Tafuta

Vatican News
Janga la Virusi vya Corona iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha: Injili ya upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kudumisha ujirani mwema, ustawi na mafao ya wengi! Janga la Virusi vya Corona iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha: Injili ya upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kudumisha ujirani mwema, ustawi na mafao ya wengi! 

Kardinali Tagle: Janga la Corona: Upendo na Mshikamano wa kidugu

Kardinali Tagle anasema, dharura ya Virusi vya Corona hii, iwawezeshe watu kujenga ari na moyo wa upendo na mshikamano, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha jirani na maskini wanaowazunguka bila ya msaada. Ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja, udugu wa kibinadamu na ujirani mwema, ili kuleta mlipuko wa matumaini kwa wale waliovunjika moyo na kukata tamaa ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Watu wengi kwa sasa wamewekwa chini ya karantini kama sehemu ya mchakato wa kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huu wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Katika muktadha huu, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kufanya toba na wongofu wa ndani; kwa kubadili pia mitazamo na vipaumbele vya maisha yao, tayari kumkaribisha Mwenyezi Mungu katika hali ya unyenyekevu, upole na kiasi na wala hakuna sababu ya “kujimwambafai” kusikokuwa na mvuto wala mashiko! Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambaye pia ni Rais wa Caritas Internationalis anasema, maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 yanazidi kutishia usalama, maisha na mafungamano ya watu sehemu mbali mbali za dunia.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linawahamasisha Wakristo kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa madaraja yanayo wakutanisha watu katika huduma ya upendo, ili kujenga ari na moyo wa utamaduni wa watu kushirikiana katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika huduma. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, katika tafakari yake kuhusu kipeo cha maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 anapenda kufafanua maneno mawili yanayopata chimbuko lake katika lugha ya Kilatini: Emergency”: “Emergere”, yaani “Dharura” inayopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Mwanadamu amekuwa akikabiliwa na matetemeko ya ardhi, dhoruba kali, mafuriko, ukame pamoja na milipuko ya magonjwa kama ilivyo kwa wakati huu.

Kipeo cha maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kinatafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza kuwa ni “Pandemic” kutokana na maneno mawili ya lugha ya Kigiriki “Pan” maana yake “Wote” na “Demos” yaani “Watu”. Kumbe, hiki ni kipeo kinachowaathiri watu wote na kinahitaji umoja, ushirikiano na mshikamano kama silaha madhubuti ya kupambana na janga hili la kimataifa linaloendelea kupukutisha maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni hulka ya binadamu katika dharura na majanga kama haya, watu kutaka kujifungia katika ubinafsi, kwa ajili yao binafsi na wale wanaowazunguka. Dharura hii, iwawezeshe watu kujenga ari na moyo wa upendo na mshikamano, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha jirani na maskini wanaowazunguka bila ya msaada. Ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja, udugu wa kibinadamu na ujirani mwema, ili kuleta mlipuko wa matumaini kwa wale waliokata tamaa.

Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 ni wakati pia wa kuhakikisha kwamba, watu “wanaambukizana fadhila ya huruma na upendo”. Historia ya ulimwengu huu itawahukumu walimwengu, ikiwa kama wamekuwa mstari wa mbele kujenga na kudumisha Injili ya huruma na mapendo! Mama Kanisa kwa namna ya pekee, anapenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa hakika wamekuwa ni chemchemi ya uponyaji na matumaini kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Ili kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona, kuna masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wote.

Kati ya masharti haya ni kuosha mikono kwa sabuni. Watu wanahimizwa kujikinga ili waweze kuwakinga wengine, kwani ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, inazuilika. Vaa barakoa “Mask” iwapo tu unamhudumia mhisiwa au mgonjwa wa Corona, au iwapo wewe mwenyewe ni mgonjwa wa Corona uliyethibika! Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anasema, tendo la kunawa mikono liwakumbushe waamini kile kilichoandikwa kwenye Maandiko Matakatifu. “Basi, Pilato alipoona ya kuwa hafai lolote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, “Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe”. Mt. 27:24.

Watu waoneshe upendo na mshikamano; kwa kuwajali na kuwahudumia maskini na wale ambao wataendelea kutumbukizwa katika umaskini kutokana na ukosefu wa fursa za ajira; wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanateseka sana kwani wao si kipaumbele cha jamii kwa wakati huu; watu wasiokuwa na makazi ya kudumu wanateseka zaidi, kwani kila mtu anatakiwa kubaki nyumbani kwake, lakini hawa hawana mahali pa kulaza vichwa vyao! Mshikamano wa upendo uwaendee wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma, ili kujenga na kudumisha imani, matumaini na mapendo kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, watu wote washikamane ili kukabiliana uso kwa uso na kipeo cha maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa njia hii, binadamu wote wataweza kuibuka kidedea dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Caritas: Upendo

LinkYoutube For Media Article:

https://www.youtube.com/watch?v=tCW-2wTt_K0&feature=youtu.be

09 April 2020, 14:06