Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2020: Kauli mbiu "Kama ilivyo kwa Kristo Yesu, alilazimishwa kwenda uhamishoni" Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2020: Kauli mbiu "Kama ilivyo kwa Kristo Yesu, alilazimishwa kwenda uhamishoni" 

Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, 2020: Kauli mbiu! Yesu Alikwenda Uhamishoni

Mama Kanisa ataashimisha Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2020, Jumapili, tarehe 27 Septemba 2020 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Kama ilivyo kwa Kristo Yesu, alilazimishwa kwenda uhamishoni”. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari tema hii na kuchukua hatua thabiti katika utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2020 itaadhimishwa Jumapili, tarehe 27 Septemba 2020 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Kama ilivyo kwa Kristo Yesu, alilazimishwa kwenda uhamishoni”. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari tema hii na kuchukua hatua kama sehemu ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, hadi wakati huu kuna watu zaidi ya watu milioni 41 ambao wanaishi kama wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani inasema, kauli mbiu ya Mwaka 2020 inachota uzoefu na mang’amuzi yake kutoka kwa Kristo Yesu, ambaye wazazi wake, yaani Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, walilazimika kusalimisha maisha yake kwa kukimbilia nchini Misri.

Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha utamaduni wa ukarimu. Ujumbe huu, utatoa ufafanuzi wa kina kuhusu: Kujifunza ili kufahamu; kujenga ujirani mwema ili kuhudumia; kusikiliza ili kujipatanisha; kushirikishana na wengine ili kukua na kukomaa; kuwahusisha wengine, ili kuwaendeleza na hatimaye, kushirikiana ili kujenga. Kutokana na unyeti wa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani kila mwezi, itajitahidi kuhakikisha kwamba, inaendesha kampeni, kwa njia ya tafakari makini, ili kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuweza kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho haya.

Itakumbukwa kwamba, Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, chimbuko lake ni mahangaiko pamoja na mateso ya watu sehemu mbali mbali za dunia kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 na kuanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu. Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, kama sehemu ya sera na mikakati ya Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Tangu wakati huo, Siku hii imekuwa ikiadhimishwa Jumapili baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko kutokana na sababu za kichungaji akaamua Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji iadhimishwe Jumapili ya mwisho wa Mwezi Septemba ya kila mwaka kutoka maombi kutoka kwenye Mabaraza la Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Siku ya 106 Wakimbizi Duniani

 

07 March 2020, 14:43