Tafuta

Vatican News
Mafungo ya Kiroho: Wito wa Musa mtumishi wa Mungu ulipania kuwakomboa Waisraeli kutoka katika utumwa, dhuluma na nyanyaso ili kulinda utu na heshima yao kama binadamu! Mafungo ya Kiroho: Wito wa Musa mtumishi wa Mungu ulipania kuwakomboa Waisraeli kutoka katika utumwa, dhuluma na nyanyaso ili kulinda utu na heshima yao kama binadamu! 

Mafungo ya Kiroho: Wito wa Musa: Utu na Haki msingi za binadamu!

Mwenyezi Mungu alimteua na kumtuma Musa kwenda kwa Farao, ili apate kuwaokoa watu wake, hao wana wa Israeli katika Misri. Haki msingi za Waisraeli waliokuwa ugenini, wakinyanyaswa na kunyonywa, zinapewa kipaumbele katika wito, maisha na utume wa Musa. Hii ndiyo changamoto mamboleo inayopaswa kudumishwa kwa ajili ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hatua ya kwanza katika maisha ya sala na tafakari inajengwa katika mazingira ya kufahamiana kwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kama inavyokaziwa kwenye maisha ya kiroho. Huu ni mchakato unaomwezesha mwamini kuona na kuonja mpango wa upendo na ukarimu wa Mungu unaotekelezwa katika maisha ya mwanadamu. Ukimya unarutubisha maisha ya sala na tafakari ya kina!  Tafakari wakati wa mafungo maisha ya kiroho kwa wasaidizi wa karibu wa Baba Mtakatifu, “Curia Romana” kuanzia tarehe 1 Machi hadi 6 Machi, 2020 huko Ariccia nje kidogo ya mji wa Roma, inaongozwa na Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Kauli mbiu ya mafungo haya ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”.

Utamaduni wa kumsikiliza Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mtu ni mang’amuzi ya kinabii kama yanavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Vielelezo vikuu hapa ni kijiti kilichokuwa kinawaka moto pamoja na Neno la Mungu lililokuwa linatoka katika moto huu na kuiangazia njia hii ya maisha. Padre Pietro Enrico Bovati, anasema wito ni mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaohitaji jibu linalofumbatwa katika katika usikivu na utii, ili kuanza kutembea katika njia mpya ya maisha au kwa maneno mengine ni kuzaliwa upya kunakomwezesha mtu kuunda udugu mpya wa kibinadamu. Haya ni mambo msingi katika maisha ya Sala. Musa mtumishi wa Mungu ni mfano wa mtu anayesikiliza na hatimaye kujibu kwa utii wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Musa alikuwa ni mtu wa kawaida tena mchungaji, anateuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni kiongozi wa Waisraeli, katika maisha ya kiroho.

Mwenyezi Mungu katika mpango wake wa daima, alimwandaa Musa ili aweze kutekeleza dhamana na wajibu wake mpya, kwa kumtaka ajitoe sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa ndugu zake. Musa hakujua mahali alipotakiwa kwenda, pale alipokuwa anazungumza na Mwenyezi Mungu katika kijiti cha moto, kielelezo cha ufunuo wa Mungu na chemchemi ya maisha na wito wa kinabii. Musa akajibu na kuitikia “Mimi hapa Bwana”. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Daudi, mpakwa mafuta wa Bwana, alivyomtwanga Goliathi na hivyo kushuhudia ukuu wa Mungu kwa njia ya mtumishi wake Daudi. Nabii Yeremia alipoitwa na Mwenyezi Mungu alitaka kupinga wito huo kwa kujisingizia kwamba, bado alikuwa ni kijana sana! Jambo la kushangaza, huyu ndiye aliyeteuwa na Mungu kutangaza na kushuhudia uwepo wa Mungu kati ya waja wake.

