Tarehe 13 Machi 2020 imegota Miaka 7 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 13 Machi 2020 imegota Miaka 7 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. 

Papa Francisko: Miaka 7 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa!

Kardinali Jorge Mario Bergoglio alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 13 Machi 2013 na kuchagua jina la Papa Francisko, ili kuendelea kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi katika huduma ya: Amani, Maskini na mazingira. Uchaguzi wa Papa Francisko uliwashangaza Makardinali wengi na hii ikawa ni alama ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na Kanisa lake.

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2020 anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; kwa kujikita katika mambo makuu matatu: Maskini, Amani na Mazingira. Anahimiza utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” pamoja utume wa Kanisa miongoni mwa vijana ili kuwajengea leo na kesho yenye matumaini makubwa zaidi. Anasema, Familia ni kitovu cha urithishaji wa imani, maadili na utu wema. Kumbe,  maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika mahojiano maalum na Vatican News, anayaangalia matukio makuu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kipindi cha miaka saba iliyopita. Anasema, aliteuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Kardinali tarehe 24 Novemba 2012 na hivyo kubahatika kushiriki katika Mkutano wa Makardinali “Conclave”, uliomchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio, kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro hapo tarehe 13 Machi 2013 na kuchagua jina la Papa Francisko, ili kuendelea kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kujikita katika huduma ya: Amani, Maskini na Utunzaji bora wa mazingira. Uchaguzi wa Papa Francisko uliwashangaza Makardinali wengi na hii ikawa ni alama ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko alionekana kuinamisha kichwa chini, akiwa na mawazo kede kede, lakini tayari kujiaminisha mbele ya Mungu, ili kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Alipotokeza kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, umati mkubwa wa watu ulivutwa na unyenyekevu wake, hasa pale alipowaomba kusali na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika kipindi cha miaka saba ya maisha na utume wake anasema Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Baba Mtakatifu Francisko ametoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu; maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakipewa kipaumbele cha kwanza. Hata katika mikusanyiko mikubwa ya watu, lakini bado aliweza kumwona mtu mmoja mmoja na kuguswa na mahitaji yake. Baba Mtakatifu anatambua dhamana na wajibu wake kama mchungaji wa watu wa Mungu na wala si “Mkombozi”.

Kardinali Luis Tagle anakiri kwamba, tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2008 wamekuwa wakifanya utume pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wakati ule wakiwa kwenye Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu. Hata baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kuonesha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, maisha ya kawaida, ucheshi na mtu wa kiasi, asiyependa makuu. Ni mtu anayeguswa na maisha ya jirani zake, tayari kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Katika ulimwengu mamboleo, uongozi una changamoto zake kwani hata katika hali na mazingira ya Baba Mtakatifu Francisko bado kuna watu ambao hawaridhiki wala kufurahia upendeleo wake kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na jitihada zake za kuwahamasisha watu wa Mungu kujikita katika mwelekeo wa wongofu wa kiekolojia.

Lakini, ikumbukwe kwamba, upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni changamoto endelevu kutoka katika Maandiko Matakatifu. Ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa kama yalivyomwilishwa na watakatifu, wafiadini na waungama imani wa nyakati mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, na walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu. Ni wajibu na dhamana ya kila mwamini kutumia: karama na vipaji, muda na fursa mbali mbali walizo nazo kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo kwa maskini. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wajenge madaraja na utamaduni wa kukutana na maskini, tayari kuwasaidia katika mahitaji yao ya: kiroho na kimwili.

Waamini watambue kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuzungumza na waja wake hata kwa njia ya maskini! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2019 alimteuwa Kardinali Tagle, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Kabla ya uteuzi huu, Kardinali Tagle alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza waamini kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kanisa linaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa. Dhamana hii, inatekelezwa kwa namna ya pekee, kwa kukutana na Kristo Yesu, Mfufuka, ili kwa njia ya mang’amuzi ya imani, matumaini na mapendo; wamtambue Kristo Yesu kuwa ndiye Mwokozi wa Ulimwengu.

Wakristo wakiwa wamesheheni furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu, wawe tayari kuwashirikisha pia majirani zao. Wahusika wakuu katika mchakato wa uinjilishaji ni Kristo Yesu na Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana! Vingine, mchakato mzima wa uinjilishaji utakuwa ni mradi wa kibinadamu na wala si sehemu ya utume na maisha ya Mama Kanisa. Uinjilishaji mpya unafumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kanisa linawahitaji wamisionari wema, watakatifu na wachapakazi na wala si wafanyakazi. Huu ndio mwelekeo utakaoliwezesha Kanisa kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Kristo kwa walimwengu.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu anahitimisha mahojiano maalum na Vatican News, kwa kumtakia heri na baraka tele Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 7 ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, tayari kuanza mwaka 8 kwa ari na moyo mkuu. Aendelee kugundua na kushuhudia zawadi na ahadi za Mungu kwa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Aendelee kupata faraja katika sala na upendo unaoshuhudiwa kwake na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Itakumbukwa kwamba, Kardinali Tagle alizaliwa tarehe 21 Juni 1957 huko mjini Manila, nchini Ufilippini. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 27 Februari 1982 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Ilikuwa ni tarehe 22 Oktoba 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Imus na kuwekwa wakfu tarehe 12 Desemba 2001.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 13 Oktoba 2011. Na hatimaye, tarehe 24 Novemba 2012, akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Kardinali. Kuanzia tarehe 14 Mei 2015 amekuwa ni Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Biblia vya Kanisa Katoliki  Caritas Internationalis. Na tarehe 8 Desemba 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Propaganda Fide.

Papa: Utume Miaka 7

 

13 March 2020, 14:36