Tafuta

Vatican News
Kardinali Peter Turkson: Janga la Virusi vya Corona halitambui mipaka wala rangi ya mtu; muhimu kwa familia ya Mungu kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kardinali Peter Turkson: Janga la Virusi vya Corona halitambui mipaka wala rangi ya mtu; muhimu kwa familia ya Mungu kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. 

Virusi vya Corona, COVID-19: Janga lisiofahamu mipaka wala rangi ya mtu: Mshikamano muhimu!

Mlipuko wa ugonjwa huu, umeonesha udhaifu mkubwa wa binadamu pamoja na sera na mikakati yake ya ulinzi na usalama wa watu na mali zao. Ugonjwa huu umegusa kutikisa maisha ya watu wengi, uchumi wa kitaifa na kimataifa. Umeleta athari kubwa kwa wafanyabiashara; maeneo ya kazi na safari. Sekta ya utalii, michezo, elimu na hata maisha ya maisha ya kiroho, zote zimeguswa.

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha ukame wa maisha ya kiroho kutokana na kuenea kwa kasi kubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia, anawaalika Mapadre kuwa ni vyombo vya: imani, faraja na matumaini kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi hivi. Kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, anawaalika wawe mstari wa mbele kuwapatia Neno la Mungu pamoja na Sakramenti ya Ekariti Takatifu, ili Kristo Yesu aweze kuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini katika mahangaiko yao. Kwa upande wake, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anasema, Jumuiya ya Kimataifa imegubikwa na hofu, wasi wasi na mashaka makubwa kutokana na kuenea kwa Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vinaendelea kusababisha maafa na majanga makubwa kwa watu na mali zao. Mlipuko wa ugonjwa huu, umeonesha udhaifu mkubwa wa binadamu pamoja na sera na mikakati yake ya ulinzi na usalama wa watu na mali zao.

Ugonjwa huu umegusa kutikisa maisha ya watu wengi, uchumi wa kitaifa na kimataifa. Umeleta athari kubwa kwa wafanyabiashara; maeneo ya kazi na safari. Sekta ya utalii, michezo, elimu na hata maisha ya maisha ya kiroho, zote zimeguswa. Uhuru wa watu kutembea umedhibitiwa sana. Kardinali Peter Turkson anapenda kuchukua fursa hii, kuungana na Baba Mtakatifu Francisko, ili kuonesha uwepo wa karibu wa Mama Kanisa kwa watu wote wa Mungu wanaoteseka kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa namna ya pekee, mshikamano wa huruma na upendo, viwaendelee waathirika pamoja na familia zao; wafanyakazi wa sekta ya afya ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia waathirika wa Virusi vya Corona. Mama Kanisa anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kushikamana kwa njia ya sala, ili kuwakumbuka na kuwaombea watu wote walioathirika kutoka na ugonjwa huu, bila kuwasahau, wataalam na wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, Virusi vya Corona, COVID-19 vinadhibitiwa kikamilifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa afya ya umma.

Kwa namna ya pekee kabisa, Kardinali Turkson, anazialika taasisi za afya zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, wahudumu katika sekta ya afya pamoja na wadau wote, kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kutoa huduma makini kwa waathirika wote. Waendelee kuungana ili kutafuta tiba na chanjo ya ugonjwa huu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Shirika la Afya Duniani, WHO pamoja na viongozi wa Serikali katika nchi husika. Ni matumaini ya Kardinali Turkson kwamba, Serikali, Taasisi za Kitaifa na Kimataifa pamoja na watu binafsi wataendelea kuonesha mshikamano wa upendo kwa kuwasaidia waathirika kwa hali na mali. Kwa namna ya pekee, mshikamano huu uoneshwe kwa nchi zile ambazo bado zina mifumo dhaifu ya huduma ya afya kwa wananchi wake, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa umoja na upendo kati ya watu wa Jumuiya ya Kimataifa. Serikali, Taasisi na Sekta binafsi zishirikishane vifaa tiba na rasilimali watu ili kuwanusuru watu na janga hili. Familia ya binadamu inapaswa kujisikia kuwa inawajibika kikamilifu kwa kutumia karama na mapaji mbali mbali waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ugonjwa huu umeanza kutikisa taifa moja, lakini kwa sasa umesambaa sehemu mbali mbali za dunia na hivyo kuwa kweli ni tishio kwa maisha na usalama wa watu wengi duniani! Huu ndio wakati muafaka wa kumwilisha tunu msingi za umoja na udugu wa kibinadamu zinazofutilia mbali tofauti kwa kumtambua mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Binadamu wote wanategemeana na kukamilishana. Kwa namna ya pekee, Kardinali Turkson anapenda kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya afya ambao wanaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao pamoja na familia zao, ili kuokoa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Wafanyakazi katika sekta ya afya, wanaonesha dira na mwekeo sahihi wa namna ya kumwilisha Fumbo la Pasaka katika uhalisia wa maisha, yaani ni watu wanaojisadaka na kujitoa kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.

Wafanyakazi wa sekta ya afya ni mfano wa Msamaria mwema, wanaoonesha kwa vitendo sadaka na upendo usiokuwa na mipaka. Mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19 inaweza kuwa ni nafasi muafaka ya kutambua na kumwilisha mifumo mipya ya huruma ya Mungu kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuwarejeshea wagonjwa, faraja na matumaini thabiti. Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2020 yanabeba uzito wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kipindi ambacho waamini wengi kutoka katika nchi zilizoathirika kwa Virusi vya Corona, COVID-19 hawawezi kushiriki katika maadhimisho ya Liturujia mbali mbali za Kanisa, hususan maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Lakini kipind hiki cha Kwaresima, waamini wanaweza kuendelea kujikita zaidi katika maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani; kwa kufunga, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ni wakati muafaka wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kuhakikisha kwamba, kila mwamini anawajibika, analinda na kutunza nidhamu pamoja na kutekeleza itifaki dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ni wakati wa kushinda woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto, tayari kujielekeza zaidi katika Injili ya imani, matumaini na mapendo. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano binafsi na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu. Msaada wa hali na mali kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19 upewe kipaumbele cha pekee.

Katika kipeo hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 kuna haja kwa Serikali mbali mbali duniani kukuza na kudumisha haki jamii; kuunga mkono kiuchumi, tafiti mbali mbali dhidi ya magonjwa, ili kupambana na mtikisiko mpya wa uchumi kimataifa. Mama Kanisa kwa upande wake, ataendelea kujisadaka na kujitoa kikamilifu, ili kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa katika sekta afya ili kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19. Hiki ni kipindi cha mshikamano wa huruma na upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kard. Turkson: Corona

 

 

 

11 March 2020, 11:40