Tafuta

Tahariri: Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Pasaka 2020: Uribi et Orbi: Imani kwa Kristo Mfufuka chemchemi ya matumaini, ustawi na mafao ya wengi. Tahariri: Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Pasaka 2020: Uribi et Orbi: Imani kwa Kristo Mfufuka chemchemi ya matumaini, ustawi na mafao ya wengi.  Tahariri

TAHARIRI: Ujumbe wa Pasaka: Urbi et Orbi! Imani kwa Kristo Mfufuka!

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake anagusia: Mahubiri ya Papa Francisko, Jumamosi Kuu, Kesha la Pasaka 2020 pamoja na Ujumbe wake kwa Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2020: Urbi et Orbi. Anawaalika watu wote wa Mungu kuwajibika barabara kwa kujisikia kwamba, wote kwa pamoja na wanaunda familia kubwa ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2020: Urbi et Orbi anasema, kwa hakika Kristo Yesu amefufuka kweli kweli! Huu ni ujumbe wa matumaini hata katika nyakati hizi ambazo mwanadamu anakabiliwa na changamoto kubwa ya janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19! Kristo Yesu ndiye yule aliyeteswa, akafa na sasa amefufuka kwa wafu. Katika mwili wake mtukufu anabeba Madonda Matakatifu, chemchemi ya matumaini yanayoganga, kuponya na kutakasa madonda ya mwanadamu. Huu ni muda wa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano unaokita mizizi yake katika matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka.

Kristo Yesu awe ni matumaini kwa maskini, watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu si muda wa kuendekeza kinzani na migawanyiko, bali kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema si wakati hata kidogo wa kuendelea kutengeneza, kulimbikiza na kutumia silaha na badala yake, rasilimali fedha hii, itumike kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu duniani! Dharura ya wakati huu kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 usiifanye Jumuiya ya Kimataifa ikasahau majanga mbali mbali yanayoendelea kuwakumba watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni wakati wa “kuambukizana” fadhila ya matumaini, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya ushindi wa upendo, dhidi ya mateso na kifo; ushindi ambao umegeuza ubaya kuwa wema kama kielelezo cha nguvu ya Mungu inayookoa.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake anagusia: Mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi Kuu, Kesha la Pasaka 2020 pamoja na Ujumbe wake kwa Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2020: Urbi et Orbi. Anawaalika watu wote wa Mungu kuwajibika barabara kwa kujisikia kwamba, wote kwa pamoja na wanaunda familia kubwa ya binadamu! “Tutto andrà bene” yaani “Yote yatakwenda vyema” ni kauli mbiu ambayo imekuwa ikitumika na wengi kama chemchemi ya matumaini na faraja katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Si rahisi sana kwa mtu aliyeguswa na kutikiswa na ugonjwa huu kupokea kauli mbiu hii kwa moyo mnyofu. Hawa ni wale watu ambao wamewapoteza ndugu na jamaa zao; watu ambao wameona familia zao “zikipukutika” kama majani makavu!

Si rahisi kwa wafanyakazi ambao hawajui hatma ya maisha yao baada ya fursa nyingi za ajira kuanza kutoweka taratibu na hivyo kugumisha maisha ya watu wengi, kiasi cha kuanza kutaabika kutafuta chakula kwa ajili ya familia zao. Watu wengi wanasema, yale yajayo yanatia shaka sana katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu! Baba Mtakatifu Francisko anasema Kesha la Pasaka iwe ni fursa ya kujitwalia haki ya matumaini mapya yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi kama zawadi kubwa, ambayo kamwe wasingeweza kujitwalia wenyewe! Matumaini kutoka kwa Kristo Yesu yanaweka ndani ya moyo wa mwamini uhakika kwamba, Mwenyezi Mungu atatenda yote vyema na kwamba, hata kaburini ataweza kuchipua maisha mapya! Kwa hakika si mambo yote yataendelea kubaki kama yalivyo, lakini ukweli ni kwamba, Kristo Yesu aliyetesa na kufa Msalabani ndiye aliyefufuka kwa wafu kama ilivyosimuliwa kwenye Mateso ya Kristo Yesu, Ijumaa Kuu. Hili ni jibu muafaka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuhusu mateso na kifo.

Upendo wa Mungu ni nguvu inayookoa! Ni nguvu inayoweza kubadili ubaya kuwa wema! Huu ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kujikita hata katika suluhu mpya na uwajibikaji wa pamoja kwa kutumia rasilimali za dunia hii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati muafaka wa kugawana mikate mitano na samaki wawili ili kulisha umati mkubwa wa wenye njaa. Huu si muda wa kuendekeza kinzani na migawanyiko, bali kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ni muda wa kuachana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji na vizuia mimba vinavyofyekelea mbali maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

Watu wa Mungu waoneshe wema, upendo na ukarimu kwa kuwakunjulia mikono watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali katika maisha; watu wanaokosa hata mahitaji msingi ya maisha. Ni katika muktadha huu, umoja na mshikamano uwe ni utambulisho wa watu wa Mungu Barani Ulaya, kwa kusaidiana kwa hali na mali. Hii ni changamoto changamani kwa Umoja wa Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake kwani watu wote ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu duniani. Kishawishi cha kutaka kurejea kwenye historia ya mambo yaliyopita ni hatari sana kwa mafungamano ya amani kijamii, ustawi na maendeleo kwa vizazi vijavyo!

Tahariri: Urbi et Orbi
13 April 2020, 13:23