Tafuta

Vatican News
Sinodi ya Maaskofu Oktoba 2022: Kauli mbiu "Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume" Sinodi ya Maaskofu Oktoba 2022: Kauli mbiu "Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume"  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu 2022: Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume

Sinodi ya XVI ya Maaskofu Mwezi Oktoba 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, ushiriki na utume” Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, katika tamko lake kwa vyombo vya habari amesema kwamba, Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, ushiriki na utume” Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”.

Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Sinodi ya Kanisa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa wa kutaka kutembea kwa pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kama sehemu ya mchakato wa utambulisho wa Kanisa na uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Huu ndio ufafanuzi wa kina uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Sinodi ni chombo cha uinjilishaji unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari na mang’amuzi mbali mbali wanaweza kufikia maamuzi kama ilivyokuwa kwa Mababa wa Mtaguso wa Efeso, walipofikia uamuzi kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”. Mwelekeo wa Kanisa kwa sasa ni dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Sinodi 2022
07 March 2020, 15:23