Tafuta

Mama kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 15 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Paulo II Mama kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 15 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Paulo II 

Kumbukumbu ya Miaka 15 Tangu Afariki Dunia Papa Yohane Paulo II

Leo hii, watu wengi wamekosa imani na matumaini ya maisha na uzima wa milele! Matokeo yake wanaelemewa sana na simanzi na majonzi makubwa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika utume wake; katika magumu na mahangaiko yake ya ndani, daima alikita maisha yake katika matumaini na akawataka waamini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II alifariki dunia tarehe 2 Aprili 2005, yaani miaka 15 iliyopita na kuacha ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika mateso na mahangaiko ya binadamu. Hata leo hii, katika hofu, wasi wasi na taharuki ya kuenea kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, bado anaendelea kuwahamasisha watu wa Mungu kuwa na imani, matumaini, upendo na mshikamano wa dhati, ili baada ya dhoruba hii kali kupita, watu waweze kusimama tena na kusonga mbele! Takwimu za maambukizi na vifo vinavyotokana na Virusi vya Corona inaonekana kuongezeka maradufu, kiasi cha kuwakatisha watu tamaa ya maisha. Watu wametikiswa kutoka katika undani wa maisha yao kiasi cha kubakiza utupu na mahangaiko makubwa.

Taa ya imani kwa watu wengi imezimika kama kibatari! Lakini, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mwamini hodari na shupavu katika maisha na utume wake. Taa ya imani ilikuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake, hata pale ilipoonekana kana kwamba, anatembea katika uvuli wa mauti! Aliugua kwa muda mrefu, lakini bado aliendelea kuwa ni mtu mwenye amani, furaha na utulivu wa ndani. Ni mwamini ambaye alikuwa safarini kuelekea kwenye maisha na uzima wa milele. Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na fumbo la kifo katika maisha yao. Ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Huu ni ushuhuda wa maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, unaotolewa na Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 15 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipofariki dunia. Hata baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hapo tarehe 13 Mei 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliendelea na maisha na utume wake katika hali ya utulivu na amani ya ndani. Leo hii, watu wengi wamekosa imani na matumaini ya maisha na uzima wa milele! Matokeo yake wanaelemewa sana na simanzi na majonzi makubwa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake; katika magumu na mahangaiko yake ya ndani, daima alikita maisha yake katika matumaini na akawataka waamini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni shuhuda wa imani katika mateso na mahangaiko ya mwanadamu, si haba kwamba, aliweza kushuhudia yale yaliyokuwa yanamgusa kutoka katika undani wa maisha yake katika Waraka wake wa Kitume, “Mateso yanayookoa” “Salvific dolores”. Madaktari ni watu ambao kwa taaluma yao wamebahatika kuwasindikiza wagonjwa wao kutoka katika dunia hii na kuingia katika usingizi wa amani na maisha ya uzima wa milele, mahali ambapo wanakumbana na Fumbo la Kifo na uwepo wa Mungu anayedhihirisha nguvu yake na mwanadamu anayeonesha udhaifu wake mbele ya Fumbo la Kifo. Mtakatifu Yohane Paulo II ni kiongozi ambaye Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo vilikuwa daima mbele ya macho na akili yake. Mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanapaswa kupata jibu makini kutoka katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu anayemfahamu fika mwanadamu katika mahangaiko yake.

Kardinali Angelo Comastri anasema, maadhimisho ya Fumbo la Pasaka kwa Mwaka 2020 yamegubikwa na taharuki ya maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa mwaka huu, hakutakuwa na maadhimisho ya hadhara na badala yake, waamini wanahamasishwa kufuatilia maadhimisho haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya jamii. Lakini, Mtakatifu Yohane Paulo II kabla ya kifo chake, kutokana na kuelemewa na ugonjwa alilazimika kufuatilia maadhimisho haya akiwa chumbani mwake, hali ameshikilia Msalaba, akiwa na matumaini ya maisha na uzima wa milele baada ya kuhitimisha hija ya maisha yake hapa duniani. Katika kipindi hiki cha taharuki na hofu kubwa ya maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu katika sala, ibada, sadaka na majitoleo mbali mbali.

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kristo Yesu, kabla ya kukata roho, alipenda kuwakabidhi wanafunzi wake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria! Ndiyo maana Mama huyu alikuwa n anafasi ya pekee sana katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Katika maisha kila mtu amekabidhiwa Msalaba wake, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Msalaba huu unakuwa ni chemchemi ya upendo na mwanga angavu wa maisha! Mtakatifu Yohane Paulo II ni kiongozi aliyeitupa mkono dunia akiwa na siri kubwa moyoni mwake! Hii ni siri ya mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanayokoa na kukomboa, changamoto kubwa hapa ni kuwapekelea wengine ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Yohane Paulo II alikuwa ni mgonjwa aliyejitahidi kushirikiana vyema na madaktari wake, kwa kuwaelezea kwa kina mapana yale yaliyokuwa yanamsumbua mwilini mwake!

Mtakatifu Yohane Paulo II
01 April 2020, 14:47