 19:27. Hii sehemu ya Maandiko Matakatifu inayoonesha matukio muhimu katika maisha ya Bikira Maria, kama kioo cha Kanisa, mwaliko ni kumkubali na kumwingiza katika uhalisia wa maisha ya waamini. Mwinjili Yohane, katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu anatoa ushuhuda wa jinsi ambavyo Bikira Maria aliweza kuhitimisha maisha yake, akiwa chini ya ulinzi wa Yohane. Huyu ndiye Mama wa Mungu na Kanisa. Waamini wanahamasishwa kumkaribisha Bikira Maria ili kuweza kupata neema ya kuamua na kutenda kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Waamini wajiaminishe kwake kama udongo mikononi mwa mfinyanzi wakitambua pia nafasi na dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Roho Mtakatifu awasaidie waamini kuweza kumshirikisha Bikira Maria katika undani wa maisha yao, kwa sababu huyu ni Mama wa Fumbo la Umwilisho. Bikira Maria ni njia rahisi ya kumwendea Kristo Yesu “Ad Jesus per Mariam”. Roho Mtakatifu anawaongoza waamini kwenda kwa Yesu kupitia kwa Bikira Maria sanjari na kukubali wosia wake. Bikira Maria awe ni mwandani, mshauri na mwalimu wa waamini.

Padre Raniero Cantalamessa anasema kwamba, Bikira Maria alikuwa na nafasi ya pekee sana katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu, karibu sana na Msalaba wa Yesu, kielelezo na chemchemi ya imani na matumaini; ambayo kamwe hayataweza kutoweka katika sakafu ya nyoyo za watu wanaokumbuka uweza wa Mungu milele. Waamini wamkimbilie Bikira Maria nyakati za giza na uvuli wa mauti, ili waweze kujiaminisha chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu ambaye amemfanya Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mataifa na katika uzao wake Mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu ya utii kwa sauti ya Mungu. Kwa hakika, Mataifa yote watamwita mbarikia! Utii wa Bikira umekuwa ni sababu ya ukombozi wa walimwengu. Ni chombo cha baraka kutokana na neema aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Bikira Maria amebarikiwa kuliko wanawake wote. Kwa hakika imani yake haitatoka mioyoni mwa watu wanaokumbuka ukuu na uweza wa Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu kwamba, matumaini na ujasiri wa Bikira Maria hautaweza kutoweka katika moyo na kumbu kumbu ya Mama Kanisa.

Kwa ufupi, Kanisa kwa kutumia muhtasari wa Fumbo la Pasaka kama linavyofafanuliwa na Mtakatifu Paulo linaweza kusema kwamba, Bikira Maria ingawa alikuwa ni Mama wa Mungu, lakini hakuona kwamba, hiki kilikuwa ni kitu cha kung’angania sana. Bali alikubali kuacha vyote, akachukua hali ya mtumishi, na kuishi kama wanawake wengine wote. Akajinyenyekesha na kutoweka machoni pa watu; akawa mtii mpaka kifo cha Mwanae, tena kifo cha Msalaba. Kwa sababu hiyo, Mungu alimwinua juu kabisa, akampa jina ambalo ni kuu kuliko majina yote; ili kwa jina la Bikira Maria, kila goti lipigwe, mbinguni na duniani na kuzimu; na kila ulimi ukiri kwamba Bikira Maria ni Mama wa Mungu kwa utukufu wa Mungu Baba!

Bikira Maria
03 April 2020, 13:14