Tafuta

Vatican News
Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2020 imegubikwa na simanzi, majonzi na hali ya watu kukata tamaa! Caritas Internationalis inasema, Pasaka ni wakati wa kujenga umoja na mshikamano! Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2020 imegubikwa na simanzi, majonzi na hali ya watu kukata tamaa! Caritas Internationalis inasema, Pasaka ni wakati wa kujenga umoja na mshikamano!  (ANSA)

Caritas Internationalis: Ujumbe wa Pasaka kwa Mwaka 2020: Umoja!

Serikali nyingi zinalenga kuokoa uchumi wa nchi zao unaoendelea kudidimia na kuzama badala ya maisha ya watu wao, ambayo kimsingi ndiyo rasilimali tete inayoweza kuinua uchumi unaodhohofu! Katika shida, mahangaiko na mateso ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia, jambo muhimu ni kifungo cha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo katika Kristo Yesu! Huu ni ukweli ambao Wakristo wa Kanisa la mwanzo waliusadiki na kuunafsisha katika uhalia wa maisha yao kama kiini cha ukweli. Imani hii imeendelezwa kwa njia ya Mapokeo ya Kanisa na kuithibitisha kwa njia ya Maandiko Matakatifu katika Agano Jipya. Imani hii wakaitangaza na kuishuhudia kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka sanjari na Fumbo la Msalaba. Mama Kanisa anakiri na kufundisha kwamba, “Akasulubiwa pia kwa ajili yetu sisi; akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akafa, akazikwa. Akafufuka siku ya tatu ilivyoandikwa. Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni, mwanadamu amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, "Caritas Internationalis" katika ujumbe wake katika kipindi hiki cha Sherehe ya Pasaka kwa Mwaka 2020 anasema, maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa mwaka huu yamejengeka katika simanzi, majonzi pamoja na hali ya kukata tamaa katika maisha kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Kristo Ijumaa kuu! Huu ni ukweli unaotokana na athari za maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Changamoto kubwa kwa wakati huu, ni kwa Jumuiya ya Kimataifa kuungana na kushikamana kwa dhati, ili ikiwa imeungana iweze kuvuka dhoruba hii kali inayopukutisha maisha ya watu kama “Nzige”.

Kutokana na madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, inaonekana kana kwamba, wafuasi wa Kristo bado wako na Kristo Yesu katika ile Bustani ya Gethsemane. Watu wengi wanateseka, kiasi cha kudhani kwamba, maendeleo ya sayansi ya tiba ya mwanadamu yamegonga mwamba na wala hakuna tena matumaini! Serikali nyingi zinaona giza nene mbele yake kwa kushindwa kuokoa maisha ya wananchi wake wanaoendelea kuambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19; kuugua, kufa na wale wenye bahati kama mtende kupona! Mbele ya changamoto hii, inaonekana kana kwamba, hakuna suluhu kwa wakati huu. Janga hili linaendelea pia kuwatesa wakimbizi na wahamiaji; wazee na yatima, wagonjwa na maskini sanjari na watu wasiokuwa na fursa za ajira.

Caritas Internationalis inawahimiza viongozi wa Serikali sehemu mbali mbali za dunia, kuhakikisha kwamba, watu wote bila ubaguzi wanapata ulinzi wa kutosha na tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasibu. Upendeleo wa pekee unapaswa kutolewa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali zao. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kujizatiti zaidi katika mchakato wa ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa Kimataifa, ili kuweza kuwajibika kwa pamoja. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anapenda kuwachangamotisha watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kutafakari na kunafsisha maana ya umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa! Ni wakati wa kuamua na kutenda katika ukweli, uwazi na ujasiri. Lengo ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa kwenye familia kubwa ya binadamu.

