Vatican News
Vatican: Utu, heshima na haki msingi za walemavu zinapaswa kuheshimiwa na wote sanjari na kushirikishwa katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayowazunguka! Vatican: Utu, heshima na haki msingi za walemavu zinapaswa kuheshimiwa na wote sanjari na kushirikishwa katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayowazunguka!  (AFP or licensors)

Vatican: Walemavu: Utu, heshima na haki zao msingi ziheshimiwe!

Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za walemavu. Kuna haja pia ya kuondokana na mgongano uliopo kati ya kanuni maadili ya kibaiolojia, haki msingi za binadamu pamoja na ulemavu. Jambo la msingi hapa ni kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu, tangu mtoto anapotungwa hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Walemavu ni watu wanaopaswa kupewa tiba, lakini zaidi waonjeshwe upendo, watambuliwe, waheshimiwe na kushirikishwa katika maisha ya jamii inayowazunguka. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kuwaangalia walemavu kwa jicho la imani na kuwashirikisha upendo wa dhati na kwa kufanya hivi watambue kwamba, wanamshirikisha Kristo Yesu mwenyewe anayejitambulisha na ndugu zake walio wanyonge na maskini. Kuna haja ya kuimarisha haki msingi za walemavu na ushiriki wao katika maisha ya kijamii, ili kuondokana na unyanyapaa na hatimaye, kujenga utamaduni wa watu kukutana pamoja na kuwa na maisha bora zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kumekuwepo na maendeleo makubwa kwenye tiba na huduma msingi za binadamu, lakini hata leo hii bado kuna watu wanabaguliwa kiasi cha kushindwa kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Walemavu wanapaswa kusindikizwa katika hatua mbali mbali za maisha yao, kwa kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini utu na heshima yao vikipewa kipaumbele cha kwanza. Walemavu washirikishwe kikamilifu katika maisha ya jamii inayowazunguka. Hii ni hija yenye ugumu na changamoto zake, lakini ni muhimu sana katika kufunda na kuelimisha dhamiri nyofu, ili kutambua utu na heshima ya kila binadamu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, walemavu wanaonekana kuwa kama ni “watu walioko kwenye kifungo cha ndani katika familia na jamii nyingi”.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Ivan Jurkovič mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva nchini Uswis, katika mchango wake kwenye mkutano wa Tume ya Haki ya Umoja wa Mataifa, hivi karibuni, amneitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za walemavu duniani, kwa sababu hata wao wanao mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika mwelekeo huu, kuna haja pia ya kuondokana na mgongano uliopo kati ya kanuni maadili ya kibaiolojia, haki msingi za binadamu pamoja na ulemavu. Jambo la msingi hapa ni kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu, tangu mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Askofu mkuu Ivan Jurkovič anakaza kusema, kanuni, sheria na taratibu hizi zinapaswa kuheshimiwa katika masuala ya teknolojia ya kibaiolojia  na hususan katika sekta ya afya, ili kulinda utu wa binadamu na kwamba, shughuli zote hizi zisiwe ni kwa ajili ya mafao ya kiuchumi na kibiashara zaidi! Hii ni changamoto ya kuondokana na utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba na kifo laini, ambacho kwa wakati huu kinapambwa kwa majina mbali mbali na kusimamiwa hata na sheria za nchi. Hakuna mtu mwenye haki ya kutema zawadi ya uhai kwa sababu maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu ambaye ni bora kuliko mtu mwingine, kumbe, kuna haja ya kuwashirikisha walemavu katika sera na vipaumbele vya jamii husika. Utu, heshima na haki zao msingi ziheshimiwe na kuthaminiwa na wote. Ujasiri na karama mbali mbali walizokirimiwa watu wenye ulemavu zinapaswa kuthaminiwa na kamwe walemavu wasiwe ni vikwazo katika maendeleo, bali wachangiaji katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Walemavu
03 March 2020, 10:45