Maandiko Matakatifu hayatoi ufafanuzi wa kina kuhusu kile kijiti kilichokuwa kinawaka moto bila kuteketea, kuwa ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, unaomtia Musa ari na nguvu ya kutekeleza utume wake. Kwa upande mwingine, kijiti hiki ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu. Moto kadiri ya Maandiko Matakatifu ni kielelezo cha nguvu ya Mungu. Krisdto Yesu katika Agano Jipya anawafafanulia wafuasi wake utambulisho wake kuwa ni “Mwana wa Mungu, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu” kama inavyoshuhudiwa kwenye kiri ya imani ya Mtakatifu Petro. Hili ni jibu linalobubujika kutoka katika maisha na mang’amuzi ya mwamini binafsi. Kumbe, wito unapata chimbuko lake katika moyo wa mtu binafsi na unaomwajibisha mtu binafsi.

Kwa njia hii, mwamini anaonja mabadiliko ya ndani katika maisha yake, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Kristo Yesu, na kwa namna ya pekee Petro mtume, hata katika udhaifu wake wa kibinadamu, lakini bado neema ya Mungu iliweza kumwinua juu na kuwa ni Mwamba wa Kanisa! Wafanyakazi wa “Curia Romana” wamekumbushwa kwamba, kama Petro wamepewa dhamana na majukumu mazito katika maisha na utume wa Kanisa, lakini wanahimizwa kujikana wenyewe, kujitwika Misalaba yao na kufumasa Kristo Yesu katika ile Njia ya Msalaba, kwa kutambua kwamba, umoja na upendo wa Mungu unawasindikiza na kuwaambata daima!

Padre Pietro Enrico Bovati baada ya kufafanua kuhusu wito wa Mungu, amebainisha kwamba, Mwenyezi Mungu alimteua na kumtuma Musa kwenda kwa Farao, ili apate kuwaokoa watu wake, hao wana wa Israeli katika Misri. Haki msingi za Waisraeli waliokuwa ugenini, wakinyanyaswa na kunyonywa, zinapewa kipaumbele cha pekee katika wito, maisha na utume wa Musa. Hii ndiyo changamoto mamboleo inayojionesha hata miongoni mwa Wakristo kwa kukengeuka na kumezwa na malimwengu; kwa ukanimungu na kutopea katika dhambi na udhaifu wa maisha ya kiroho. Hata leo hii, bado kuna akina Farao wanaojibu kwa dharau, kejeli na kipigo kwa wale wote wanaojitokeza kusimama kidete kudai: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hii ni changamoto ambayo wakati mwingine pia inajitokeza hata katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutumia nguvu kubwa kupambana na watu; kwa kuendekeza malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko; kwa kutumia nguvu ya rasilimali fedha; mambo ambayo yanaweza kulitumbukiza Kanisa kiasi cha kumezwa na malimwengu, kinyume kabisa cha mapenzi ya Mungu. Leo hii kuna tabia kubwa ya kukataa kutekeleza mapenzi ya Mungu wala kusikiliza sauti ya kinabii, kielelezo cha kiburi cha binadamu na utepetevu wa mawazo pamoja na ubinafsi. Watu wengi wanaendelea kumezwa na malimwengu kwa kupinga kimasomaso Mafundisho ya Kanisa.

Viongozi wenye dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu wanapaswa kujiuliza katika misingi ya ukweli na uwazi, mchango wao katika kurekebisha mitazamo hii. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani katika maisha na utume wa Kanisa. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya viongozi wa Kanisa wanajificha nyuma ya pazia la:Mapokeo ya Kanisa, Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa kwa ajili ya mafao yao binafsi. Mchakato wa mageuzi ndani ya Kanisa katika masuala ya kitaalimungu na taasisi za Kanisa, Lituturujia, Katekesi na shughuli za kichungaji ni sehemu muhimu sana ya Kanisa katika kusoma alama za nyakati. Katika hali na mazingira kama haya, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuweza kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuzifanyia kazi katika maisha na utume wa Kanisa.

Mfano wa mpanzi unadhihirisha nguvu ya Mungu inayobubujika kutoka katika Neno lake. Kwa upande mwingine, linaonesha jinsi ambavyo baadhi ya waamini wanavyokataa kupokea neema ya Mungu kutokana na wivu pamoja na ubinafsi unaowafana baadhi ya viongozi kudhani kwamba wao ni bora zaidi kuliko wengine. Unyenyekevu na kiasi ni silaha madhubiti za kuweza kupokea upendo wa Mungu kwa ajili ya huduma na majitoleo endelevu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa!

Mafungo ya Kiroho

 

 

04 March 2020, 11:30