Kwa bahati mbaya sana, sera na mikakati ya shughuli za kiuchumi imepewa kipaumbele cha kwanza badala ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, haki msingi za binadamu, utu na heshima yake! Serikali nyingi zinalenga kuokoa uchumi wa nchi zao unaoendelea kudidimia na kuzama badala ya maisha ya watu wao, ambayo kimsingi ndiyo rasilimali tete inayoweza kuinua uchumi unaodhohofu! Katika shida, mahangaiko na mateso ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia, kuna jambo moja ambalo linaendelea kutia matumaini yaani kifungo cha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa watu wa Mataifa. Ni mshikamano ambao kwa miaka kadhaa haukupewa umuhimu wa kutosha. Kutokana na athari za Janga la Corona, COVID-19, watu wamegundua kwamba, kila mtu ni muhimu kwa jirani zake na kwamba, hakuna mtu anayeweza “kujimwambafai” anajiweza na kujitegemea mwenyewe!

Watu wanategemeana na kukamilishana katika safari ya maisha yao hapa duniani! Uchoyo, ubinafsi na hali ya baadhi ya Mataifa kujiamini kupita kiasi ni sawa na lile “Jiwe la Kaburi la Yesu” lililowaogofya wanawake waliokwenda kaburini, asubuhi na mapema ile Siku ya Kwanza ya Juma! Jiwe hili kwa sasa limeondolewa na Mwanga wa Kristo Mfufuka unaanza kuonekana! Wachunguzi wa mambo wanasema, kutokana na watu kujifungia ndani, ubora wa hali ya hewa umeendelea kuongezeka maradufu na kwa hakika hili ni kosa lenye heri! Makundi hasimu yaliyokuwa yanapigana; nchi zilizokuwa zinaendesha vita, kwa sasa mambo yote yametulia, kila upande unaangalia na kutafakari Janga la Corona-COVID-19. Kadiri ya Maandiko Matakatifu, Kristo Yesu alifufuka Siku ya tatu! Kumbe, hata kifo hakina sauti ya mwisho, bado Injili ya matumaini inaweza kupeta na kukita mizizi yake katika akili na nyoyo za watu!

Mashirika mbali mbali ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas yanaendelea kuchakarika usiku na mchana ili kuwahudumia waathirika wa Janga la Corona, COVID-19 kwa hali na mali, sehemu mbali mbali za dunia. Caritas inapenda kutahadharisha, kukinga na kuwahudumia waathirika wa Janga la Corona, COVID-19. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, anapenda kuchukua fursa hii ya Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi na watu wa kujitolea wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Wote watambue kwamba, “Caritas Christi Urges Nos” yaani “Upendo wa Kristo Unawawajibisha”. 2 Kor. 5:14. Upendo wa Kristo ambao unaonekana kuwa ni kidogo sana kama mbegu ya haradali, lakini ndani yake ni chemchemi ya matumaini na mshikamano, mwaliko na changamoto ya kuyaambata na kuyakumbatia ya mbeleni kwa kujikita katika mfumo mpya wa maisha.

Janga la Corona, COVID-19 halichagui wala kubagua; halina mipaka ya kiimani, hali na uwezo wa mtu! Kipeo cha Janga hili kinaweza kupata ufumbuzi wake kwa njia ya umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa. Pasaka ya Mwaka 2020 inaonesha ukame wa maisha ya kiroho, kwa watu kushindwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka! Katika hali na giza nene, waamini wawe na ujasiri wa kuruhusu mwanga wa imani, matumaini na mapendo kutoka kwa Kristo Yesu, kuweza kupenyeza katika uhalisia wa maisha yao. Pasaka ya Bwana, iwe ni nguvu kwa watu wa Mungu kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Watu wakubali yale mambo wanayoweza kubadili; wawe na ujasiri wa kubadili mambo yaliyoko kwenye uwezo wao pamoja na busara ya kuweza kuona tofauti. Iwe ni fursa ya kutafuta na kufahamu maana ya ndani zaidi katika Janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni mwaliko wa kuambata imani na matumaini katika Fumbo la Pasaka ya Bwana!

Caritas: Pasaka 2020
24 April 2020, 14:00