Tafuta

Vatican News
Virusi vya Corona, COVID-19: Vatican yaguswa na kuchukua hatua ya kufunga Zahanati yake ambayo inasadikiwa kwamba, ilipokea mgonjwa wa homa ya Virusi vya Corona. Virusi vya Corona, COVID-19: Vatican yaguswa na kuchukua hatua ya kufunga Zahanati yake ambayo inasadikiwa kwamba, ilipokea mgonjwa wa homa ya Virusi vya Corona.  (ANSA)

Virusi vya Corona, COVID-19: Vatican yaguswa; yafunga Zahanati yake!

Ijumaa tarehe 6 Machi 2020, Vatican imelazimika kusitisha huduma zinazotolewa kwenye Zahanati ya Kurugenzi ya Afya na Usafi mjini Vatican ili kupulizia dawa kwenye Zahanati hii ambayo inasemekana kwamba, ilipokea mgonjwa aliyekuwa ameambukizwa Virusi vya homa ya Corona, COVID-19. Hata hivyo Kitengo cha dharura bado kinaendelea kutoa huduma hasa kwa maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amebainisha kwamba, Sekretarieti kuu ya Vatican inaendelea kufanya tafakari ya kina ili kuweza kuchukua maamuzi magumu kuhusu shughuli za Baba Mtakatifu Francisko na Vatican katika ujumla wake kwa siku za usoni, kama sehemu ya mbinu mkakati wa kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo kwa sasa vimekuwa ni tishio la usalama wa maisha ya watu wengi ndani na nje ya Italia. Ijumaa tarehe 6 Machi 2020, Vatican imelazimika kusitisha huduma zinazotolewa kwenye Zahanati ya Kurugenzi ya Afya na Usafi mjini Vatican ili kupulizia dawa kwenye Zahanati hii ambayo inasemekana kwamba, ilipokea mgonjwa aliyekuwa ameambukizwa Virusi vya homa ya Corona, COVID-19.

Hata hivyo Kitengo cha dharura bado kinaendelea kutoa huduma hasa kwa maskini na wale wasiokuwa na makazi maalum. Kurugenzi ya Afya na Usafi mjini Vatican imekwisha kutoa taarifa kwa Serikali ya Italia na kwamba, kwa wakati huu inaendelea kutekeleza Itifaki ya Usafi ili kuzuia kuenea kwa Virusi vya Corona. Dr. Matteo Bruni anasema, Vatican itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali ya Italia ili kutekeleza sera na mikakati iliyobainishwa na Serikali ya Italia kama sehemu ya mapambano ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimekwisha kusababisha maafa na madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Ugonjwa wa Virusi vya Corona huenezwa kwa njia ya maji maji yatokayo katika njia ya hewa, au mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya pamoja na kugusa maji maji yatokayo puani, au anapogusana na mtu mwingine mwenye maambukizi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona.

Wakati huo huo, Dr. Matteo Bruni amewaambia waandishi wa habari, Ijumaa tarehe 6 Machi 2020 kwamba, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya yake baada ya kushambuliwa na mafua makali; afya yake inaendelea kuimarika siku kwa siku. Baba Mtakatifu ameendelea kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican pamoja na kufuatilia mafungo ya kiroho yaliyokuwa yanatolewa na Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma. Kauli mbiu ya mafungo haya ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”.

Virusi vya Corona: Vatican
06 March 2020, 16:05