Jarida la Civiltà Cattolica linalohaririwa na kuchapishwa na Wayesuit, mwaka 2020 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 170 tangu kuanzishwa kwake na sasa linachapishwa pia kwa lugha ya Kichina. Jarida la Civiltà Cattolica linalohaririwa na kuchapishwa na Wayesuit, mwaka 2020 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 170 tangu kuanzishwa kwake na sasa linachapishwa pia kwa lugha ya Kichina. 

Jubilei ya Miaka 170 ya Jarida la "Civiltà Cattolica: Toleo la Kichina

Jarida la “Civiltà Cattolica” limeipokea changamoto hii kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwa sasa linaanza kuchapishwa pia kwa Lugha ya Kichina na kusambazwa kwa njia ya mitandao ya kijamii. Lengo kuu ni kuendelea kuwa ni chombo cha Habari Njema ya Wokovu. Wayesuit wanaandika ukurasa mpya wa urafiki unaowakutanisha na utamaduni wa watu wa Mungu nchini China.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jarida la “Civiltà Cattolica” linalohaririwa na kuchapishwa na Shirika la Wayesuit, kwa Mwaka 2020 linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 170 tangu kuanzishwa kwake. Hii ilikuwa ni changamoto iliyotolewa na Mwenyeheri Papa Pio IX. Tangu wakati huo, Jarida hili limeendelea kuwa aminifu kwa Mafundisho ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, aliwashukuru Wayesuit kwa huduma hii makini wanayoendelea kuitoa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu katika ujumbe wake huo aliwataka Wayesuit kusoma alama za nyakati na kuendelea kujikita katika ustaarabu wa Kikatoliki unaofumbatwa katika dhana ya Msamaria mwema, yaani huduma makini kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni wakati wa kusoma alama za nyakati, kwa kujikita katika kipaji cha ubunifu, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi katika lugha wanayoifahamu. Jarida lijikite zaidi katika mchakato wa kupambana na chuki, ubinafsi na maamuzi mbele.

Wasi wasi na ugumu wa maisha iwe ni fursa ya kusoma alama za nyakati ili kutambua mpango wa Mungu kwa ajili ya mwanadamu! Jarida la “Civiltà Cattolica” limeipokea changamoto hii kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwa sasa linaanza kuchapishwa pia kwa Lugha ya Kichina na kusambazwa kwa njia ya mitandao ya kijamii. Lengo kuu ni kuendelea kuwa ni chombo cha Habari Njema ya Wokovu. Wayesuit wanaandika ukurasa mpya wa urafiki unaowakutanisha na utamaduni wa watu wa Mungu nchini China. Jarida la Civiltà Cattolica limekuwa ni sawa na mwandishi mwenye elimu ya Ufalme wa mbinguni, kwani wametoa katika hazina yao vitu vipya na vya kale. Hii ni sehemu ya ujumbe alioandika Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Padre Antonio Spadaro, S.J., Mkurugenzi mkuu wa Jarida la “Civiltà Cattolica” katika uzinduzi wa Jarida hilo linaloanza pia kuchapishwa kwa lugha ya Kichina.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wayesuit kujenga madaraja yanayowakutanisha watu; ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiutu! Kardinali Pietro Parolin, anapenda kuchukua fursa hii kutoka katika undani wa moyo wake, kuwapongeza na kuwashukuru Wayesuit kwa jitihada zao. Ni matumaini yake kwamba, Makala kwa lugha ya Kichina itakuwa ni fursa makini ya kutajirishana kitamaduni na kisayansi miongoni mwa watu wa Mungu wanaotafuta uzuri na ukweli. Ni matumaini yake kwamba, makala kwa lugha ya Kichina yataandaliwa na kuhaririwa kwa ari na moyo mkuu, ili yalete mvuto kwa wasomaji na kama hatima ya kazi hii ni kusaidia mchakato wa ujenzi wa ustaarabu ambao uko wazi kwa ajili ya majadiliano na amani ya kudumu kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia!

Anuani ya tovuti hii ni: https://www.gjwm.org. Tovuti hii imegawanyika katika sehemu kuu 4 ambazo ni: Habari (新闻), Ulimwengu (观世界), Tafakari ya Kikristo (基督教文化研究) na Utamaduni. (文化及评论).

Kardinali Parolin
21 April 2020, 07:22