Tafuta

Virusi vya Corona, COVID-19: Vatican imeamua kuchuku hatua za dharura ili kuthibiti kuenea kwa Virusi vya Corona ambavyo vimekwisha kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao! Virusi vya Corona, COVID-19: Vatican imeamua kuchuku hatua za dharura ili kuthibiti kuenea kwa Virusi vya Corona ambavyo vimekwisha kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao! 

Virusi vya Corona: Vatican yachukua hatua za dharura!

Kuanzia, Jumapili, tarehe 8 Machi 2020, Baba Mtakatifu ameanza kutoa tafakari yake ya Sala ya Malaika wa Bwana kutoka katika Maktaba yake badala ya kuitolea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama ilivyozoeleka. Katekesi zitakuwa zinatolewa kwa njia ya Video na watu wanaweza kufuatilia Katekesi hizi kwa njia ya luninga pamoja mitandao ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa kuonesha mshikamano wa dhati na uwepo endelevu wa Kanisa karibu na wagonjwa pamoja na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo kwa sasa vinaendelea kupukutisha maisha ya watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Mapambano haya yanapaswa kukita mizizi yake katika: imani, matumaini na mapendo ya dhati kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na ugonjwa huu. Maendeleo makubwa ya sayansi na tiba ya mwanadamu yaendelee kurutubishwa kwa kufunga, sala na maombi; nidhamu na uwajibikaji, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Sekretarieti kuu ya Vatican kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, imeamua kuchukua hatua kadhaa ili kudhibiti kusambaa kwa Virusi vya Corona, COVID-19 ndani na nje ya maeneo ya Vatican. Kumbe, Vatican imeamua kuchukua hatua ya tahadhari ili kuepuka mikusanyiko mikubwa ya watu hasa katika matukio yanayohusisha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko na mji wa Vatican katika ujumla wake. Kuanzia, Jumapili, tarehe 8 Machi 2020, Baba Mtakatifu ameanza kutoa tafakari yake ya Sala ya Malaika wa Bwana kutoka katika Maktaba yake badala ya kuitolea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama ilivyozoeleka. Katekesi kwa Jumatano, zitakuwa zinatolewa kwa njia ya Video na watu wanaweza kufuatilia Katekesi hizi kwa njia ya luninga pamoja mitandao ya kijamii wakiwa majumbani mwao, bila kulazimika kwenda mjini Vatican.

Huduma hii itatolewa na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Kwa vituo vya Televisheni vinavyotaka kupata huduma hii, vinaweza kutuma maombi ili kuwashirikisha watu zaidi katika tafakari hizi hasa katika kipindi hiki kigumu cha wasi wasi na hofu kuu kutokana na kusambaa kwa kasi kubwa kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hizi zote ni jitihada za Vatican kwa kushirikiana na Serikali ya Italia kutaka kudhibiti kuenea kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Kurugenzi ya Afya na Usafi mjini Vatican imeagiza kwamba, kuanzia sasa hadi tarehe 15 Machi 2020 waamini hawataruhusiwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu inayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kutoka katika Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Lakini, Baba Mtakatifu ataendelea kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa faragha, kama kielelezo cha mshikamano na waathirika wote wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Vatican itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali ya Italia ili kutekeleza sera na mikakati iliyobainishwa na Serikali ya Italia kama sehemu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimekwisha kusababisha maafa na madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Ugonjwa wa Virusi vya Corona huenezwa kwa njia ya maji maji yatokayo katika njia ya hewa, au mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya pamoja na kugusa maji maji yatokayo puani, au anapogusana na mtu mwingine mwenye maambukizi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Hatua kadhaa zimechukuliwa ili kudhibiti Virusi vya Corona visiingie mjini Vatican. Kuanzia sasa hadi tarehe 3 Aprili 2020 huduma ya kutembelea Makumbusho ya Vatican na Vituo vya Makumbusho kwenye Makanisa ya Kipapa zimesitishwa.

Taarifa rasmi zinabainisha kwamba, hadi kufikia Jumapili tarehe 8 Machi 2020, kumekuwepo na mtu mmoja tu aliyebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 mjini Vatican. Huyu ni mgonjwa wa nje aliyekuwa anatafuta tiba kwenye Zahanati ya Vatican ambayo kwa sasa imesitisha kutoa huduma kwa wagonjwa. Watu watano waliokutana na mgonjwa huyu kwa sasa wamewekwa chini ya karantini, kwa tahadhari zaidi.

 

 

 

 

 

09 March 2020, 08:12