Papa Francisko anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa kwa kuwasindikiza watu wa Mungu kwa: Sala na Sadaka ya Ekaristi Takatifu. Papa Francisko anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa kwa kuwasindikiza watu wa Mungu kwa: Sala na Sadaka ya Ekaristi Takatifu.  Tahariri

Papa Francisko: Miaka 7 ya Maisha na Utume: Virusi vya Corona!

Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuwasindikiza watu wa Mungu kwa sala na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kwa kuwaaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, afya ya wagonjwa. Katika kipindi hiki cha hofu na mashaka, Ibada ya Misa Takatifu inayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Na Padre Richard Mjigwa, - Vatican.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake anasema, tarehe13 Machi 2020 Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 7 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, tayari kuanza miaka 8 hapo tarehe 19 Machi 2020. Baba Mtakatifu anaadhimisha tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, huku hofu na mashaka ya kasi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, ikiwa imetanda sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima: muda wa sala, tafakari kufunga na matendo ya huruma alisema, majivu yanawakumbusha waamini kwamba, wametolewa katika mavumbi, lakini wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, wana thamani kubwa sana mbele ya Mungu kwa sababu wao ni matumaini ya Mungu, amana na furaha yake. Majivu yanawakumbusha waamini kwamba, safari ya maisha yao inaanza katika mavumbi, changamoto na mwaliko wa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaunda.

Kwa bahati mbaya mwanadamu anapokabiliwa na shida, magumu na changamoto za maisha mbele yake anaona mavumbi peke yake. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwatia shime kwamba, hata katika hali hii bado wanayo thamani kubwa mbele ya macho yake. Hii inatokana na ukweli kwamba, mwanadamu amezaliwa kwa ajili ya kupendwa na kwamba, wao ni watoto wa Mungu. Dr. Andrea Tornielli anafafanua kwamba, huu ni mwaliko wa nguvu kwa watu wa Mungu kuelekeza macho yao ya imani katika mambo msingi ya maisha, kama ambavyo siku hii ilivyoadhimishwa, tofauti na miaka mingine iliyopita. Hiki ni kipindi kigumu ambacho waamini wengi wameguswa na kutikiswa katika undani wa maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuwasindikiza watu wa Mungu kwa sala na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kwa kuwaaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, afya ya wagonjwa. Katika kipindi hiki cha hofu na mashaka, Ibada ya Misa Takatifu inayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican inatangazwa moja kwa moja sehemu mbali mbali za dunia kwa kutumia njia mbali mbali za mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Baba Mtakatifu ambaye kimsingi ndiye “Baba Paroko” wa Kanisa la Kiulimwengu, anatoa mahubiri yake kwa waamini wachache, ili kuwashirikisha mang’amuzi yake kuhusu Neno la Mungu kwa siku hiyo. Huu ni upya katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Mahubiri haya ya siku kwa siku, yamekuwa ni chemchemi ya faraja kwa waamini na watu wengi katika kipindi cha miaka saba ya maisha na utume wake. Muhtasari wa mahubiri ya Baba Mtakatifu umekuwa ukitolewa na vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Baba Mtakatifu anaendelea kumtolea Mwenyezi Mungu, mateso na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea: wagonjwa na familia zao; wafanyakazi na wahudumu katika sekta ya afya; watu wa kujitolea; walemavu na wazee wanaokabiliana na upweke; wafungwa na viongozi mbali mbali wa Serikali. Faraja hii inayobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhimu sana kwa wakati huu wa ukame wa maisha ya kiroho, kumbe maadhimisho haya yanakuwa ni faraja

Papa Francisko anasema, leo hii watu wengi wanarudishwa mavumbini kutokana na: milipuko ya magonjwa majanga, vita, vitendo vya utoaji mimba pamoja na wazee kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Watu wanarejeshwa mavumbini kutokana na mahusiano tenge ndani ya familia, kinzani na mipasuko mbali mbali; kwa kukosa kuomba na kutoa msamaha wa kweli, tayari kuanza maisha mapya. Lakini kwa bahati mbaya, watu wengi ni wepesi kudai haki zao na wala hawana upendo wa dhati; mambo yanayohatarisha zawadi ya maisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, haitoshi kutenda matendo ya huruma, kusali na kufunga, ikiwa kama bado kuna watu wanatawaliwa na unafiki pamoja na ubinafsi. Kwa hakika maneno yanapaswa kudhihirishwa kwa vitendo!

Mawazo ya ndani yadhiirishwe kwa njia ya maisha ya nje, ili kweli mavumbi yasichafue na wala majivu yasizime moto wa upendo wa Mungu. Ni katika muktadha wa mazingira haya, Mtume Paulo anasema: “twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu”. Baba Mtakatifu anawakumbusha tena waamini kwamba, wao ni mavumbi, lakini wanapendwa na Mwenyezi Mungu, kwani wao ni matumaini, amana na utukufu wake. Upatanisho na Mungu utawasaidia kuishi kama watoto wapendwa wa Mungu; wadhambi waliosamehewa; wagonjwa walioponywa, na waliopotea njia, kupata kiongozi. Waamini wajiachilie mbele ya Mwenyezi Mungu ili awapende nao waweze kupenda. Wawe na ari ya moyo wa kusimama kuelekea katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Kwa njia hii watakuwa na furaha ya kugundua kwamba, Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuwafufua tena kutoka katika majivu yao!

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 10 Machi 2020 katika Ibada ya Misa Takatifu alisali kwa namna ya pekee, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre, ili katika Kipindi hiki tete cha maisha na utume wa Kanisa, wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na faraja ya Mungu kwa waja wake. Wawe na ujasiri wa kutoka na kuwaendelea wagonjwa, ili kuwapatia faraja ya nguvu ya Neno la Mungu pamoja na Ekaristi Takatifu. Wawasindikize wafanyakazi na wahudumu katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika kipindi hiki tete cha maisha ya watu wengi duniani.

Tahariri

 

13 March 2020, 14:07