Vatican: Mabadiliko ya Mfumo wa Elimu Kimataifa:" Global Compact on Education" sasa kutiwa saini hapo tarehe 15 Oktoba 2020 Vatican: Mabadiliko ya Mfumo wa Elimu Kimataifa:" Global Compact on Education" sasa kutiwa saini hapo tarehe 15 Oktoba 2020 

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa kutiwa saini 15 Oktoba 2020

Kwa sasa tukio hili la kihistoria litaadhimishwa kuanzia tarehe 11-18 Oktoba 2020 na Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” utatiwa mkwaju hapo tarehe 15 Oktoba 2020. Taarifa hii imetolewa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki ambalo limekabidhiwa dhamana ya kuratibu matukio haya. Lengo la Papa ni kujenga Mfumo Mpya wa Elimu Fungamanishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969 alizindua Mpango mkakati wa mwaka 2020, tukio la kimataifa ambalo lilikuwa limepangwa kuzinduliwa rasmi hapo tarehe 14 Mei 2020, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya Mfumo wa Elimu Kimataifa”. Kwa sasa tukio hili la kihistoria litaadhimishwa kuanzia tarehe 11-18 Oktoba 2020 na Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” utatiwa mkwaju hapo tarehe 15 Oktoba 2020. Taarifa hii imetolewa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki ambalo limekabidhiwa dhamana ya kuratibu matukio haya. Mabadiliko haya ni kutokana na kuenea kwa kasi kubwa kwa Virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia.

Ni matumaini ya Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kwamba, hali itakapokuwa shwari, kutakuwepo na ushiriki mkubwa zaidi wa wadau wa elimu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hili ni tukio ambalo linalenga kuzishirikisha taasisi za elimu, wasomi na wanazuoni; viongozi wa kidini, mashirika ya elimu kimataifa, wanasiasa, wachumi na wadau katika sekta ya utamaduni na sanaa. Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki linaendelea kufanya mchakato wa utekelezaji wa matukio haya mintarafu nia njema ya Baba Mtakatifu Francisko. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti, kwa kujikita katika elimu fungamanishi inayowataka vijana kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa elimu itakayosaidia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiekolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ndio mwelekeo pia wa tukio la "Economy of Francesco" yaani "Uchumi wa Francisko” ambalo kwa sasa litaadhimishwa hapo tarehe 21 Novemba 2020.

Baba Mtakatifu anataka kuzama zaidi katika uchumi unaouhisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaokita mizizi yake katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu hali ambayo imesababisha hata kinzani na mabadiliko si tu katika masuala ya kitamaduni bali pia kuhusiana na elimu ya binadamu, kwa kuunda lugha mpya ambayo inawatenga watu na kudhohofisha dhana ya elimu ya jadi. Leo hii kuna kile kinachoitwa mchakato wa mwendokasi wa elimu unaofumbatwa katika kasi kubwa ya teknolojia na matumizi ya komputa yanayokinzana na kasi ndogo ya mabadiliko ya kibaiolojia.

Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika elimu unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote kadiri ya dhamana zao wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi kwa ajili ya ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa elimu. Kuna umuhimu wa kuanzisha kijiji cha elimu kabla ya kuanza kutoa elimu, kwa kuandaa mazingira ya udugu wa kibinadamu pamoja na kuondokana na ubaguzi. Kijiji cha elimu anasema Baba Mtakatifu ni jukwaa ambalo inakuwa rahisi kuweza kufikia muafaka wa elimu fungamani inayomheshimu binadamu na kuunganisha masomo na hali halisi ya maisha kati ya wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, michezo, siasa, biashara na wenyeji wote wa nyumba ya wote. Ili kuweza kufikia ujenzi wa kijiji cha elimu, kwanza kabisa binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kukazia mifumo rasmi na isiyo rasmi ya elimu, ili kuwa na mwelekeo wa pamoja kuhusu: elimu ya binadamu, uchumi, siasa, ukuaji na maendeleo fungamani.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisadaka bila ya kujibakiza ili kutengeneza mtandao utakaowawezesha kushirikishana: ujuzi, elimu, maarifa, weledi pamoja na kipaji cha ugunduzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, udugu na majadiliano, tayari kupandikiza mbegu hizi, ili ziweze kukua na kukomaa, kwa njia ya uongozi makini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Vijana wanakumbushwa kwamba wao ni leo ya Mungu, wanayopaswa kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao; kwa kushirikiana na wengine ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi.

Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa

 

 

05 March 2020, 13:55