Tafuta

Vatican News
Askofu Mstaafu Silas Silvius Njiru wa Jimbo Katoliki la Meru, Kenya amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 akiwa nchini Italia. Askofu Mstaafu Silas Silvius Njiru wa Jimbo Katoliki la Meru, Kenya amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 akiwa nchini Italia. 

Askofu Mstaafu Silas S. Njiru wa Jimbo la Meru, Kenya amefariki dunia kwa COVID-19.

Askofu Mstaafu Silas Silvius Njiru wa Jimbo Katoliki la Meru, Kenya alizaliwa tarehe 10 Oktoba 1928. Tarehe 17 Desemba 1955 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 2 Oktoba 1975, akateuliwa na Papa Paulo VI kuwa Askofu Msaidizi wa Meru na kuwekwa wakfu tarehe Mosi, Januari 1976. Na tarehe 9 Desemba akateuliwa kuwa Askofu wa Meru. Tarehe 18 Machi 2004 akang’atuka madarakani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taarifa iliyotolewa na Padre Pedro José da Silva Louro, IMC., Katibu mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, inaonesha kwamba, Askofu Mstaafu Silas Silvius Njiru wa Jimbo Katoliki la Meru, nchini Kenya, amefariki dunia tarehe 28 Aprili 2020, baada ya kulazwa kwenye Hospitali ya Rivoli, Torino, Italia kuanzia tarehe 25 Aprili 2020 kutokana na kushambuliwa na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baada ya kung’atuka kutoka madarakani, tarehe 18 Mei 2004, aliomba Shirika la Wamisionari wa Consolata kuishi kwenye nyumba ya wazee wa Shirika ya “Beato Giuseppe Allamano, huko Alpignano, Torino.

Hii ni kutokana na historia na urafiki mkubwa aliokuwa nao na Shirika la Wamisionari wa Consolata tangu ujana wake. Itakumbukwa kwamba, Askofu Mstaafu Silas Silvius Njiru wa Jimbo Katoliki la Meru, Kenya alizaliwa tarehe 10 Oktoba 1928 huko Kevote, Meru, nchini Kenya. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Desemba 1955 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 2 Oktoba 1975, akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Meru na kuwekwa wakfu tarehe Mosi, Januari 1976 na Kardinali Maurice Michael Otunga wa Jimbo kuu la Nairobi.  Tarehe 9 Desemba 1976 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Meru, Kenya. Tarehe 18 Machi 2004 akang’atuka kutoka madarakani. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, sasa aweze kumstahilisha mtumishi wake kuyaona mafumbo aliyokuwa anayaadhimisha, kuyatangaza na kuyashuhudia katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu!

 

 

29 April 2020, 12:37